Mke wa mwanasiasa mwenye
ushawishi mkubwa nchini Uchina Bo Xilai amepatiwa hukumu ya kifo ambayo
badala yake atatumikia kifungo gerezani kwa mauaji ya mfanyabiashara wa
Uingereza Neil Heywood.
Gu Kailai hakupinga mashitaka dhidi yake katika
kesi hiyo iliyochukua siku moja ya kumuua kwa kutumia sumu Bwana Heywood
mwezi Novemba mwaka 2011.Bwana Bo, kiongozi mkuu wa zamani wa chama mjini Chongqing, alikuwa akitegemewa kugombea nafasi ya uongozi wa juu kabisa baadaye mwaka huu.
Lakini hajaonekana hadharani tokea kuanza kwa uchunguzi dhidi ya mkewe Gu kutangazwa kuanza.
Msaidizi wa Gu, Zhang Xiaojun, alihukumiwa kifungo cha miaka tisa kwa ushiriki wake katika mauaji hayo.
Heshima ya kipekee
Hukumu hii kwa mtu mashuhuri kuwahi kutokea kwa miaka mingi nchini Uchina, imetolewa siku ya Jumatatu huku kukiwa na ulinzi mkali mahakamani.Vyombo vya habari nchini Uchina vimeripoti kuwa, wakati wa kesi hiyo tarehe tisa Agosti, Gu alikiri kuwa alimlisha sumu Neil Heywood katika chumba cha hotel mjini Chongqing, akisaidiwa na msaidizi wake.
Alisema alikuwa akiathiriwa na matatizo ya kisaikolojia na kwamba Bwana Heywood alimtishia kijana wake wa kiume katika mvutano wa kibiashara kuhusu nyumba. Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti.
Picha zilizoonyeshwa kupitia televisheni ya taifa ya Uchina zimemuonyesha Gu akiitikia hukumu hiyo. ''Hukumu hii ni haki. Inaonyesha heshima maalum kwa sheria, uhalisia na uhai,'' ameongeza.
Akizungumza baada ya hukumu hiyo kusomwa, msemaji wa mahakama Tang Yigan amesema mahakama inaamini Bwana Heywood alimtishia mtoto wa Gu lakini hakutekeleza vitisho hivyo. Imegundua pia Gu alikuwa akiathiriwa na matatizo ya kisaikolojia'', alisema.
Msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amesema Uingereza iliweka bayana kwa Beijing kuwa kesi hiyo ni lazima ichunguzwe ipasavyo, lakini matokeo yalikuwa ni ''juu ya mamlaka za Uchina".
Mwanasheria wa familia ya Heywood amesema wanaheshimu uamuzi wa mahakama.
Hukumu ya kifo iliyoahirishwa kwa muda wa miaka miwili inamaanisha kuwa, iwapo Gu hatafanya kosa la jinai akiwa gerezani, hukumu yake itaanza baada ya miaka miwili kutumikia kifungo cha maisha, na inaweza kupunguzwa zaidi iwapo ataonyesha tabia nzuri. Mtaalamu wa masuala ya sheria Profesa Donald Clarke anaandika katika blogu yake.
Watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Uchina walianza kutoa maoni yao mara moja kuhusu hukumu hiyo kupitia mitandao kijamii hususani ule wa Twitter.
Wengi wameonyesha kutoridhika wakisema kuwa wauaji wengi nchini Uchina hunyongwa wakilinganisha na kesi hii ya Gu. Wengine wametoa wasiwasi wao kuwa Gu huenda akaachiliwa kwa kutumia kipengele cha msamaha kwa misingi ya kiafya.
Mabadiliko ya uongozi
Katika siku tofauti ya kesi hiyo mnamo tarehe 10 Agosti, maafisa wa ngazi ya juu wa polisi mjini Chongqing walikiri mashitaka ya kuficha ushahidi dhidi ya kesi ya Gu. Afisa wa mahakama amesema walipewa hukumu ya kifungo cha kati ya miaka mitano na kumi na moja gerezani. Shirika la habari la AFP limeripoti.Chanzo cha kifo cha Bwana Heywood awali kilirekodiwa kuwa ni shinikizo la moyo.
Kesi hiyo ilikuja hadharani baada ya makamu wa Bo Xilai, mkuu wa polisi Wang Lijun, alipokimbilia ubalozi wa Marekani mwezi Februari akiwa na vielelezo vinavyohusiana na kesi ya Gu.
Hajawahi kuonekana hadharani toka wakati huo na vyombo vya habari vya serikali vinasema nafanyiwa uchunguzi.
Haijulikani ni kwanamna gani chama cha kikomunisti kinapanga kushughulika na Bwana Bo, anayeonekana mwenye ushawishi mkubwa.
Wachambuzi wengi wanatarajia kuona akipandishwa cheo katika kamati maalum ya watu tisa baadaye mwaka huu.
Wajumbe saba wa kamati hiyo wanatarajiwa kustaafu kukiwa na kizazi kipya cha viongozi wanaotarajiwa kuchukua nafasi zao katika mkutano wa chama hicho baadaye mwaka huu.
Bwana Bo amevuliwa vyeo vyake vya uongozi akiwa nachunguzwa kwa utovu wa nidhamu,'' vyombo vya habari vya serikali vinasema.
Kufichuliwa kwa kesi ya Gu Kailai's katika uhalifu huo kumesambaratisha nyota ya mumewe Bo Xilai katika siasa na kusababisha mgawanyiko mkubwa katika chama cha Kikomunisti wakati kikijiandaa kubadili uongozi.
No comments:
Post a Comment