ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 20, 2012

Mitihani darasa la saba 'yapotea' Dar

Na Masau Bwire 

MTIHANI wa taifa ya kuhitimu elimu ya msingi jana ulianza kwa dosari jijini Dar es Salaam, kwa kuchelewa kuanza kufanyika muda uliopangwa kutokana na kupotea kwa ofisa aliyekuwa akisambaza mtihani huo.


Dosari iliyojitokeza jana katika Shule za Msingi Ndumbwi na Mbezi Juu, zilizopo Manispaa ya Kinondoni ambapo mtihani ulichelewa kuanza kwa zaidi ya saa 3. Katika shule hizo mitihani ilianza kufanyika saa 5: 15 na nyingine saa 5:45 badala ya saa saa 2:00 kamili asubuhi

Mkuu wa msafara aliyekuwa akisambaza mtihani huo katika shule hizo, Bw. Jonasi Peter, ambaye ni Mratibu Elimu Kata ya Mikocheni, alidai hakuwa anajua mahali shule hizo zilipo, hali iliyomfanya apotee njia na kufika shuleni hapo akiwa amechelewa baada ya kuuliza kwa wenyeji wa maeneo hayo.


Akieleza sababu za mtihani huo kuchelewa kufikishwa katika shule hizo, mbele ya Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo Bw. Philipo Mulugo, aliyefika katika shule hizo baada ya kupigiwa simu na Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Ndumbwi, Bi. Joyce Nyamwela, kumweleza tatizo hilo, Ofisa Elimu wa Manispaa hiyo Bw. Hassan Kalinga, alisema tatizo hilo limesababishwa na uzembe wa Mratibu Elimu Kata hiyo.

Bw. Kalinga alimweleza Waziri Mulugo kwamba, alichokifanya mkuu huyo wa msafara kuchelewesha mtihani kufika katika shule hizo ni uzembe, kwani alitakiwa atembelee eneo lake kabla ya siku ya mtihani ili azifahamu shule zake lakini yeye kwa uzembe alishindwa kufanya hivyo na kusababisha yote hayo yaliyotokea.

Baada ya maelezo hayo ya Ofisa Elimu, Waziri Mulugo alimwagiza asimamie utaratibu wa chakula kwa wanafunzi hao shuleni hapo na kuzuia wanafunzi kutoka eneo la shule na simu zote za walimu zikusanywe ili kuepuka mawasiliano na shule nyingine.

Aidha Waziri Mulugo alisema, Mratibu huyo mara baada ya mtihani wa mwisho kumalizika atatakiwa kueleza sababu zilizomfanya acheleweshe mitihani hiyo na kwa nini asichukuliwe hatua kwa uzembe alioufanya, uliolenga kuvuruga usimamizi wa mitihani.

Mtihani katika shule ya Ndumbwi ulifikishwa saa 5 na kuanza saa 5.15 asubuhi wakati katika shule ya Mbezi Juu ulifika saa 5.30 na kuanza saa 5. 45.

Waziri Mulugo jana alizitembelea shule kadhaa katika Manispaa ya Kinondoni na Temeke kuangalia jinsi ulivyokuwa ukifanyika.

Shule alizozitembelea katika Manispaa ya Kinondoni ni Victoria, Makumbusho, Kijitonyama, Kijitonyama Kisiwani, Mwangaza, Ndumbwi na Hazina ambayo ni shule isiyo
ya Serikali.

Katika Manispaa ya Temeke Waziri Mulugo alizitembelea shule za Mivinjeni, Wailes na Likwati ambapo leo amepanga kuzitembelea shule katika Manispaa ya Ilala na Temeke eneo la Kigamboni.

Majira

No comments: