ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 20, 2012

YANGA IMEIVA, YAICHAPA AFRICAN LYON 4-0


 Mshambuliaji wa Yanga, David Luhende (kulia) akichuana na beki wa African Lyon, Musasa Obina wakati wa mchezo wa kirafiki uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Yanga imeshinda 4-0.
 Mashabiki wa Yanga
Moja ya heka heka zilizotokea katika lango la African Lyon

MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga imezidi kudhihirisha kuwa msimu huu ni moto wa kuotea mbali baada ya kuinyoa African Lyon kwa kuibugiza mabao 4-0 katika mchezo uliofanyika leo Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo ya kirafiki ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, Yanga inayonolewa na Tom Saintfiet, ilianza kwa kasi mchezo huo na kusababisha beki Mussa Obina wa Lyon kujifunga dakika ya 7 tu, akiwa katika harakati za kuokoa.
Yanga iliendelea kuliandama lango la Lyon huku wapinzani wao nao wakijibu mapigo kwa mashambulizi ya kushtukiza, ambako dakika ya 30, Adam Kingwande alipiga shuti kali lakini likapanguliwa na kipa Yaw Berko wa Yanga.
Hadi dakika 45 zinamalizika Yanga ilikuwa mbele kwa bao hilo moja. Kipindi cha pili, kila timu ilifanya mabadiliko ili kuboresha vikosi vyao.
Haruna Niyonzima alipopachika bao la pili kwa Yanga dakika ya 55, kwa mkwaju wa penalti, baada ya Simon Msuva kuangushwa eneo la hatari na Semmy Kessy.
Kama haitoshi, dakika ya 72, Msuva alikandamiza bao la tatu, baada ya Mohamed Samatta kumrudishia kipa wake Abdul Seif mpira mfupi, kabla ya kukosa bao dakika ya 84, baada ya kuwatoka mabeki wa Lyon pamoja na kipa wao, lakini mpira aliyoupiga ukatoka nje kidogo ya lango.
Jerry Tegete ambaye inadaiwa na baadhi ya mashabiki kuwa siku hizi ‘sumu’ yake imepingua, akitokea benchi alihitimisha karamu ya mabao kwa Wana Jangwani hao, baada ya kutupia kambani bao la nne akimalizia murua, pande la Idrisa Rashid.
Hadi filimbi ya mwisho, Yanga ilitoka Uwanjani na ushindi huo mnono. Yanga tangu usajili wa msimu huu, imekuwa ikifanya vema katika mechi zake zote za kirafiki na kimashindano, ambako imepoteza mchezo mmoja tu dhidi ya Atletico Olympics wakati wa mashindano ya Kagame Cup, ilipolala kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja huo wa Taifa.
Yanga iliwakilishwa na: Yaw Berko, Shadrack Nsajigwa ‘Fusso’/Godfrey Taita, Oscar Joshua/Stephano Mwasika, Kelvin Yondani/Ladslaus Mbogo, Nadir Haroub ‘Canavaro’/Ibrahim Job, Athumani Idd ‘Chuji’, David Luhende/Shamte Ally, Haruna Niyonzima/Rashid Gumbo, Didier Kavambangu/Idrisa Rashid, Hamis Kiiza/Jerry Tegete, Simon Msuva.

Lyon: Abdul Seif/Noel Munishi, Musasa Obina, Yusuf Selemani, Robert, Semmy Kessy/Bakari Mpakala, Juma Sunday, Benedicto Jacob/Bryton Owen, Johanes Kajuna/Zuberi Ubwa, Adam Kingwande/Paulo Mama, Idi Mbaga/Hood Mayanja na Mohamed Samatta/Ahmed Matola. 





Kocha wa timu ya Africa Lyon, Muargentina, Pablo Velez, akionekana kulalamikia jambo kwenye benchi la ufundi la timu yake wakati timu yake ilipokutana na timu ya Yanga katika mchezo wa kirafiki kwenye uwanja wa Taifa jioni hii.

No comments: