Wednesday, August 22, 2012

SHEKHE ALIYESHAWISHI WAISLAMU KUTOSHILIKI SENSA AKAMATWA TANGA

JESHI la Polisi Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, linamshikilia Shekhe Juma Koosa (52), mwenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za kutumia kipaza sauti akiwa msikitini na kuwatangazia waumini wa Kiislamu wasishiriki Sensa ya Watu na Makazi.

Shekhe Koosa ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Kiislamu mkoani Morogoro, alikamatwa Agosti 19, mwaka huu katika Msikiti wa Miembeni, uliopo Mazinde baada ya kukaribishwa na wenyeji wake.

Baada ya kukaribishwa na wenyeji wake, Shekhe Koosa alieleza sababu za kuwataka Waislamu wasishiriki sensa na kusoma ujumbe ulioandikwa na Bw.Matimba kupitia kitabu chake chenye kurasa 31.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Bw.Constantine Massawe, alithibitisha kukamatwa kwa Shekhe Koosa ambaye alikutwa na nakala 10 za kitabu alichokuwa akikitumia kuhamasisha Waislamu wasishiriki sensa iliyopangwa kuanza usiku wa kuamkia Agosti 26, mwaka huu.

"Kukamatwa kwa mtu huyu kulitokana na taarifa zilizotolewa na baadhi ya wananchi ambao miongoni mwao ni waumini wa Kiislamu ambao walihisi kuchanganywa na taarifa hizo.

"Wakati Shekhe Koosa akitoa taarifa yake, baadhi ya waumini walikubaliana naye lakini wengine walimpinga hivyo ukatokea mtafaruku ndipo wale wenye dhamira ya kushiriki sensa wakatoa taarifa polisi ambao walikwenda kumkamata," alisema.

Alisema baada ya kukamatwa, alipelekwa Kituo cha Polisi Mombo kwa mahojiano na kudai kuwa, kile alichokuwa akikisema hakujua kama kilikuwa na madhara pia ni kinyume cha sheria za nchi.

Aliongeza kuwa, baada ya mahojiano Shekhe Koosa alihamishiwa Kituo cha Polisi Wilaya ya Korogwe, kutokana na tishio la baadhi ya Waislamu kutaka kuandamana ili kupinga kukamatwa kwake.

"Tunatarajia kumfikisha Mahakamani wakati wowote baada ya taratibu za kuandaa mashtaka kukamilika, naomba watu wengine wanaohamasisha wenzao kutoshiriki sensa waache mara moja," alisema Kamanda Massawe.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake