Advertisements

Wednesday, August 22, 2012

UNA HISIA MBAYA KWA MWENZAKO? SOMA HAPA! - 2

HABARI marafiki, ni matumaini yangu mnaendelea na shughuli zenu za kila siku. Kama hivyo ndivyo basi ndiyo furaha yangu.
Najua wengi mmenunua gazeti hili na moja kwa moja mmefungua ukurasa huu kwa ajili ya kupata mwendelezo wa makala ya wiki iliyopita.
Mmewahi hapa kwa ajili ya tiba ya matatizo yenu, mnataka kujifunza na kuongeza maarifa pale kwenye upungufu. Nami naahidi kuwapa kile kile mnachokitarajia.

Wote mna haki ya kupata tiba ya kile kinachowasumbua, marafiki siku zote muungwana hutimiza kile alichokiahidi hivyo nachukua fursa hii kuwakaribisha kutoka pale nilipoachia wiki iliyopita. Najua mnajua pale nilipoishia.  Basi tuache blablaa na kuingia katika mada husika ili kuweza kutibu mioyo yenu.
Tunazungumzia hisia, kwamba kila binadamu ana hisia ambazo zinapatikana kupitia milango mitano ya fahamu.
Ndiyo, mtu anaweza kuhisi kitu kwa kukigusa kwa ngozi yake, kwa kuona  kwa macho yake, kulamba kwa ulimi wake, kunusa kwa pua yake na kusikia kwa masikio yake.
Lakini hapa tunazungumzia hisia mbaya. Binadamu anakuwa na hisia mbaya kwa mpenzi wake bila ya kuona, kunusa, kuonja, kugusa na kusikia bali hisia za ziada ndizo zinazomfanya mtu aweze kumhisi vibaya mpenzi wake. Nadhani bado sijawaacha sana, kwa wale tuliokuwa pamoja wiki iliyopita wanakumbuka tuliishia kwenye kipengele  cha kutojiamini.
Basi marafiki, tumalizie mada yetu kwa kuendelea na kipengele hicho, kisha tutashuka katika vipengele vilivyosalia na kupata tiba sahihi ya kuondokana na hisia mbaya kwa mpenzi wako.

3. Kutojiamini
Mpenzi anashindwa kujiamini kwa kuona haendani na mwenza wake, anajitathmini kisha anajikosoa na kujiona yeye siyo mzuri na kuhisi labda haendani na mwenzake. Nataka niwafundishe kitu, imani ya mtu huyumba pale unapojenga tabia ya kujilinganisha thamani yake na mpenzi wake.
Hali ya uchumi
Siku zote mapenzi ni upofu, mtu anaweza kumpenda mtu wa hali ya chini kimaisha kwa kuwa ni chaguo lake na akataka kumpandisha hadi pale alipo yeye.
Mara ngapi tumeshuhudia, wanaume wenye uwezo wa kifedha wanaamua kuwachukua madada powa na kuwapangia nyumba huku wakiwaambia watulie ili wawaoe?
Hapo ndipo utakapogundua kuwa mapenzi hayawezi kupewa thamani kutokana na uwezo wa mtu kifedha au ki-cheo.
Tatizo kubwa ni kwa wanaume wasio na uwezo kifedha wanapokuwa  na wapenzi wenye uwezo, huanza kujishtukia na kukosa amani ndani ya mioyo yao. Kila wakati wanahisi kuibiwa na kufikia kujishusha thamani.
Sitaki kuwatetea wanawake kwamba hawana tatizo hili ingawaje kwa upande  wao halipo kwa kiasi  kikubwa kama kwa wanaume. Wapo wanawake wenye fedha wanaohofia kuibiwa waume zao kutokana kuwapa hadhi ya kimaisha na kukubali kuolewa nao. 
Kuishi kwa historia
Siku zote historia za wapenzi wawili haziwezi kufanana, ni mara chache sana tukio hilo hutokea lakini mpaka leo kuna wapenzi wanaoishi kutokana na historia za nyuma za wapenzi wao.
Kama mwenzio aliishi maisha ya uhuni siku za nyuma, amini kwamba anaweza kubadilika na kuwa mama au baba mzuri wa kuongoza nyumba.
Kwa kufuata historia hizo, utakuta uaminifu unatoweka ndani ya nyumba kwa kutawaliwa na hisia mbaya, mume au mke huhisi mwenzake anamuongopea hata akimwambia kuwa atachelewa kurudi nyumbani kutokana na shughuli za kiofisi.
Kila siku kuchunguzana kupitia simu zao, utakuta mmoja akienda kuoga mwingine anatafuta meseji au namba za simu zenye mashaka  ili aweze kuuliza huyu ni nani.
Tiba halisi
Ndugu zangu, haihitaji nguvu nyingi sana kuepukana na hisia mbaya kwa mpenzi wako, unachotakiwa kufanya ni kumwamini.
Kama umeshaingia naye kwenye ndoa, kipindi chako cha kumchunguza kilikuwa ni kabla  ya ndoa, pale ndipo ulitakiwa kujua kuwa unaoa au unaolewa na mtu wa aina gani.
Kama umeshazama kwenye ndoa na unahisi mwenzio anakudanganya,  hapa kuna tiba ya kugundua uongo wake. Muangalie kwa makini usoni mwake wakati akiwa anakwambia alikochelewa. Siku zote kama anasema uongo utamjua kwa kuwa atababaika kwa kuwa atahisi macho yako makali yanauona moyo wake unavyodanganya.
Ukifanya hivyo, atakuogopa na kuhisi unajua nyendo zake, ukiona kuna tatizo kwa mpenzi wako, mwambie ukweli kwa njia ya utaratibu  kwani hakuna haja ya kukurupuka na kupayuka.
Jiamini! Kuna kitu cha kujifunza, unapokuwa katika uhusiano, unapaswa kujiamini na kuridhika na hali aliyonayo mpenzi wako.
Amini kwamba, mpenzi wako anakuona wewe ndiyo mzuri kuliko wengine  wote duniani.Ukilishinda hilo, basi hata kama mkiwa na tofauti zenu lakini mtadumu milele kwenye mapenzi.
Asanteni kwa kunisoma, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine.

www.globalpublishers.info

No comments: