ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 28, 2012

Nyumba, magari, nguruwe 60 zachomwa moto


Nyumba zipatazo sita, magari mawili na nguruwe zaidi ya 60, vinavyosadikiwa kuwa ni mali ya Wakristo vimechomwa moto na watu wasiofahamika katika Wilaya ya Tunduru Mjini, mkoani Ruvuma.

Akizungumza na gazeti hili juzi kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Deusdedit Nsimeki, alithibitisha kutokea kwa matukio hayo licha ya kutokubainisha idadi ya nyumba na mali zingine zilizoteketezwa.

Nsimeki aliongeza kuwa matukio haya yametokea kwa siku tatu mfululizo tangu Septemba 7 hadi 10, mwaka huu.

Nsimeki aliongeza kuwa tangu vitendo hivyo vya uhalifu vianze kutokea, hakuna mtu yeyote aliyekamatwa na kwamba Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo inaendelea na uchunguzi kuwabaini wahusika.

Hata hivyo, baadhi ya mashuhuda kutoka wilayani humo, wamedai kuwa matukio hayo yametokea kati ya Septemba 17 hadi jana.

Kiongozi wa Kanisa la Pentekoste Tanzania lililoko wilayani Tunduru, Mchungaji Stephen Milinga, alisema usiku wa kuamkia juzi, magari mawili, moja likiwa ni mali ya mzee wa Kanisa la EAGT na lingine lenye namba za usajili T134 BGJ, mali yake yaliteketezwa kwa moto na watu wasiojulikana.

Aliongeza kuwa baada ya kutokea tukio hilo usiku huo walipeleka taarifa katika kituo cha polisi cha Tunduru Mjini. Aliongeza kuwa watu hao waliwahi kufanya tukio lingine usiku wa kuamkia Aprili 25, mwaka huu kwa kung’oa uzio wa magogo wa kanisa hilo na kuuchoma moto.



Alisema usiku huo pia walikwenda kutoa taarifa katika kituo hicho cha polisi ambapo ilifunguliwa kesi namba TUN/IR 405/2012, lakini hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa. Mchungaji alisema kati ya Septemba 17 -19 mwaka huu, nyumba zaidi ya sita na mabanda ya nguruwe vilichomwa moto na kusababisha zaidi ya nguruwe 60 kufa.

Alisema usiku wa kuamkia Septemba 19, mwaka huu watu hao walifanya jaribio la kuchoma moto mashine ya kusaga mali ya mkazi mmoja na kugonganisha nyaya za umeme, lakini  kabla ya kuleta madhara ulizimwa na wasamaria wema.

Kati ya Septemba 19-20, mwaka huu mabanda mawili ya nguruwe moja likiwa ni mali ya chungaji wa Kanisa la Biblia na Padre wa Kanisa  la Anglikana yalichomwa moto.
CHANZO: NIPASHE

No comments: