ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 20, 2012

Bunge la Somalia lakutana Mogadishu


Wabunge wa Somalia

Wabunge wa Somalia
Bunge la kwanza la Somalia lililochaguliwa ndani ya nchi hiyo limeapishwa rasmi katika mji mkuu Mogadishu na kuashiria kumalizika kwa muda wa serikali ya mpito iliyodumu kwa muda wa miaka minane iliyopita.

Wabunge hao wamefanya kikao chao cha kwanza katika uwanja mkuu wa ndege, moja ya maeneo yenye ulinzi mkubwa mjini humo.
Jukumu kuu la wabunge hao sasa ni kumchagua rais mya wa nchi hiyo na shughuli hiyo inatarajiwa kukamilika katika muda wa wiki mbili zijazo.
Rais anayeondoka ambaye ni Muislamu mwenye siasa za wastani, Sheikh Sharif Sheikh Ahmed, amekuwa madarakani tangu mwaka wa 2009 na anatarajiwa na wengi kuibuka mshindi.
Wagombeaji wengine wanaopigiwa kumpa rais wa sasa upinzani mkali, ni pamoja na waziri mkuu Abdiweli Mohamed Ali na aliyekuwa spika wa bunge la nchi hiyo Sharif Hassan Sheikg Aden.
Zoezi hilo ni muhimu katika historia ya taifa hilo na hasa tangu kupinduliwa kwa serikali ya Siad Bare mwaka wa 1991.
Tangu wakati huo Somalia imekuwa chini ya wababe wa kivita, wanamgambo wa Kiislamu na serikali za nchi jirani zimekuwa zikishughulikia masuala ya taifa hilo.
Kwa ushirikiano na usaidizi wa wanajeshi wa Muungano wa Afrika, serikali ya mpito ya Somalia imefanikiwa kudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo, lakini kundi la wapiganaji wa Al Shabaab, ambalo lilijiunga na kundi la Al Qaeda bado linadhibiti maeneo kadhaa ya kati na kusini mwa nchi hiyo.
Wabunge hao wapya walifanya kikao chao cha kwanza leo asubuhi, katika uwanja wa ndege ambao kwa sasa unalindwa na wanajeshi wa Muungano wa Afrika.
Bunge hilo wawakilishi litakuwa na wabunge 275 ili hali bunge la Senate litaluwa na takriban wabunge 54.
Kufikia sasa jumla ya wabunge 211 wameapishwa idadi ambayo inazidi idadi inayohitajika kwa bunge kukutana na kufanya vikao vyake.

No comments: