Tuesday, August 14, 2012

Wewe unaweza kuwa mchawi wa mapenzi yako -2

KAMA nilivyotangulia kueleza wiki iliyopita, kuna watu wanaamini mno katika uchawi. Wanamaliza fedha kwa waganga wa kienyeji wakiamini kwamba wamerogwa, hivyo wanatafuta ufumbuzi kutoka kwa wataalamu wa mambo ya asili. Wapo wanaoita mambo ya Kiswahili.
Kwangu napinga kuita hivyo kwa sababu nami ni Mswahili na kwa uzoefu wangu, sisi Waswahili hatuna utamaduni wa kutegemea mitishamba kuamua hatma za uhusiano wetu wa kimapenzi. Ila baadhi wapo, tena wengi haswaaa!

Shika hili kwamba wewe mwenyewe pengine ndiye mchawi wa mapenzi yako mwenyewe. Hujiulizi kwa nini wengine wanadumu? Ni vipi wenzi wengine wanaheshimiana? Inakuaje kwako imekuwa kinyume? Siyo suala la upepo, wakati mwingine ni kujitakia.
Kivipi mwenzi wako hakuheshimu? Ni makosa gani ambayo wewe umefanya? Ukishapata majibu ya maswali hayo, utaweza kujua faida za wewe kujitambua. Nakuasa ushike moja kuu kwamba mapenzi ni nidhamu.
Yapo kama kioo, ukiyaheshimu nayo yatakuheshimu na utayaona murua. Endapo utayachukulia kwa mzaha, nayo hayatasita kukufanyia mzaha. Mwisho utakuja kugundua kwamba yanakutesa, ukifika hapo usiache kukumbuka nawe ulivyoyatesa. Mambo haya yafuatayo ndiyo uchawi wenyewe;

1. KUTOSEMA KWELI
Katika mapenzi uongo ni kitu kibaya sana, uongo wa aina yoyote ile ni mbaya katika uhusiano wowote ule na huweza kupunguza mapenzi ya dhati na uaminifu kwa kiasi kikubwa hasa kama mmojawapo atagundua kuwa mwenzi wake ni muongo, anamdanganya.
Wapo ambao wakigundua mpenzi wake ni muongo wanauliza au kuongea nao ambacho ni kitu kizuri na siku zote napenda sana kusisitiza suala la wapenzi kujadili vitu mbalimbali vinavyotokea kwenye uhusiano wao, lakini wengine wanaamua kunyamaza au kuacha kabisa.

2. KUTENGENEZA PENZI LA PEMBENI
Moja ya jibu nililolipata kwa watu wengi niliojaribu kujadiliana nao mada hii walisema kuwa uhusiano mwingine unasababisha mapenzi kupungua, inaumiza sana kugundua yule unayempeda kwa dhati ana mpenzi/wapenzi wengine. Kubali au kataa, hii ni moja ya sababu kubwa zinazofanya mapenzi kupungua au kuvunjika kabisa.
Kamwe usimuumize moyo akupendaye kiukweli, usimfanye ajutie penzi lako,usimfanye anung’unike kwa unayomtendea, ipo siku utahitaji mapenzi ya kweli kwa mwingine na hutayapata, ukimuumiza ipo siku nawe utaumia tu, mapenzi ya kweli yanawezekana kama kunakuwa na uaminifu.

3. UPUUZI 
Hii pia huchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza mapenzi kama siyo kuyamaliza kabisa. Unapokuwa kwenye uhusiano jitahidi kumpenda mtu wako kwa hali yoyote na usiwe na dharau kwake au hata kwa marafiki zake au ndugu zake au hata wengineo. Hakuna mtu anayependa mtu mwenye dharau hata awe nani. Hata kama mwenzi wako ana uwezo mdogo kuliko wewe hiyo isiwe sababu ya wewe kumdharau.

4. MSEMA HOVYO
Hakuna kitu kinachoweza kumfanya mwenza wako kukukimbia au hata kukosa uaminifu na wewe kama akija kugundua kama wewe ni mropokaji na huna ‘’kifua’’ hasa kwa yale mambo ambayo ni ya chumbani na hayakutakiwa kutoka nje. Hakuna mtu anayependa siri zake kutoka hadharani na huwa inaumiza sana kwenye mapenzi kumpa mtu siri zako halafu yeye anaenda kuwaeleza wengine .
Mambo mnayafanya mkiwa wawili tena ndani lakini kesho anaenda kusimulia kwa watu si jambo la busara kabisa.

5. USIRI
Miongoni mwa vitu hatari pia kwenye uhusiano ni pamoja na hili la usiri wa kupitiliza. Kama una vitu moyoni na upo kwenye mapenzi/ uhusiano bora kabisa si vizuri kuvificha na hasa vile vinavyohusiana na mapenzi yenu moja kwa moja.
Ni kweli kuna vingine huwezi kumwambia kwa sababu havina uhusiano wa moja kwa moja na uhusiano wenu ila kuna vingine ni lazima avijue ili kutoleta ugomvi au matatizo hao baadaye.
Kama kuna kitu hukuwahi kumwambia na unahisi ukimwambia atakasirika ni bora umtafutie nafasi nzuri umwambie kuliko aje kugundua mwenyewe itakuwa shida sana kukuelewa.

6. TAMAA 
Tamaa ni kitu kingine ambacho hufanya uhusiano mwingi kukosa nguvu na mwingine kuvurugika kabisa. Kama mpo kwenye mapenzi na mmeamua kupendana kwa shida na raha basi haitakiwi mmoja wenu kuwa na tamaa na kukosa uvumilivu hasa kwa yale mambo yanayoweza kuzuilika.
Kama mpenzi wako ni wa hali fulani na umeamua kuwa naye basi usiwe na tamaa kwa vitu vingine ambavyo vinaweza kukusababishia uhusiano wenu kukosa nguvu na kufa kabisa. Amini kuwa ipo siku mtakuwa na vitu kama unavyotamani kwa kuongeza bidii kutafuta na kushauriana nini cha kufanya lakini si kwa kutafuta ‘’shortcut’’/njia nyepesi nyepesi zinazoweza kukugharimu hapo baadaye.

7.  KUKOSA MSIMAMO
Hii kitu huwakuta wengi sana kwenye mapenzi ya siku hizi. Nadhani ni hali halisi ya wapenzi wengi siku hizi wamekosa msimamo kwenye mapenzi/uhusiano wao na unakuta  mtu anakosa msimamo hasa katika maamuzi anayochukua, kuwa na msimamo na utambue uliyenaye ndiye unayempenda.

8. KUTOKUWA NA MSAADA KWA MWENZAKO
Tabia hii pia kwa kiasi kikubwa inaumiza sana na kusababisha kushuka kwa thamani ya mapenzi miongoni mwa wapendanao. Kama kweli unampenda mpenzi wako basi msaidie anapopata matatizo na umjali na kumchukulia kama mpenzi wako na mtu wako wa karibu na siyo kukimbia majukumu bila sababu za msingi.
Kama huwezi kujali na kusaidia basi usiingie kwenye uhusiano, bora ukae peke yako.

www.globalpublishers.info

1 comment:

Anonymous said...

Nimesoma soma la leo. Yoote ya maana sana. Kubwa zaidi ya ni NAMBA 2.
Huyo ni kirusi mkubwa na ana nguvu kuliko ukimwi! SOMENI KWA MAKINI hasa paragrafu ya mwisho hapo namba 2. Tukumbuke kuwa MUOSHA HUOSHWA...