Thursday, August 23, 2012

SUMAYE AJITOSA KUGOMBEA UJUMBE NEC KUCHUANA NA MARY NAGU

 DR,MERY NAGU
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye
BAADA ya kuwa kimya kwa muda mrefu, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amejitokeza tena katika ulingo wa siasa baada ya jana kuchukua fomu za kuwania Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Wilaya ya Hanang’ Mkoa wa Manyara akichuana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji), Dk Mary Nagu.Mara ya mwisho kuingia katika ulingo wa kuomba kura kwa Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa kipindi chote cha miaka 10 ya utawala wa Awamu ya Tatu chini ya Benjamin Mkapa, ni mwaka 2005 wakati alipoomba kuchaguliwa na CCM kuwa mgombea urais na kushindwa.



Katika uchaguzi wa Hanang’, Sumaye anachuana na Nagu ambaye alimwachia kiti cha ubunge katika Jimbo la Hanang' huku duru za siasa kutoka ndani ya chama hicho mkoani Manyara zikieleza kuwa hiyo inatokana na uhusiano wa kisiasa wa vigogo hao sasa kutokuwa mzuri.

Uchukuaji huo wa fomu jana uliuteka Mji wa Hanang’ baada ya vigogo hao kufika katika ofisi za CCM kwa nyakati tofauti, huku kila mmoja akiwa na msafara wake wa pikipiki na wapambe.
Dk Nagu ndiye aliyeanza kuchukua fomu akifuatiwa na Sumaye ambaye alisindikizwa na idadi kubwa ya wapambe.Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Hanang', Goma Gwaltu alithibitisha viongozi hao kuchukua fomu kwa nyakati tofauti jana.

Kimbisa, Guninita nao wajitosa

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Adam Kimbisa amejitokeza kuwania uenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma. Mwanasiasa huyo alichukua fomu jana katika Ofisi za CCM Mkoa wa Dodoma ikiwa ni siku ya kwanza tangu kuanza mchakato huo utakaodumu kwa siku saba.

Kimbisa ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kupitia Mkoa wa Dodoma, alichukua fomu hizo akiwa ameongozana na wazee maarufu wa Dodoma akiwamo Mwenyekiti mstaafu wa mkoa huo, Pancras Ndejembi.

Katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CCM anayemaliza muda wake, John Guninita jana alichukua fomu kutetea nafasi hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Guninita alisema amejipima na kuona kwamba anaweza kuwa mwenyekiti katika kipindi kingine cha miaka mitano.

Mwingine aliyechukua fomu hizo, Dar es Salaam jana ni Rais wa Mtandao wa Wanataaluma Tanzania (TPN) Phares Magesa ambaye anawania nafasi ya ujumbe wa Nec.

“Nimetumia nafasi yangu ya kidemokrasia na ninaamini nina sifa za uongozi kwa sababu nimewahi kutumikia nafasi mbalimbali na nimefanya vizuri,” alisema Magesa ambaye pia ni Ofisa Mkuu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Kigwangalla aibukia Wazazi
Mbunge wa Nzega Dk Hamisi Kigwangalla jana alichukua fomu kuwania uenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa na kusema dhamira yake ni kusimamia rasilimali za jumuiya hiyo ambazo alisema zimekuwa zikiwanufaisha watu wachache.

Dk Kigwangalla ambaye alichukua fomu hizo katika Ofisi za Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mwanza alisema: “Chama Cha Mapinduzi hakijapoteza mvuto, ndiyo maana katika Uchaguzi Mkuu uliopita kiliweza kushinda viti vingi vya ubunge dhidi ya upinzani. Kinazo sera nzuri na mipango mizuri inayosimamiwa katika kuendesha nchi.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina naye amechukua fomu kutetea nafasi yake akisema hahusiki na kupoteza viti vitatu vya ubunge katika mkoa wa Mwanza katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Mabina alisema kupoteza ubunge katika Majimbo ya Nyamagana, Ilemela na Ukerewe ambayo yalichukuliwa na Chadema kulitokana na kampeni chafu kwa wapinzani kutoa ahadi hewa kama za kusomesha bure jambo ambalo alieleza kuwa kwa sasa wananchi wameona ukweli.

Mwingine aliyejitokeza kuwania uongozi ni Mwanasheria wa CCM kutoka Makao Makuu, Glorious Luoga ambaye anawania ujumbe wa NEC Wilaya ya Songea Vijijini.

Alisema Wilaya ya Songea Vijijini imekuwa na changamoto nyingi ikiwamo kwenye shule za sekondari za kata ambazo nyingi zimekuwa hazina maabara, walimu, vitabu pamoja na madawati vitu ambavyo vingeweza kutatuliwa na wananchi wenyewe kupitia Serikali zao za vitongoji na vijiji.

Habari hii imeandikwa na Habel Chidawali, Dodoma;
Joyce Joliga, Songea; Mussa Juma, Arusha; Frederick Katulanda, Mwanza na Nora Damian, Dar

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake