ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 28, 2012

Dk. Slaa: CCM kinakufa


  *Ni kutokana na kushindwa kuwaengua Chenge, Lowassa
  *Atamba Chadema kushinda uchaguzi wa jiji Mwanza leo

Katibu  Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.Wilbrod Slaa, amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeonyesha kila dalili ya kufa baada ya kushindwa kuwaengua  katika nafasi za kuwania uongozi watuhumiwa wakubwa wa ufisadi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana katika mahojiano maalum yaliyofanyika kwenye  Hoteli ya Midland, Dk. Slaa alisema  alitarajia kuwa CCM kingetumia fursa hiyo kujisafisha dhidi ya ufisadi kwa kuwaengua mapema wale wote waliokumbwa na kashifa hizo.



“Katika hili nisingependa kumumunya maneno, sioni dhamira ya CCM kujirekebisha hasa kwa vile imeshindwa kuwaengua watuhumiwa wakubwa wa ufisadi,” alisema.

Alidai kwamba Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, ambaye amepitishwa kuwania Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa  (NEC) kupitia Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu, ni mtuhumiwa ambaye ushahidi upo wazi kuwa alikula rushwa kupitia ununuzi wa rada, lakini chama hicho bado kimemuona anafaa kuwa kiongozi.

“Mtu kama Chenge eti naye amepitishwa. Wote  tunafahamu kwamba alikutwa na pesa nyingi sana kwenye akaunti yake ya nje na alipoulizwa akadai eti ni za urithi, alipobanwa zaidi akadai eti alizipata baada ya kutoa ushauri, akaulizwa aliwezaje kufanya kazi hiyo wakati alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akakosa jibu,” alisema Dk. Slaa.

Aliongeza kwamba binafsi (Dk. Slaa) alipeleka ushahidi kwa Mkurugnzi wa Mashitaka (DPP) kuhusu tuhuma hizo za ufisadi dhidi ya Chenge, lakini CCM wamemuona kuwa ni kiongozi anayefaa kukiongoza chama hicho.

Katibu Mkuu huyo wa Chadema pia alimgusia Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kwamba  ni miongoni mwa watuhumiwa wakubwa wa ufisadi, lakini CCM kimempitisha kuwania ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha.

“Kabla sijaondoka bungeni nilimwambia Lowassa kwamba kwa vile amejiuzulu kwa madai kwamba anawajibika, ina maana alikuwa anamjua mtu aliyesababisha ajiuzulu, hivyo tukamtaka amtaje ili sisi tumsafishe, lakini akashindwa kumtaja,” alisema.

Chenge alituhumiwa kukutwa na Dola za Marekani milioni moja katika akaunti yake kwenye kisiwa cha Jersey, nchini Uingereza.

Fedha hizo zilihusishwa na fedha za ununuzi wa rada ya kijeshi ambayo Tanzania iliuziwa na Kampuni ya BAE-Systems ya Uingereza mapema miaka ya 2000 kwa bei ya juu tofauti na bei halisi.

Hata hivyo, mara kwa mara Chenge amekuwa akikanusha kuhusika na kashfa hiyo.

Hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari Ikulu, jijini Dar es Salaam, alimsafisha Chenge kwa kusema kuwa hapakuwepo na rushwa katika ununuzi wa rada.

Kwa upande wake, Lowassa ambaye alijiuzulu mapema Februari 2008, anatuhumiwa kuhusika katika mchakato wa kutoa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura kwa Kampuni ya Richmond ya Marekani kwa njia za upendeleo.

Kampuni hiyo ilipewa zabuni ya kuzaliwa megawati 100 wakati wa ukame mwaka 2006, lakini baadaye ilidaiwa kutokuwa na uwezo wa kuzalisha umeme huo na kulilazimisha Bunge kuunda Kamati Teule ya Uchunguzi chini ya uenyenkiti Mbunge wa Kyela, Dk. Harisson Mwakyembe.

Kamati hiyo iliwasilisha taarifa yake bungeni na kusema kuwa Richmond ilikuwa kampuni hewa, hivyo kumshauri Lowassa atafakari.

Mwingine aliyejiuzulu kutokana na sakata la Richmond  ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi.

Hata hivyo, Karamagi naye amepitishwa na CCM kugombea ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Bukoba Vijijini, mkoani Kagera.

ASEMA CHADEMA KITASHINDA UMEYA

Katika hatua nyingine, Dk. Slaa ambaye amekuwepo jijini Mwanza  kusimamia uteuzi wa wagombea nafasi za mameya na manaibu wao katika uchaguzi utakaofanyika leo kwenye Halmashauri za Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela, alisema chama chake kitashinda katika uchaguzi huo.

Alisema licha ya migogoro ambayo iliibuka ndani ya Chadema iliyosababisha madiwani kumung’ao aliyekuwa Meya kupitia chama hicho, Josephat Manyerere, kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye, lakini chama hicho bado kiko imara.

Aidha, alisema hata baada ya Chadema kuwafukuza uanachama madiwani wake wawili, Henry Matata wa Kata ya Kitangiri na Adam Chagulani wa Kata ya Igoma, lakini wananchi wasiwe na wasiwasi kwa sababu wamejipanga vizuri kuhakikisha chama hicho kinaongoza Halmashauri zote mbili.

Alifafanua kwamba Chadema hakina mgogoro isipokuwa hali hiyo imetokana na watu wengi, wakiwemo baadhi ya madiwani kutofahamu vizuri katiba ya chama hicho.

Alibainisha kwamba kinachodaiwa kuwa mgogoro ndani ya Chadema hasa katika Wilaya ya Ilemela kimefafanuliwa vizuri sana katika kanuni na maazimio mbalimbali ya vikao  vya chama hicho, lakini wapo baadhi ya watu ambao wanapotosha kwa makusudi.

Katika uchaguzi wa mameya wa Halmashauri za Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela unaotarajia kufanyika leo, kuna mchuano mkali kati ya Chadema na CCM huku kila chama kikichanga karata kuhakikisha kinanyakua nyadhifa hizo.

Kwa upande wa Manispaa ya Ilemela ambayo imemegwa kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Chadema kina Madiwani wanane na Mbunge mmoja, hivyo kuwa na jumla ya kura tisa wakati CCM kina Madiwani watano na Mbunge mmoja hivyo kuwa na jumla ya kura sita.

Hata hivyo kuna uwezekano wa Chadema kubakiwa na kura nane baada ya kumfukuza uanachama Diwani wa Kitangiri, Henry Matata, ambaye hata hivyo, kuna taarifa kuwa atashiriki uchaguzi huo kwa sababu ana pingamizi la mahakama kupinga hatua hiyo ya kufukuzwa, ingawa Chadema pia kimesema hakitambui pingamizi hilo.

Pia katika Halmashauri hiyo ya Ilemela, kuna Mbunge mmoja wa CUF ambaye kuna kila dalili kwamba atashirikiana na Chadema katika uchaguzi huo.

Kwa upande wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Chadema kina Madiwani saba na Mbunge mmoja hivyo kuwa na jumla ya kura nane, lakini kinaweza kuwa na kura mbili za ziada kutoka kwa Madiwani wawili wa CUF baada ya kukubaliana kuwaachia nafasi ya Naibu Meya.

Hata hivyo, huenda Chadema kikakosa kura ya Diwani wa Igoma, Adam Chagulani, ambaye alifukuzwa uanachama, lakini kama atashiriki uchaguzi huo kwa amri ya mahakama kama ilivyo kwa Diwani wa Kitangiri na akaamua kumpigia kura mgombea wa CCM kutasababisha mchuano kuwa mkali.

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, CCM kina madiwani saba, lakini kuna tetesi ambazo Chadema kinazilalamikia kwamba kuna mchezo unaofanyika kumhamisha Mbunge Maria Hewa (CCM) kutoka Manispaa ya Ilemela ili apige kura kumchagua Meya wa Jiji.


CHANZO: NIPASHE

No comments: