ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 28, 2012

Cuf yadai kufanyiwa vurugu na Chadema

Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF,Profesa Ibrahim Lipumba
Chama Cha Wananchi CUF kimewatuhumu wafuasi sita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jijini Arusha kwamba walihusika na vurugu za kulishambulia gari lale la matangazo na kumpiga mawe mfuasi wao huku wakilitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua za kisheria.
 
Akitoa tamko hilo jana katika ofisi za chama hicho jijini Arusha, Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa wa CUF, Mbarala Maharagande, alisema CUF kina ushahidi  wa kutosha kwamba mfuasi wao, Athuman Abdulraham, alipigwa mawe na wafuasi wa Chadema wakati akiwa katika gari la matangazo.
 
Maharagande alisema kwamba mfuasi wao alikuwa katika eneo la Levolosi karibu na eneo lililovamiwa na wamachinga na wakati akiwa ndani ya gari hilo, wafuasi wa Chadema walianza kumyooshea alama ya vidole viwili kabla ya kuanza kumpopoa kwa mawe.
 
Alisisitiza kwamba tayari mfuasi huyo ameshatoa tarifa kwa Jeshi la Polisi kufungua jalada namba AR/RB/12419/012 na kulitaka Jeshi hilo kuwakamata wafuasi wa Chadema  hadi kufikia keshokutwa na kutishia kuwa wakishindwa, wao watachukua hatua za kisheria wanazozijua.
 
“Kijana amepigwa na wafuasi wa Chadema na tayari tunawajua wako sita, tumeshatoa tarifa polisi wawachukulie hatua na kama wakishindwa, basi sisi tutachukua hatua za kisheria tunazozijua,” alisema Maharagande. 


 
Alisema wana tarifa za kutosha kuwa wafuasi wa Chadema wamefanya vurugu za kutaka kuharibu mkutano wa hadhara wa chama chao unaotaraji kufanyika Jumapili ijayo na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wao wa Taifa,Profesa Ibrahim Lipumba, na Makamu mwa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad .
 
Hata hivyo, Katibu wa Chadema moka wa Arusha, Amani Golugwa, alisema chama chake hakihusiki na madai ya CUF na kwamba hakiwezi kuwafanyia vurugu kwa kuwa kimejiimarisha. “Kama tuliking’oa chama tawala Arusha kwa nini CUF ambao siyo saizi yetu,” alisema na kuwaomba Polisi ichunguze. 
CHANZO: NIPASHE

No comments: