Wednesday, August 22, 2012

SELIKALI YAPEWA SIKU SABA KULIFUNGULIA MWANAHALISI

SIKU chache baada ya Gazeti la MwanaHalisi kufungiwa kwa muda usiojulikana, Serikali imepewa siku saba kuhakikisha inalifungulia bila masharti yoyote kwa sababu ya kuandika habari zinazomuhusu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dkt. Steven Ulimboka.

Mwenyekiti wa Kamati ndogo iliyoundwa baada ya Serikali kulifungia gazeti hilo, Bw. Marcossy Albanie, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema kama Serikali itashindwa kufanya hivyo, asasi mbalimbali za kiraia zitaitisha maandamano makubwa nchi nzima kupinga hatua ya kufungiwa gazeti hilo bila sababu za msingi.

Aliongeza kuwa, maandamano hayo yataitishwa na wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu pamoja na waandishi wa habari kwani sheria iliyotumika kulifungia gazeti hilo ni kandamizi.

"Serikali imelituhumu gazeti hilo kwa kuchapisha habari ambazo zinakiuka vifungu vya sheria ya magazeti namba tatu ya mwaka 1976, habari iliyoandikwa inahusu kutekwa kwa Dkt.Ulimboka, kuteswa na kutupwa katika Msitu wa Mabwepande,"alisema.

Bw. Albanie alisema Serikali imetumia mabavu kulifungia gazeti hilo kwani hawakutaka kusikiliza upande wa pili ambapo Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, anafahamu sheria iliyotumika ni ya kikatili na imepitwa na wakati.


"Serikali itekeleze haraka suala hili ndani ya siku saba, asasi za kijamii hazikubaliani na kauli ya Bw. Pinda ya kutaka wahusika waende kwenye vyombo vya juu kwa sababu sheria ya magazeti hairuhusu ukataji rufaa kwa Waziri wa Habari ambaye ndiye aliyetuhumu na kutoa hukumu,"alisema.

Aliongeza kuwa, Bw. Pinda hakusema kama amepokea malalamiko ya gazeti hilo kuandika habari ya kichochezi hivyo hiyo ni njia mojawapo ya kukwepa wajibu wake.

"Serikali inashinikiza MwanaHalisi waende mahakamani wakati kesi nyingi zinacheleweshwa zikiwa huko hivyo hali hiyo itasababisha gazeti hili kutopata haki," alisema Bw. Albanie.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA), Bw. Tumaini Mwailenge, aliitaka Serikali kulishughulikia tatizo hilo haraka na kuondokana na sheria kandamizi kwa vyombo vya habari.
Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia suala la kufungiwa kwa Gazeti la Mwanahalisi, Bw. Marcossy Albanie (katikati) akitoa tamko  kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), Dar es Salaam jana, kuitaka Serikali ilifungulie gazeti hilo ndani ya siku 7. Kushoto ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA-Tan), Bw. Mohammed Tibanyendera na Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Bw. Tumaini Mwailenge

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake