Boniface Meena
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), kimemshtaki Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, ili aweze kujieleza kuhusu madai kuwa Chadema imekuwa ikitumia harambee zao kuhalalisha mabilioni ya fedha wanazopewa na wafadhili nje ya nchi.
Pia, chama hicho kimesema kuwa kimepeleka nakala kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, kutaka jeshi lake lishughulikie shutuma hizo na pia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi katika vyama.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Anthony Komu, alipokuwa akizungumza na gazeti hili kuhusu madai yaliyotolewa na Nnauye, dhidi ya chama chake.Komu alisema chama chake, hakijawahi kufadhiliwa na wahisani kutoka nje na kwamba mapato yake yanatokana na ruzuku ya Sh235 milioni inayotolewa na Serikali kila mwezi.
“Tumekuwa tukipata fedha kutokana na michango ya wanachama wetu ya kila mwaka,”alisema Komu.
Hata hivyo, Nnauye kwa upande wake alisema chombo chochote kitakachohitaji ushirikiano wake kuhusu suala la Chadema atakuwa tayari kufanya hivyo.
Alisema kama Chadema wataendelea kumung’unya maneno, ataanika hadharani kinachofanywa waziwazi na chama hicho.
“Chadema wakiendelea kuumauma maneno kuhusu mikataba yao nitawaanika wazi wazi,”alisema Nnauye.
Kaimu Msajili Msaidizi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Piensia Etanga, alisema hajapata taarifa kutoka Chadema kwa kuwa yupo safarini.“Sijapata barua hiyo na niko nje ya ofisi, tupo Mtwara hivyo hatuwezi kujua kama imepelekwa ofisini au la,”alisema Etanga.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, alisema hakuna nakala yoyote kutoka Chadema iliyoelekezwa katika jeshi hilo, ikizungumzia kuhusu suala hilo.“Hakuna barua yoyote iliyoelekezwa kwetu kuhusu suala hilo,”alisema Senso.
Hivi karibuni Nnauye alisema CCM imeshangazwa kuona Chadema kikiwahadaa Watanzania kufanya harambee ili kuhalalisha fedha kutoka kwa wafadhili.
“Chama Cha Mapinduzi kimeshangazwa na kusikitishwa sana na usanii huu mkubwa unaofanywa na Chadema kwa kuwahadaa Watanzania kwa usanii wa kufanya harambee, ili kuhalalisha uwepo wa mabilioni waliyopewa na wafadhili wao wa nje ya nchi.”
Aliongeza: “Mfano mzuri wa usanii huu ni kwenye Hoteli ya Serena ambako ilifanyika harambee na kurushwa moja kwa moja na kituo kimoja cha televisheni.”
No comments:
Post a Comment