ames Magai
WAKILI wa mshtakiwa katika kesi ya kughushi wasia wa marehemu na kisha kuwasilisha mahakamani nyaraka feki, juzi alimweka katika wakati mgumu mshtakiwa huyo, baada ya kushindwa kufika mahakamani bila taarifa. Mshtakiwa katika kesi hiyo ni mwalimu Janeth Mahunguhungu (50) wa Shule ya Msingi Wabegi, iliyoko Bunju wilayani Kinondoni.
Shahidi huyo pia ni mwanasheria ambaye alitarajiwa kutoa ushahidi kwa upande wa mshtakiwa, lakini si yeye wala wakili wake waliojitokeza mahakamani, hatua iliyoilazimisha mahakama kutoa onyo la kuwataka wasichezee muda. Hata hivyo, Hakimu Mkazi, Othman Kasailo anayeisikiliza kesi hiyo aliamua kuahirisha kesi hiyo hadi Alhamisi ijayo na kutoa nafasi ya mwisho kwa mshtakiwa, kuhakikisha kuwa shahidi na wakili wake wanakuwepo mahakamani.Hata hivyo, kabla ya kuahirisha kesi hiyo, hakimu alimuuliza mshtakiwa kuhusu shahidi wake.
Katika maelezo yake, mshtakiwa alidai kuwa alikuwa katika maeneo ya Kariakoo, akiwa njiani kwenda mahakamani na kwamba hakuwa na mawasiliano na wakili wake.Majibu hayo yalionyesha kumkera Hakimu ambaye alihoji sababu za shahidi ambaye ni mwanasheria, kushindwa kufika mahakamani kwa wakati.
“Shahidi wako ni mwanasheria, anajua taratibu za mahakamani iweje hadi sasa hivi saa tano bado hajafika,” alihoji Hakimu Kasailo kwa hali ya kuchukizwa na kitendo hicho.Kesi hiyo imekuwa ikikwama kuendelea na kulazimika kuahirishwa mara kwa mara kutoka na wakili wa mshtakiwa huyo, Majura Magafu na mashahidi kutofika mahakamani.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 1161/ ya mwaka 2011, mshtakiwa anakabiliwa na tuhuma za kughushi wasia wa marehemu na kuwasilisha mahakamani.Inadaiwa kuwa mshtakiwa alighushi wasia unaoonyesha kuwa ulitolewa na kusainiwa na marehemu Tijani Mzee Mahunguhungu Aprili 25 mwaka 2003, akitambua mshtakiwa kuwa ndiye mrithi wa mali zote za marehemu.
Pia inadaiwa kuwa Januari 26 mwaka 2007 mshtakiwa aliwasilisha katika Mahakama ya Mwanzo, maelezo ya uongo na nyaraka za kughushi.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka, akiwemo mtaalamu wa maandishi, mahakama iliridhika kuwa mshtakiwa ana kesi ya kujibu na kwamba atapaswa kujitetea.
Katika ushahidi wake, wakati akijitetea mshtakiwa alidai kuwa aliolewa na marehemu kwa ndoa ya kimila mwaka 1982 na baadaye wakafunga ndoa ya kiserikali.
Alidai kuwa katika ndoa yao, walibahatika kuzaa watoto watano.Alidai kuwa baada ya kifo cha mumewe, kikao cha ukoo kilimteua yeye kuwa mrithi wa mali za marehemu kwa kuzingatia wasia aliouacha marehemu.
Pia aliwasilisha mahakamani vielelezo mbalimbali ambavyo hata hivyo vilizua mvutano mkali na upande wa mashtaka ambao ulidai kuwa ni vya kughushi.
Vielelezo hivyo ni pamoja na muhtasari wa kikao cha familia na ndugu wa marehemu, alichodai kuwa kilimteua yeye kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu.
Kielelezo kingine ni cheti cha kifo cha marehemu ambacho pia kilizua mvutano wa hoja baada ya upande wa mashtaka, kukipinga ukidai kuwa ni cha kughushi.Hata hivyo mahakama ilivitupilia mbali vielelezo hivyo baada ya kuwekewa pingamizi na upande wa mashtaka kuwa ni vya kughushi.
“Kuna majina mengine hapa ya wajumbe ambayo yameandikwa kwa mkono na wengine kama huyu mjumbe namba 19 Mayasa Hamad, ambalo nalo limeandikwa kwa mkono ni marehemu na alifariki hata kabla ya marehemu Tijani hajafariki,” alidai wakili Magoma.
Alidai kuwa upande wa mashtaka ndiyo wenye cheti halisi cha kifo cha marehemu, kibali cha mazishi na tangazo la kifo cha marehemu.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment