Kipigo cha magoli 3-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar walichopata mabingwa wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga kimeonekana kuichanganya timu hiyo iliyoangukia katika nafasi ya pili kutoka mkiani kutokana na kuwa pointi moja huku ikiwa haina hata goli moja la kufunga baada ya mechi mbili.
Viongozi wa klabu hiyo walifanya kikao cha pamoja na wachezaji wao ili kutaka kufahamu kinachoendelea katika timu hiyo kwenye makao makuu yao mtaa wa Jangwani na Mafia jijini Dar es Salaam jana.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa viongozi wa Yanga (jina tunalihifadhi) alisema kwamba uongozi umeamua kukutana na wachezaji wote ili kufahamu kama kuna tatizo au matokeo yanayopatikana uwanjani yanatokana na kuzidiwa.
Chanzo hicho kiliendelea kusema kwamba viongozi wanashangaa kuona kikosi kile kile kilichofanya vizuri katika mashindano ya Kombe la Kagame na kushinda mechi zote za kirafiki za kujiandaa na msimu kimeshindwa kuhamishia makali kwenye ligi hiyo inayoshirikisha timu 14.
"Hakuna anayedai, hakuna malalamiko, lakini wameamua kuitisha kikao ili kujipanga zaidi na kuepusha jahazi lisizame zaidi, si unajua Yanga ilivyo," alisema kiongozi huyo.
Benchi la ufundi halikuwapa mapumziko wachezaji wake na baada ya kuwasili kutoka mkoani Morogoro walienda mazoezini moja kwa moja kujiandaa na mchezo wao utakaofanyika kesho dhidi ya JKT Ruvu ambayo nayo itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kichapo cha magoli 2-0 kutoka kwa Simba.
Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet alisema kwamba ameamua kutowapumzisha wachezaji wake ili kuwafanya wachezaji wajisikie kwamba wana deni na ili kulipa deni hilo ni kuhakikisha wanashinda mechi yao hiyo ya tatu.
Katika kikao cha pamoja kati ya kocha huyo na wachezaji, Mbelgiji huyo aliwaeleza kwamba wana wajibu wa kujituma na kushinda katika mechi ya kesho kwa sababu watakuwa wamemuweka kwenye nafasi ngumu ndani ya klabu hiyo.
"Kocha ametueleza kuwa endapo tutaendelea kufungwa kuna mawili, yeye (Saintfiet) kuondoka au uongozi kumtimua," alisema mmoja wa wachezaji wa Yanga.
Kocha huyo aliwaambia wachezaji kwamba anashangazwa kuona timu inacheza vizuri lakini umaliziaji umekuwa mbovu na kupoteza nafasi wanazozitengeneza na hivyo mwisho wa mechi walijikuta wamepoteza pointi.
Alisema inashangaza kuona timu inatengeneza nafasi nane na zote inazipoteza na kuona mpinzani akitumia vyema nafasi chache alizotengeneza na kuibuka mshindi.
Kocha huyo pia alisema wachezaji wake wamekuwa wakibweteka kutokana na mafanikio waliyopata kwenye Kombe la Kagame na kusahau kuwa michuano hiyo ilimalizika na sasa wako kwenye ligi.
Aliwaambia nyota wake katika kikao cha jana kwamba wanatakiwa kubadilika haraka ili kuwapa furaha mashabiki wa timu hiyo kwa sababu wana kikosi bora kuliko timu nyingine kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Hata hivyo, Saintfiet alimtetea mshambuliaji Hamis Kiiza kwa kukosa penalti ya dakika ya 89, akisema alikuwa tayari amechanganyikiwa na kipigo, kama ilivyokuwa kwa wachezaji wenzake.
Katika mechi hizo mbili walizocheza dhidi ya Prisons na Mtibwa Sugar, Yanga haijafunga goli hata moja na imefungwa magoli matatu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment