Basil Mramba (71), Waziri mwandamizi
aliyetumikia awamu nne zote za nchi hii katika wizara mbalimbali, jana
alianza kujitetea dhidi ya kesi ya matumizi mabaya ya ofisi na kumtaja
Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, kuwa ndiye aliyemuagiza kutoa msamaha wa
kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart.
Katika kesi hiyo anayodaiwa kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni
11.7, kwa misamaha ya kodi, pia alidai kuwa Mkapa alimuagiza
kuhakikisha gharama za kuilipa Kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) ya
Uingereza iliyoingia mkataba wa ukaguzi wa madini kupitia kampuni tanzu
ya Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation, zinatoka
ndani ya serikali au Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mramba wakati huo akiwa Waziri wa Fedha, alidai kuwa Mkapa alitoa amri
ya kufanya mchakato wa kuileta nchini kampuni hiyo kwa aliyekuwa Gavana
wa BoT wakati huo, marehemu Daud Bilali, baada ya kushinda zabuni.
Mramba ambaye ni mshitakiwa wa kwanza kati ya washitakiwa watatu, alitoa
ushahidi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, jijini Dar es
Salaam huku akiongozwa na mawakili wa utetezi, Herbert Nyange
akisaidiana na Peter Swai mbele ya jopo la mahakimu watatu wakiongozwa
na Jaji John Utamwa na Sam Rumanyika wa Mahakama Kuu.
Majaji hao wamepewa kibali na Jaji Mkuu kuendelea kusikiliza kesi hiyo
wakisaidiana na Hakimu Saul Kinemela. Majaji hao walianza kusikiliza
kesi hiyo mwaka juzi wakati huo wakiwa mahakimu.
Mramba ambaye pia ni shahidi wa kwanza wa upande wa utetezi, aliiambia
Mahakama hiyo kuwa anatarajia kuita mashahidi watano ambao ni aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo, Andrew Chenge; mwakilishi wa
kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS), Erwin Florence; aliyekuwa Gavana wa
BoT (wakati huo), Daud Balali au atakayemteua kumwakilisha mahakamani
hapo; Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC), John Cheyo na Mshauri wa Masuala ya Kodi, Florian Msigala.
Mbali na mashahidi hao watano, Mramba aliiambia Mahakama kuwa shahidi
wake wa sita bado hajathibitisha, lakini wakati wowote atatoa jibu la
kufika kwake mahakamani hapo.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Mramba wakati akiongozwa na Wakili Nyange:
Wakili Nyange: Shahidi chimbuko la kesi hii ni nini?
Mramba: Chimbuko la kesi ni malalamiko yaliyokuwepo bungeni, kwa
wananchi na vyombo vya habari kuhusu Tanzania kutokufaidika na migodi
yake.
Kwamba kulikuwa na baadhi ilikuwa inadanganya juu ya uzalishaji wao na
uuzaji wao wa madini aina ya dhahabu kuwa ulikuwa haueleweki vizuri
kwenye soko la nje.
Wakili Nyange: Tatizo lilianzia wapi na kwa nini uko hapa mahakamani?
Mramba: Niko hapa mahakamani kwa sababu ya mashtaka yanayonikabili.
Nilipokuwa Waziri wa Fedha, nilitoa msamaha wa kodi kwa Kampuni tanzu ya
Alex Stewart (ASSAYERS) iliyoletwa nchini na serikali kufanya ukaguzi
wa migodi ya madini ya dhahabu pamoja na kukusanya maoni juu malalamiko
ya watu.
Wakili Nyange: Nani aliialika Kampuni tanzu ya Alex Stewart (ASSAYERS) hapa nchini?
Mramba: Serikali ilitoa maagizo kwa BoT kumtafuta mkandarasi anayefaa
ili aweze kufanya kazi hiyo na iliingia mkataba na Kampuni tanzu Alex
Stewart (ASSAYERS) ambayo iko kwenye kundi la Kampuni ya Alex Stewart
(ASSAYERS) ya Uingereza.
Wakili Nyange: Nani aliiagiza BoT?
Mamba: Rais wa awamu ya tatu, Mkapa.
Wakili Nyange: Shahidi, wewe ulikuwa na cheo gani wakati huo?
Mramba: Waheshimiwa mahakimu, wakati huo mimi nilikuwa ni Waziri wa Fedha.
Wakili Nyange: Ukiwa kama Waziri wa Fedha ulipewa jukumu gani?
Mramba: Nikiwa kama Waziri wa Fedha wakati huo, Rais Mkapa aliniagiza
nihakikishe garama za kuilipa kampuni hiyo ya ushauri wa ukaguzi wa
madini zinafanywa ndani ya serikali au BoT.
Wakili Nyange: Nani alikuwa anawajibika kwa mwenzake kati yako na Gavana (wakati huo Balali)?
Mramba: Hakuna, siyo mimi wala Gavana aliyekuwa anawajibika kwa mwenzake, kila mtu aliwajibika moja kwa moja kwa Rais.
Wakili Nyange: Nani kati yako na Gavana alikuwa na wajibu wa kuileta kampuni ya kufanya ukaguzi huo?
Mramba: Gavana.
Wakili Nyange: Je, zoezi hilo alilolifanya Gavana ni nani alimtafuta mshauri huyo?
Mramba: Mimi sikuhusika kumtafuta mshauri.
Wakili Nyange: Ushahidi wa Jamhuri ulisema kulikuwa na timu ya kuichagua
Kampuni tanzu ya Alex Stewart (ASSAYERS). Je, ulihusika?
Mramba: Sikuhusika wala sikutuma mtu kwenda kuniwakilisha katika timu hiyo.
Wakili Nyange: Ulifahamu vipi kama kampuni hiyo imeteuliwa?
Mramba: Nilifahamu baada ya kuarifiwa na Gavana na Katibu Mkuu, Gray Mgonja, wakati tunajadili maendeleo ya mkataba huo.
Wakili Nyange: Wizara ya Fedha ilikuwa na mamlaka gani katika mchakato huo?
Mramba: Sifahamu.
Wakili Nyange: Mkataba wa makubaliano ulisainiwa na nani?
Mramba: Waheshimiwa mahakimu ni Gavana.
Wakili Nyange: Je, shahidi unaweza kuieleza Mahakama mkataba wa makubaliano ulisainiwa kati ya nani na nani?
Mramba: Mkataba wa makubaliano ulisainiwa kati ya Gavana Balali na
Makamu wa Rais wa Kampuni tanzu ya Alex Stewart (ASSAYERS), Florence.
Wakili Nyange: Kama siyo wewe, Gavana asingesaini mkataba huo ni kweli au siyo kweli?
Mramba: Mimi na Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (wakati huo),
kazi yetu kwenye mkataba huo tulikuwa mashahidi tu ili uweze
kutekelezwa.
Shahidi huyo alitaka kuwasilisha mahakamani nakala ya barua
aliyomwandikia Yona. Hata hivyo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili
wa Serikali Mkuu, Fredrick Manyanda, alipinga barua hiyo kupokelewa kwa
madai kuwa ni nakala na kuomba iwasilishwe barua halisi.
Wakili Nyange alidai kuwa mshitakiwa aliwasilisha orodha ya kuomba
nakala halisi ya barua Desemba 2009, lakini hadi jana upande wa Jamhuri
ulidai kuwa haujapata barua hiyo halisi.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi leo Jopo hilo litakapotoa uamuzi wa ama
kuipokea au kuikataa nakala ya barua ya Mramba kwenda kwa Yona. Pia
Mramba ataendelea kutoa utetezi wake.
Mashahidi waliotajwa na Mramba mahakamani hapo, pia watawatetea washtakiwa wenzake kwenye kesi hiyo ambao ni Yona na Mgonja.
Mapema saa 4:45 asubuhi, ukumbi namba moja wa Mahakama hiyo ulifurika
watu waliofika kusikiliza utetezi wa washtakiwa hao ambao walikuwa
viongozi waandamizi wa serikali.
Saa 5:10 asubuhi, jopo la mahakimu liliingia na Mramba alipanda
kizimbani na kuanza kutoa utetezi wake baada ya kiapo, akiwa amevaa suti
ya rangi nyeusi ya mikono mifupi na viatu vyeusi.
Katika kesi ya msingi, washitakiwa wanadaiwa kuwa kati ya Agosti mwaka
2002 na Juni 14 mwaka 2004, jijini Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa
umma kama mawaziri na katibu mkuu, walitumia vibaya madaraka yao.
Ilidaiwa kuwa kwa kupitia kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) ya
Uingereza iliyoingia mkataba wa ukaguzi wa madini kupitia kampuni tanzu
ya Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation, waliingia
mkataba kukagua kiwango cha uzalishaji wa madini ya dhahabu kinyume cha
Sheria ya Manunuzi ya Umma.
No comments:
Post a Comment