Nd. Waislam,
Nd. Viongozi wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislam.
Nd. Waandishi wa habari.
Assalaamu alaykum warahmatullaah,
TAMKO LA JUMUIYA YA MAIMAMU ZANZIBAR KUHUSU VITENDO VYA UVUNJIFU WA
AMANI NA UTULIVU VILIVOTOKEA KATIKA UCHAGUZI MDOGO JIMBO LA BUBUBU
NAFASI YA UWAKILISHI TAREHE 16/9/2012.
Sifa njema zote zinamstahikia Mwenyezi Mungu, wingi wa Utukufu na
Mwenye nguvu zisizoshindika na Mlezi wa viumbe. Sala na salamu zimshukie Mtume wetu Muhammad (
salallahu alayhi wa sallam ) ambaye ameletwa na dini ya haki ili izishinde dini
nyengine zote hata kama makafiri watachukia. Rehema na Allah ziwafikie jamaa
zake, Masahaba na wale wote waliowafuata
hao na kusimama kuinusuru dini yao hadi mwisho wa ulimwengu huu.
Jumuiya ya Maimamu Zanzibar ( JUMAZA) imesikitishwa mno na vitendo vya
uvunjifu wa amani na utulivu vilivyotokea katika uchaguzi mdogo jimbo la Bububu
uliofanyika tarehe 16/9/2012.
JUMAZA inawakumbusha Wazanzibari wote kuwa ni kosa kubwa mno kuibeza
na kudharau neema ya amani na utulivu alivyotutunuku Allah (S.W) baada ya muda
mrefu kuishi katika migogoro, uhasama na chuki zilizotokana na siasa za chuki
kama tulivyowahi kutanabisha katika tamko letu tulilolitoa siku tatu kabla ya
uchaguzi kufanyika tarehe 14/9/2012. Kila Mzanzibari ni shuhuda juu ya maafa
yaliyotokea kutokana na siasa hizo za chuki ikiwemo kuharibu mali za watu,
kususiana kupoteza heshima za watu na kupoteza maisha ya Wazanzibari wengi
katika kilele cha vurugu hizo mwaka 2001.
JUMAZA inalani vikali matumizi ya nguvu kupita kiasi kulikofanywa na
vikosi vya SMZ hususan KMKM kwa hatua yao ya kutumia hata risasi za moto kwa
kuwashambulia raia wasio na hatia. Aidha na hatua ya KWTZ ya kutumia nguvu na
vitisho vilivyopelekea khofu katika eneo la uchaguzi. Aidha JUMAZA inalani
vitendo vilivyofanywa na watu wasiojulikana waliofunika nyuso zao na kubeba
silaha kuwashambulia raia. Ndugu Wazanzibar wapendwa vurugu na vitendo vya
uvunjifu wa amani na utulivu vilivyotokea katika uchaguzi mdogo katika jimbo la
Bububu vimeleta maafa makubwa yakiwemo kuwajeruhi watu, kuleta khofu ndani ya
jamii, kuharibu mali za watu, kuvunja heshima za watu na kusadikiwa kupotea kwa
maisha ya kijana wa Kizanzibari asiye na hatia kwa kupigwa risasi. Matukio haya
kwa hakika yametia doa kubwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyopatikana kwa
gharama kubwa na taufiq ya Allah (S.W)
JUMAZA inaamini kuwa vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani na
utulivu vilivyotokea katika uchaguzi huo ni miongoni mwa mikakati
inayotekelezwa na kikundi cha watu wanaopinga Serikali ya Umoja wa Kitaifa
pamoja na kupatikana mamlaka kamili ya Dola ya Zanzibar.
Kutokana na vitendo hivi, JUMAZA inaiomba SMZ kumuwajibisha kamanda
Mkuu wa KMKM pamoja na Afisa wa operesheni kwa kuliingiza jeshi hilo katika
kadhia ya kuvuruga uchaguzi katika jimbo la Bububu.
JUMAZA inamuomba Rais wetu mpendwa wa Zanzibar Mheshimiwa Dr Ali
Muhamed Shein na Makamo wa kwanza wa Rais Mheshimiwa Seif Sharif Hamad
watekeleze ahadi yao waliyoichukua pale Bwawani na JUMAZA ni mshahidi baada ya
matokeo ya uchaguzi mkuu 2010 ambapo waliahidi mbele ya Allah (SW) kuwa
watadumisha amani na utulivu na kuwalinda Wazanzibar. Kwa nia njema
tunawakumbusha viongozi wetu hawa wawe na yakini wataulizwa siku ya malipo kwa
kiasi gani wameitekeleza ahadi hiyo.
JUMAZA inawaomba Wazanzibari wote wasikubali kurejeshwa walikotoka
bali wawe na subra na kudumisha mapenzi na mshikamano wao ili kufikia malengo
makubwa waliyojipangia. Aidha Jumuiya inawaomba Wazanzibari wote kuiunga mkono
Serikali ya Umoja wa Kitaifa pamoja na kuwaunga mkono viongozi wetu wa ngazi za
juu. JUMAZA kwa upande wake itasimama kidete kuilinda Serikali ya Umoja wa
Kitaifa. Aidha Wazanzibari wote bila ya kujali sera za vyama vyao wanaombwa
kuwa tayari kupigania mamlaka kamili ya Dola ya Zanzibar kwa gharama yoyote ile
.
Mola wetu Mtukufu tunakuomba uinusuru Zanzibar na watu wake dhidi ya
maadui wa ndani na nje wasioitakia mema nchi yetu.
No comments:
Post a Comment