ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, September 29, 2012

CCM yaigaragaza Chadema


  *CUF nayo yapigwa mweleka, yashindwa u-Naibu Meya
  .Nape abeza �utabiri� wa Dk Slaa kuhusu kifo cha CCM
Katibu wa Itikadi na Uenezi wake, Nape Nnauye
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanikiwa kutwaa uongozi wa halmashauri ya jiji la Mwanza, baada ya kushinda nafasi ya Meya iliyokuwa ikishikiliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Chadema ilitwaa nafasi hiyo baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, ambapo diwani wa Nyakato, Josephat Manyerere alishinda.

Kwa ushindi huo, Manyerere akawa Meya wa kwanza wa jijini hilo kutoka upinzani, tangu Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi uliofanyika 1992.

Kwenye uchaguzi wa jana, CCM kilimsimamisha diwani wa kata ya Mkolani, Stanslaus Mabula, kuwania nafasi ya Meya wa jiji wakati Naibu Meya ikimshirikisha John Minja (diwani wa Igogo).

Kwa upande wa Chadema, kilimsimamisha diwani wa kata ya Mahina, Charles Chinchibela, kuwania nafasi ya Meya na kuacha nafasi ya Naibu Meya kuwaniwa na diwani wa kata ya Mirongo (CUF), Daud Mkama.



Matokeo ya jana yakawa CCM kuibuka ‘mbabe wa siasa za Mwanza’ baada ya Mabula kupata kura 11 dhidi ya nane za Chinchibela.

Dhoruba ya kisiasa ya CCM iliuangukia upinzani katika nafasi ya Naibu Meya ambapo mgombea wake, Minja, alipata kura 10 dhidi ya kura 8 alizopata Mkama wa CUF.

Kabla ya kufanyika uchaguzi huo, madiwani wa Chadema wakiongozwa na Mbunge wa Nyamagana, Hezekiah Wenje, walijaribu kugomea uchaguzi huo wakipinga hatua ya CCM kuwahamisha Mbunge wa viti maalum (CCM), Maria Hewa na diwani wa viti maalum (CCM), Leticia Simba, kutoka wilaya ya Ilemela kwenda Nyamagana.

Madiwani hao wa Chadema walikusudia kugomea uchaguzi huo kwa madai kwamba, Mbunge Hewa na Diwani Simba ni wakazi halali wa wilaya ya Ilemela, na hati zao za viapo bungeni na katika baraza la madiwani, zinatamka hivyo.

Hata hivyo, baada ya kujadiliana kwa kina, hatimaye madiwani hao wa Chadema walikubali kurudi na kuendelea na uchaguzi na kujikuta `wakiangukia pua’ na kuiacha halmashauri ya jiji la Mwanza katika uongozi wa CCM.

SABABU ZA UCHAGUZI


Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Mwanza unafuatia hatua ya madiwani wa Jiji la Mwanza kumng’oa madarakani aliyekuwa Meya, Josephat Manyerere, kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.

Lakini pia ilitokana na hatua ya serikali kuunda halmashauri mpya ya manispaa ya Ilemela.

Kufuatia hali hiyo serikali ilipanga kufanyika kwa chaguzi mbili tofauti za Mameya ambapo madiwani kutoka kata zilizopo wilaya ya Nyamagana, walitakiwa kumchagua Meya wa Jiji la Mwanza.

Pia madiwani kutoka kata zilizopo wilaya ya Ilemela walitakiwa kumchagua Meya wa manispaa ya halmashauri hiyo.

NAPE AMKEJELI SLAA

Kufuatia ushindi huo, CCM kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wake, Nape Nnauye,  amesema matokeo hayo ni fedheha kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa.

Nape alisema Dk Slaa alikakariwa jana akisema CCM inaelekea kufa, ‘utabiri’ uliodhihirika kuwa kutokuwa na ukweli.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Nape alisema ushindi wa CCM katika uchaguzi huo umedhihirisha kuwa chama hicho bado kina nguvu.

“Huyu mzee (Dk.Slaa) anazeeka vibaya, atasemaje kwamba CCM kinakufa, mbona tumeshinda umeya wa jiji la Mwanza. Chama kinachoelekea kufa kinawezaje kushinda uchaguzi,” alihoji Nape.

Toleo la gazeti hili jana, lilichapisha habari iliyomnukuu Dk. Slaa akisema kwamba CCM kinaelekea kufa, kutokana na kushindwa kuwaengua katika nafasi za kuwania uongozi wa chama hicho watuhumiwa wakubwa wa ufisadi.

Hata hivyo, Nape alisema utabiri huo wa Dk. Slaa unaonyesha jinsi kiongozi huyo wa anavyozeeka vibaya, kauli ambayo (Nape) amekuwa akiirejea mara kwa mara.

“Katika siasa huwezi kucheza ngoma inayopigwa na mpinzani wako, yeye (Dk.Slaa) yuko nje ya vikao vyetu, hawezi kujua tunachojadiliana, mambo yetu atuachie sisi, tunajua tunachofanya”alisema.

Aliongeza kwamba CCM kina uzoefu mkubwa wa kushughulikia migogoro ya ndani, hivyo akihitaji maoni ya mtu mwingine katika kuamua mwanachama gani afukuzwe na nani asifukuzwe.
Nape alidai hatua ya Chadema kupoteza umeya wa jiji la Mwanza, inatokana na chama hicho kuendeshwa kibabe na kwa misingi ya undugu na ukanda.

Wakati huo huo uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa manispaa ya Ilemela, umeshindwa kufanyika kutokana na kile kilichoelezwa kwamba kuna pingamizi la mahakama lililowekwa na diwani wa kata ya Kitangiri, Henry Matata.

Diwani huyo alifukuzwa uanachama na chama chake cha Chadema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe, alitangaza kuahirisha uchaguzi huo, baada ya kusoma barua kutoka kwa Matata iliyoambatanishwa na pingamizi la mahakama, kisha kutolewa ufafanuzi na Mwanasheria wa jiji.

Alisema, kutokana na pingamizi hilo ameamua kuahirisha uchaguzi huo hadi hapo utakapotangazwa tena baada ya kufikia muafaka wa suala hilo.





 
CHANZO: NIPASHE

No comments: