Katibu Mkuu akiwa na Balozi Manongi mara baada ya kupokea hati hizo za utambulisho.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akisalimiana na Balozi
Tuvako N. Manongi, Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa
kabla ya kukabidhi hati zake za Utambulisho.
Balozi Tuvako Manongi, akiwa katika picha ya pamoja na maafisa na
wafanyakazi wa Ubalozi mara baada ya kuwasilisha hati za Utambulisho kwa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.Picha na Mpiga picha Maalum
NA MWANDISHI MAALUM, UN
Balozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa
Mataifa, Tuvako N. Manongi jana Jumatano amewasilisha hati zake za
utambulisho kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon.
Balozi Manongi alikuwa kati ya Mabalozi Sita waliowasilisha hati zao
siku hiyo ya jumatano ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kwa Mkutano
wa 67 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa utakaowahusisha Wakuu wa Nchi
na Serikali kutoka nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Hafla ya kukabidhi hati hizo imefanyika Ofisini kwa Katibu Mkuu na
kushuhudiwa na baadhi ya Maafisa Waandamizi kutoka Ubalozini .
Baada ya kukabidhi hati hizo, Katibu Mkuu Ban Ki Moon alifanya mazungumzo na Balozi Tuvako Manongi.
Katika
mazungumzo hayo, Katibu Mkuu amesema anaendelea kuitegemea Tanzania
kama nchi kiongozi na mshawishi katika kusukuma mbele ajenda zake,
zikiwamo zile zinazolenga kufanya mapitio ya baadhi ya majukumu ya
Umoja wa Mataifa.
Akasem.“Ninayo
mahusiano ya karibu na ushirikiano mzuri sana na Rais Jakaya Mrisho
Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Nje Bernard
Membe na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wangu Asha-Rose Migiro. Mimi na
wewe tunafahamiana vizuri tumefanya kazi kwa karibu. Ninakutumainia
wewe na nchi yako kwamba mtaendelea kuwa msaada kwangu na kushirikiana
nami kwa karibu” akasititiza Ban Ki Moon.
Aidha Katibu Mkuu huyo wa UM , ambaye alionyesha wazi kufurahishwa na
Uteuzi wa Balozi Manongi kuwa Balozi katika Ubalozi wa Kudumu wa
Tanzania katika UM, na hasa ikizingatiwa kwamba alikuwa mmoja wa
maafisa wake waandamizi kabla ya uteuzi huo. Na amemhakikishia
Balozi ushirikiano wa karibu na kwamba milango iko wazi wakati
wowote akimhitaji.
Kwa upande wake, Balozi Manongi pamoja, na kufikisha kwa Katibu Mkuu
Salamu rasmi alizotumwa na Mhe. Rais Jakaya Kikwete amesema, atatumia
uzoefu wake kusukuma mbele ajenda si tu za Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa bali pia hasa zile ambazo zina maslahi kwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Afrika kwa Ujumla.
Sehemu ya salamu rasmi za Mhe. Rais Jakaya Kikwete kwa Ban Ki Moon,
zilikuwa ni pamoja na kumshukuru Mkuu huyo wa UM kwa uamuzi wake wa
kuitisha mkutano maalum utakaojadili mgogoro na kuzotora kwa
usalama na amani katika eneo la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo ( DRC).
Mkutano
huo utawashirikisha viongozi mbali mbali wakiwamo wakuu wa Nchi na
Serikali na wadau wengine kujadiliana ambapo watajadiliana na
kubadilishana mawazo kuhusu namna bora ya kuchagia upatikanaji wa amani
ya kudumu katika eneo la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo. Mkutano huo utafanyika Septemba 27 hapa Umoja wa Mataifa na
unatarajiwa kutoka na tamko rasmi.
Ikumbukwe pia kwamba, Rais Jakaya Kikwete ni Mwenyekiti wa Asasi ya
Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za
Kusini mwa Afrika ( SADC) na amekuwa mstari wa mbele katika kutafuta
suluhu na amani ya kudumu katika eneo hilo na Mashiriki ya DRC.
Balozi Tuvako Manongi anakuwa Balozi wa kumi na Nne (14) tangu
kuanzishwa rasmi kwa Ubalozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Mabalozi wengine ambao wamewahi kushika wadhifa huo huko nyuma, ni
Balozi Vedast K. Kyruzi, Balozi A.Z. Nsilo Swai, Balozi Chifu Erasto
A.M. Mang’enya, Balozi John W.S. Malecela, Balozi Akil B.C. Daniel,
Balozi Salim Ahmed Salim, Balozi Paul M. Rupia, Balozi Mohamed Ali Foum,
Balozi Dr.Wilbert K. Chagula, Balozi Anthony B. Nyaki, Balozi Daudi N.
Mwakawago, Balozi Dr.Augustine P. Mahiga, na Balozi Ombeni Y. Sefue.
Balozi
Manongi atafanya kazi kwa karibu na kwa ushirikiano mkubwa na Naibu
Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi anayetarajiwa kuwasili kituoni wakati
wowote.
No comments:
Post a Comment