SIKU moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, kutengua matokeo ya
uchaguzi ya Jimbo la Igunga, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki
na Mbunge wa Jimbo la Urambo mkoani Tabora kwa tiketi ya CCM, Bw.Samuel
Sitta, amewataka wana-CCM kuheshimu uamuzi huo na kuendelea kujipanga.
Bw.Sitta aliyasema hayo jana mjini Tabora, wakati
akikabidhi kompyuta na mashine ya kutolea nakala (printer) kwa Umoja wa
Vijana wa Kanisa Katoliki (VIWAWA) zenye thamani ya sh.milioni 2.5.
Akizungumza
mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Bw.Sitta alisema Mahakama ina
mamlaka yake kisheria wana-CCM hawana budi kuyaheshimu maamuzi hayo.
"Kama
kuna mtu anaona hukumu hiyo haikutenda haki, anaweza kwenda mahakamani
kukata rufaa, lakini mimi nashauri ni vyema tujipange upya tuingie
ulingoni," alisema, Bw.Sitta na kuongeza;
"Ni vyema tukakaa na kutafakari yaliyotokea huko Igunga, ili basi
tukiona inafaa kukata rufaa sawa, au kama tunaingia ulingoni yote ni sawa."
Kwa
upande wa Ofisi ya Bunge imesikitishwa na aliyekuwa mbunge wa Jimbo la
Igunga, Dkt.Peter Kafumu, kuvuliwa wadhifa huo, hasa kwa kuzingatia
alikuwa mtu mtaratibu na mpole sana.
Kauli hiyo ilitolewa na
Naibu Spika wa Bunge, Bw.Job Ndugai, alipoulizwa na gazeti hili jana
jisi ofisi yake ilivyopokea uamuzi huo wa mahakama.
Bw.Ndugai
alisema; "Tunaheshimu maamuzi ya mahakakama, lakini kitendo cha kuvuliwa
ubunge Dkt.Kafumu kimenisikitisha kwani kwa jinsi ninavyomjua hana
maneno na mtu."
Alisema kutokana na hukumu hiyo ni wakati mzuri
wa watu wengine kujifunza, wakishindwa waheshimu uamuzi unaotolewa na
si kuanza kutoa sababu mbalimbali.
Kwa upande wa wanasiasa waliozungumzia hukumu hiyo, walisifu uamuzi huo, wakisema umelenga kupanua wigo wa demokrasia nchini.
Mwenyekiti
wa Tanzania Labour Party (TLP), Bw.Augustino Mrema alisema, hukumu hiyo
itatoa fundisho kwa wanasiasa wenye tabia ya kukiuka sheria za uchaguzi
na kuwa waadilifu.
"Nimesifu sana uamuzi wa Jaji Shangali (Mary
Shangali) hukumu hii itaondoa vitendo vya wanasiasa kutoa rushwa kwa
wapiga kura wakati wa uchaguzi na jambo hili linatokana na viongozi wetu
kutokuwa na maadili," alisema.
Alisema CCM inapaswa kukubali
kujifunza kuwa waadilifu, wacha Mungu na kuachana na sera za kusema ovyo
pindi wanapokuwa majukwaani, ili kuepusha gharama zisizo za lazima
pindi matokeo yanapotenguliwa.
"Tatizo CCM hawako tayari kukubali
mabadiliko na wanatupeleka katika hali ngumu ya maisha kutokana na
kuiingiza nchi katika gharama, wasiwe watu wa kujivunia utajiri wa fedha
walizonazo kwa kuwa eti wana Serikali, hii ni hatari kubwa,"
alisisitiza Bw.Mrema.
Naye Naibu Mkurugenzi Habari na Uenezi wa
Chama cha Wananchi(CUF), Bw.Abdul Kambaya, alisema hukumu hiyo ni
fundisho kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuanza kusimamia sheria za
uchaguzi na kuweka pembeni nyazifa za viongozi walioko serikalini
kutoshiriki katika uchaguzi.
"Nilikuwepo wakati wa uchaguzi huo,
ni mengi yaliyofanywa na CCM, lakini hata CHADEMA iwapo wangeshinda nao
ushindi wao ungepingwa mahakamani kwani pia walihusika katika kampeni
chafu," alisema.
"Naishauri Serikali kuchunga rasilimali zake,
fedha nyingi zinapotea bure wakati wa uchaguzi huku walimu na madaktari
wakigoma kila siku kutokana na masilahi duni ya mishahara na wanafunzi
nao wakilalamikia kutopatiwa huduma bora zinazotakiwa kama vile vitabu
na walimu wa kutosha," alisema.
Alipoulizwa kama chama chake
kitashiriki uchaguzi mdogo iwapo utaitishwa jimboni humo, Bw.Kambaya
alisema,vikao vya Chama hicho ndivyo vitakavyoamua.
Ofisa wa
Idara ya Elimu na Habari wa NEC, Bi.Luth Mashamu,ilipoulizwa kuhusu
hukumu hiyo alisema hawajapata taarifa rasmi, licha ya kuzipata kupitia
vyombo vya habari nchini.
"Hatuwezi kulizungumzia suala hilo
kwani hatujapata rasmi nakala ya hukumu hiyo, tunasubiri tuletewe
(hukumu) ikiwa ni pamoja na barua ya kuiarifu Tume kutoka kwa Spika wa
Bunge juu ya nafasi hiyo kuwa wazi, lakini bado hiki ni kipindi cha
kutafakari kwa aliyeenguliwa kwa kuwa naye ana haki yake huenda akakata
rufaa," alisema ofisa huyo.
Wakati huo huo CCM imesema
inatafakari kama itakata rufaa Mahakama Kuu ili kupinga uamuzi wa
kutengua matokeo yaliyompatia ushindi aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo
kupitia chama hicho, Dkt.Kafumu.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
CCM, Bw. Nape Nnauye, alisema kuwa chama hicho kimetafakari na kitatoa
uamuzi iwapo kitakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
"Chama
kimetafakari hukumu ya kesi ya uchaguzi iliyotolewa Agosti 21, mwaka huu
na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, kimejiridhisha kitachukua uamuzi wa
kukata rufaa dhidi ya hukumu ya kesi ya uchaguzi, dhidi ya Mbunge wa
Jimbo la Igunga mkoani Tabora, Dkt.Kafumu," alisema Bw.Nnauye.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake