ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 19, 2012

Malecela azungumzia mgogoro wa ziwa Nyasa

Waziri  Mkuu mstaafu, John Malecela, ameonya kuwa Serikali ya Malawi ichukue hatua ya kuyafukuza na isiruhusu tena kampuni kufanya utafiti wa gesi na mafuta ndani ya Ziwa Nyasa kabla ya tatizo la mpaka halijapatiwa ufumbuzi kwani kufanya hivyo itakuwa chanzo cha Tanzania na Malawi kugombana.
Alitoa msimamo huo juzi wakati akielezea historia ya mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwenye kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV.


“Walioanza kufanya utafiti wa gesi na mafuta ndani ya ziwa Nyasa na kuvuka upande wa Tanzania ndio wanaleta uchokozi na tunawasihi wenzetu wa Malawi wasiruhusu watu hao maana vitu hivi vitu vidogo ndio vinaleta watu kugombana, waache tumalize  kusuluhisha ifahamike mpaka upo wapi na kama itabainika mpaka upo wapi hata wakija kufanya utafiti upande wa Tanzania tutawaruhusu tu,” alisema Malecela.
Alisema ili kufikia mwafaka wa tatizo hili kinachotakiwa ni kwa kila nchi kuwa na nia nzuri kwani suala linaweza kukapatiwa ufumbuzi kama ilivyokuwa Mto Songwe.
Malecela alisema historia inaonyesha kuwa Malawi ilianza harakati za kudai sehemu ya Tanzania na aliyekuwa Rais wa Malawi Dk. Kamuzu Banda ambaye hakudai tu ziwa bali hata baadhi ya mikoa kama Mtwara na Ruvuma akidai ni sehemu ya Malawi.
Alisema Rais Banda aliibuka na hoja kwa kudai kuwa mikoa hiyo ni sehemu ya Malawi kutokana na historia ya Afrika ya kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kinaitwa na The Greate Malawi Empire kwa maana ya mikoa yote ya kusini. 
Alisema Rais wa wakati huo, hayati Mwalimu Julius Nyerere alimjibu Dk. Banda kuwa kama anadai mikoa yote ya kusini ni sehemu ya Malawi hivyo ni afadhali achukue Tanzania yote ili iungane na Malawi na kuifanya kuwa nchi moja ambapo baada ya kuelezwa hivyo suala hilo lilikwisha.
Malecela alisema katika kipindi chote msimamo wa Tanzania umekuwa ni wa kuzingatia sheria za kimataifa ambazo zinaeleza kuwa mahali popote ambapo nchi mbili zinaunganika mpaka uwe ni katikati ya ziwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: