ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 28, 2012

'Mdororo wa uchumi umechangia kipigo kwa Watanzania Uturiki'


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule
Serikali imethibitisha kuvamiwa, kupigwa na kujeruhiwa kwa baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini Ugiriki na makundi ya watu ya nchini humo yanayodhaniwa kuendesha vitendo vya ubaguzi wa kuwanyanyasa wageni kwa imani potofu za kuzibiwa riziki na wageni.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule, alisema jana kuwa imani ya watu hao inatokana na hali ya uchumi  kuwa mbaya katika baadhi ya nchi za Ulaya, Ugiriki ikiwamo.



“Unajua hali ya uchumi katika baadhi ya nchi za Ulaya ni mbaya. Kuna makundi yanafanya shughuli za kibaguzi wa kuwanyanyasa wageni, kuwa wanawanyima riziki. Kwa hiyo, matukio kama hayo (ya wageni kupigwa) huwa yanajitokeza,” alisema Haule.

Alisema ndio maana wanashindwa kuunganisha tukio la kupigwa na kujeruhiwa kwa Watanzania hao na lile la daktari wa nchi hiyo, Petroula Chatzipantazi (48) aliyefariki dunia katika Hospitali ya Aga Khan, Jumapili wiki iliyopita, baada ya jaribio la kutaka kuporwa mkoba wake na watu wasiojulikana akiwa ndani ya gari, jijini Dar es Salaam.

“Ni kweli tukio hilo limetokea, lakini hakuna aliyeumizwa kiasi cha kulazwa hospitali au kufa,” alisema Haule.

Alisema katika tukio hilo, Ofisi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini humo iliharibiwa.

Picha zilizosambazwa juzi kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha namna vioo vya milango ya ofisi hizo vilivyoharibiwa.

Hata hivyo, alisema aliwasiliana na Balozi wa Tanzania mjini Roma, nchini Italia, Dk. James Msekela, lakini hadi jana alikuwa bado hajampelekea taarifa rasmi ya maandishi kuhusiana na tukio hilo.

Kuhusu daktari raia wa Ugiriki aliyevamiwa katika jaribio la kutaka kuporwa na baadaye kufariki dunia jijini Dar es Salaam, Haule alisema tayari wizara imemuandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, kumuarifu suala hilo na kwamba, ameanza kuchukua hatua kuimarisha doria ili kuhakikisha raia wa kigeni wanalindwa.

Kuhusu Watanzania waliopigwa na kujeruhiwa nchini Ugiriki, Haule alisema watashauriana la kufanya baada ya kupata taarifa ya maandishi kutoka kwa Balozi Dk. Msekela.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, alipoulizwa na NIPASHE jana kuhusiana na taarifa hiyo ya Haule, alisema polisi wana utaratibu wanaotumia kuhusu ulinzi wa wanadiplomasia.

Alisema katika utaratibu huo, kuna dawati maalum linaloratibu ulinzi kuhakikisha wanadiplomasia wote wanalindwa ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha doria katika maeneo yote wanakoishi.

Habari zilizopatikana juzi kutoka Ugiriki zilizothibitishwa na baadhi ya Watanzania hao zinaeleza kuwa unyama huo ulifanywa dhidi ya Watanzania hao usiku wa kuamkia juzi na watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chama cha Xrisi Avgi wakiongozwa na baadhi ya wabunge wa nchi hiyo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: