ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 11, 2012

SMZ yakiri kusajili meli 36 za mafuta kutoka Iran



Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imekiri kusajili meli 36 za mafuta kutoka nchini Iran kinyume na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN).

Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, alisema hayo alipokuwa akifunga mkutano wa nane wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), mjini hapa.

Balozi Seif alisema baada ya kuibuka taarifa za kusajiliwa kwa meli hizo serikali ilifanya uchuguzi na kubaini kuwa kampuni ya uwakala ya Philtex ilisajili meli 36  kwa niaba ya Zanzibar na kupeperusha bendera ya Tanzania.



Alisema kampuni hiyo inafanya kazi yake nchini Dubai ikiwa na mkataba na Mamlaka ya Usafirishaji baharini Zanzibar (ZMA), kama wakala wake wa kusajili meli za kigeni.

“Mheshimiwa Spika Serikali ilifuatilia suala hili kwa undani na imegundulika kuwa Mamlaka ya usafiri baharini (ZMA) kupitia kwa wakala wetu wa Dubai Philtex ilisajili meli 36 za Iran za mafuta na kutumia bendera ya Tanzania,” alisema Balozi Seif.

Iran imewekewa vikwazo vya kiuchumi na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa vya kusafirisha mafuta na kuuza kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo kushutumiwa kumiliki silaha za nyukilia na kusadia vikundi vya ugaidi duniani.

“Baada ya kugundua ukweli kwamba meli hizo zinapeperusha bendera ya Tanzania, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imo katika hatua za kuzifutia usajili meli hizo,” alisema Balozi Seif.

Alisema Serikali pia imeamua kuifutia uwakala kampuni ya Philtex ya kufanya kazi ya kusajili meli kwa niaba ya Zanzibar baada ya kufanya makosa hayo.

“Mheshimiwa Spika Serikali itafanya uchunguzi wa kina kujua ni vipi usajili huo ulifanyika.”alisema Makamu wa Pili wa Rais katika hotuba yake.

Balozi Seif alisema kitendo hicho kimekwenda kinyume na azimio la Umoja wa Mataifa (UN) pamoja na amri ya utekelezaji  (Excutive Order) iliyotolewa Marekani na nchi Jumuiya ya Ulaya.

Hata hivyo, alisema pamoja na tukio hilo uhusiano wa Iran na Zanzibar utaendelezwa kama kawaida kutokana na Zanzibar kuwa na historia kubwa na nchi hiyo.

Balozi Seif hakusema serikali itawachukulia hatua gani watendaji wa ZMA Zanzibar ambao walitoa taarifa za uongo na serikali kuwasilisha katika chombo cha kutunga sheria.

Julay 24, mwaka huu aliyekuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar, Hamad Masoud Hamad, aliwasilisha taarifa maalum ya serikali katika Baraza la Wawakilishi na kukanusha kuhusu Zanzibar kuhusishwa na kusajili meli za Iran nchini Dubai.

Hamad alisema pamoja na Zanzibar kuwa na uwezo wa kisheria wa kusajili meli imekuwa ikifanya kazi ya kusajili meli kwa umakini na kutaka choyo cha biashara kuondolewa katika biashara hiyo.

Alisema kwamba kimsingi Zanzibar kupitia wakala wake wa Dubai imesajili meli za mafuta 11 ambapo zote zinatoka katika nchi ya Cyprus na Malta.

Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alithibitisha kupokea malalamiko kuhusu Zanzibar kukiuka Azimio la Umoja wa mataifa kwa kusajili meli za mafuta za Iran kupitia wakala wake wa nchini Dubai.

Waziri Membe aliomba Marekani na Jumuiya ya Ulaya (EU) kufanya uchunguzi ili kupata ukweli wake baada ya Zanzibar kukanusha taarifa ya kusajili meli za Iran Dubai.

Waziri Hamad alijiuzulu wadhifa wake Julai 23, mwaka huu kufuatia ajali ya meli ya Mv Skagit ambapo watu 136 walikufa maji, 146 kuokolewa na watu nane kutoweka tangu kutokea ajali hiyo Julai 18, mwaka huu.

Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) limeahilishwa hadi Oktoba 10 baada ya kumaliza kujadili makadirio matumizi ya bajeti za serikali mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: