ANGALIA LIVE NEWS
Friday, September 28, 2012
Usichanganyikiwe maumivu yawe changamoto
NINA imani u mzima kwa uwezo wa Maulana, yangu hali namshukuru Muumba. Nawashukuru wote wanaosaidiwa na darasa dogo ninalotoa kwa kuyafanyia kazi yote ninayoyaandika.
Nilipokuwa mdogo niliamini wanawake wazuri na wanaume wenye fedha ndiyo wanaofaidi mapenzi, lakini baada ya kukua, nilikuta kuna tofauti kubwa kati ya uzuri, fedha na mapenzi.
Nikagundua kuwa havikai pamoja kama mafuta na maji. Najua utashangaa na kuamini mwenye fedha ndiye mwenye raha ya mapenzi. Nina imani mpaka leo wapo u wanaofikiria kitu kama hicho na kuamini mwanamke akimpata mwenye fedha au mwanaume akipata mwanamke nzuri hutulia ndani ya penzi lake. Imekuwa ni tofauti, mwanamke mzuri amegeuzwa chombo cha starehe kwa kutumiwa na wanaume, mwisho wa siku hutelekezwa kama chuma chakavu.
Si hao tu, unaweza kukuta mwanamke mzuri anampigia simu mpenzi wake, hapokei, halafu ukionyeshwa mwanamke aliyemchanganya mpenzi huyo, utashangaa. Hamfikii hata robo mwanamama wa awali.
Upande mwingine, mwanaume anampa kila kitu mwanamke likiwemo gari lakini fedha yake ndiyo inatumika kumhujumu na gari lake kwenda nje ya uhusiano.
Kuna watu ukiwaeleza haya wanaona kitu kisichowezekana au mtu kuuapia moyo wake kama angempata mwanaume au mwanamke kama yule, asingetembea nje ya ndoa mpaka anakufa. Vitu hivi vinapotokea ndipo utakubaliana na usemi wangu wa mwanzo kuwa mapenzi hayachanganywi na kitu chochote, bali yanajitegemea yenyewe, hayana gharama, hivyo ukiweka vitu hivi mbele umeumia.
Uzuri au fedha katika mapenzi ni kichocheo lakini si nguzo ya kumfanya mtu asitoke nje ya uhusiano kwa vile penzi la kweli hukaa moyoni si katika uzuri au fedha za mtu. Wengi wamechanganyikiwa na kufikia uamuzi mbaya ambao unaweza kuwaweka kwenye hatari ya kupotea kwenye dira ya dunia kwa kuamini hawana thamani kutokana na matarajio yao makubwa.
Nikuulize swali, hivi wewe mwanamke mzuri unayevutia, hata mwenyewe unaposimama mbele ya kioo bila nguo umbile lako linakuvutia na ukipita mbele ya watu hakuna mwanaume atakayeacha kukutazama na asiye mvumilivu lazima atakusemesha, kwa nini mapenzi yanakutesa? Uliyenaye haioni thamani yako kwake?
Unapiga simu hapokei au anapokea na kuonekana msumbufu na kukufokea bila sababu. Inapita hata siku mbili bila kukupigia wala kukutumia ujumbe wa simu na ukimuuliza anakujibu jibu ambalo linaonyesha kabisa hakuhitaji.
Walio pembeni wanaumizwa na majibu ya mpenzi wako na kutamani nafasi ya kukumiliki waipate wao. Unajiuliza una tatizo gani msichana mzuri kama wewe kuonekana si mali kitu kwa mpenzi wako?
Unajikuta unapandwa na hasira ya kumtafuta mwanaume mwingine ukiamini ataumia na kukutafuta. Swali linakuja, je, umejua tatizo la mpenzi wako kupoteza upendo? Unamchukua mwanaume ili kuziba pengo au umempenda?
Sehemu hii watu hukosea, usifanye tu ili mradi, thamani ya kuivua nguo yako ya ndani ni kubwa kuliko hasira zako. Hebu poteza muda kutafuta tatizo lililosababisha mpenzi wako apoteze upendo, wakati kuna watu wapo tayari kukuhonga hata gari ili wawe na wewe. Sehemu hii ndiyo itakayokugeuza uwe chombo cha starehe cha kutumiwa na wanaume wenye fedha na kukuacha. Ni kweli wewe msichana mzuri na una vigezo vyote vya kuwa mke au mpenzi wa mtu, lakini penzi lako limekuwa la maumivu, kila siku kulia, kwa nini?
Inawezekana uliamini kabisa uzuri wako ni kila kitu kwa kuamini mwanaume akikupata hawezi kukuacha, hapo ndipo unapokuwa na kiburi na dharau, hauonyeshi ushirikiano, matokeo yake yanakuwa kero kwa mwenzako na kusahau uzuri wako ndiyo uliomvuta lakini tabia zako ndizo zilizomfukuza.
Ndiyo maana nikasema mapenzi yanajitegemea, maumivu ya mapenzi yawe changamoto ya kuangalia nini tatizo ili utulie ndani ya penzi lako, ukifanya hivyo hutalia tena.
Tukutane wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment