WAPENZI wanagombana, ndoa zinavunjika na familia nyingi zipo kwenye msoto kwa sababu ya ubinafsi. Tunazungumza mengi lakini ukweli ni kwamba endapo kila mmoja atafanikiwa kuushinda ubinafasi, upendo utashamiri kila kona.
Ubinafsi una matawi mengi. Mtu anaposaliti, maana yake ametekwa na tamaa binafsi. Anashindwa kutambua kwamba yeye ni mpenzi wa mtu, kwa hiyo anatakiwa kulinda penzi la mwenzake. Hajui kama anachokifanya ni dhuluma ya hali ya juu.
Ubinafsi una matawi mengi. Mtu anaposaliti, maana yake ametekwa na tamaa binafsi. Anashindwa kutambua kwamba yeye ni mpenzi wa mtu, kwa hiyo anatakiwa kulinda penzi la mwenzake. Hajui kama anachokifanya ni dhuluma ya hali ya juu.
Ukweli ni kwamba unapoanzisha uhusiano na mtu, maana yake umeamua kumchagua yeye ndiye amiliki penzi lako. Kwa hiyo ukienda kulitoa kwa mwingine, huo ni ubinafsi. Umeingiwa na umimi kwa kuona kwamba unatoa rasilimali za ndani ya mwili wako mwenyewe.
Kwa nini ukimfumania mwenzi wako panachimbika? Ni kwa sababu alichokitoa kwa mtu mwingine ni chako, kwa maana hiyo amekutendea dhuluma. Ndiyo maana ukawa na jeuri ya kupigana kwa sababu haki yako imetumika ndivyo sivyo.
Hivyo basi, usaliti ni ubinafsi. Umeingiwa na jeuri kwamba unacho ndani ya mwili wako, kwa hiyo unaweza kukitumia bila kumshirikisha mwenzi wako. Hiyo ni tabia mbaya mno. Kabla ya kusaliti, fikiria
utakavyoumia pindi utakaposalitiwa.
Kama inauma, ni kwa nini umtende mwenzako? Je, umemuona yeye hana moyo? Anza leo kukemea ubinafsi. Popote pale utakapoona unachukua nafasi, upinge kwa sababu ni adui mkubwa mno kwenye mapenzi. Siku zote usiseme “nipo”, sema “tupo”.
Unapozunguka, usiwaze “upo”, unatakiwa kuwaza “mpo”. Hii itakusaidia kulinda siti ya mwenzako kila utakapokwenda. Hakikisha nafasi ya mwenzi wako haichafuliwi au kutolewa mkopo. Kama ilivyo kwenye soka, wachezaji huchezea timu nyingine kwa mkopo ndivyo na mapenzi ya sasa yalivyo.
Ni kweli mtu ana mpenzi wake lakini anavyojieleza anatoa picha kwa muulizaji kuona kwamba aliyepo si muhimu sana. Hii husababisha muulizaji aombe kukaa na baadaye hukaribishwa. Wengi walikaribishwa kwa mkopo, mwisho wakawa wamiliki wa jumla.
Kwa nini umwambie huyo mtu kwamba anaweza kukaa, wakati unajua siti ina mmiliki wake halali? Kwa porojo za kitoto, eti mnaambiana mfanye siri. Kinachosikitisha ni kwamba ukisikia na mwenzako naye kagawa siti yako kwa mwingine, macho yatakutoka kwa hasira.
Si wakati wa kuchukia unapotendwa, bali unatakiwa uache ubinafsi. Haliitwi penzi bila kuwepo watu wawili. Lazima uhakikishe unalinda la mwenzako ili na lako lilindwe. Somo la mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu, linafundisha kuacha ubinafsi. Mfikirie mwingine.
Kama ambavyo ubinafsi unavyowatesa wananchi pale kiongozi mwenye dhamana kiserikali anaposhindwa kutimiza majukumu yake na kuamua kushughulikia shida zake binafsi, huku akitumia rasilimali za umma, ni kirusi hatari kila upande.
Baba anapoamua kufuja fedha wakati anajifahamu anayo familia inayomtegemea, huo ni ubinafsi. Anafikiria kutumbua yeye binafsi, wakati anatakiwa kujenga msingi wa familia. Anashindwa kujua kwamba fedha anazotafuta si zake peke yake.
Kama anaona anatakiwa kutumia fedha zake peke yake, basi hapaswi kujipa mzigo wa kumiliki familia. Mtu anapokuwa baba au mama, uamuzi wake unatakiwa uwe kwa ajili ya wengi. Kumaliza mshahara kwenye kumbi za starehe ni ukatili kwa familia hususan mtoto ambaye hakukuomba umlete duniani.
Usijidanganye kwamba unajimiliki mwenyewe. Wewe unamilikiwa na familia yako, kwa hiyo una deni na wajibu mkubwa kwa wale wanaohusika. Kabla ya kwenda nyumba ya kulala wageni na huyo unayemtamani, fikiria kwamba unamilikiwa.
Baba au mama, anapokwenda hoteli na mpenzi wa nje. Akakubali kuvua nguo na kufanya mapenzi. Ajitambue kuwa anachezea maisha ya watu wengine. Kuna maradhi, kwa hiyo unatakiwa uwe na afya njema ili wanaokumiliki waendelee kupata huduma yako.
Unafahamu kwamba mapenzi yanaua. Unaelewa kuwa unaposhindwa kuwa mtulivu nyumbani, unaiba muda wa familia yako. Kumbe sasa, fedha siyo zako ila ni za familia. Unaweza kupata picha kwamba viungo ni vyako lakini penzi si lako. Ukilitoa ni wizi, ni dhuluma iliyopitiliza.
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment