Mwakilishi wa kuteuliwa na rais Bi. Marina Thomas Joel akitazama picha zinazotokana na athari za uvutaji wa sigara ambapo katika mswada uliowasilishwa umeelezea athari za uvutaji wa sigara.
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi na mawaziri wote kutoka Chama Cha Wananchi (CUF) jana wametoka nje ya ukumbi la baraza hilo wakikwepa kushuhudia kiapo cha mwakilishi mpya wa jimbo la Bububu (CCM) Hussein Ibrahim Makungu.
Kutoka kwa wajumbe hao kumekuja baada ya Spika wa baraza hilo, Pandu Ameir Kificho kumwita mwakilishi huyo kwenda mbele baraza kula kiapo cha uaminifu na kuwa mjumbe wa baraza la wawakilishi kufuatia ushindi alioupata katika jimbo hilo hivi karibuni.
Wajumbe hao wa CUF walitoka nje na kusimama kwa muda fulani wakimpisha Spika amlishe kiapo hicho huku wajumbe waliopo ndani wakishangiria kwa nyimbo za kuisifu CCM na kufurahia kwa kupigapiga meza zao.
Wakati wengine wakishangiria kwa vifijo na nderemo wapo wajumbe wengine waliokuwa wakicheza ngoma na kukata viuno huku wakiimba nyimbo za kukisifu chama chao cha CCM kutokana na ushindi huo waliouita wa kishindo.
Wajumbe hao walimshika mkono na kumsogeza mbele ya Spika kwa furaha na nyimbo na kumkabidhi mwakilishi wao kwa Spika ambapo baadae Spika Kificho alimkabidhi kitabu kitakatifu cha Quraan na kula kiapo chake huku sura yake ikionesha khofu kubwa ambapo wajumbe wenzake walimpigia vigeregere na kumpa moyo.
Baada ya kuapishwa Spika alimpongeza na kuwaambia wajumbe wa baraza hilo kwamba kuapishwa kwa mwakilishi Makungu kunakwenda sambamba na siku yake ya kuzaliwa jambo ambalo lilizidisha vigeregere na vifijo ndani ya ukumbi huo ambapo wajumbe hao walimuimbia nyimbo maalumu ya kuzaliwa.
“Happy birthday to you ….Happy birthday.... Makungu ….leo ndio siku ya kufurahi” alisema Mwakilishi wa jimbo la Kitope (CCM) Mbarouk Mshimba Mbarouk huku akicheza na kupiga makofi kitendo ambacho wajumbe wenzake wakawa wanafuatilia na kuiga ubeti wa wimbo huo.
Muda mfupi baada ya kiapo Spika aliwatambulisha watu waliofuatana na mwakilishi mpya ambapo alifuatana na familia yake akiwemo mama yake mjomba wake na mkewe ambao nao walijumuika katika kikao hicho kwa ajili ya kushuhudia kiapo.
Baada ya kiapo hicho kumalizika wajumbe wa CUF waliingia ndani ya kuendelea na shunguli za kikao hicho kama kawaida ambapo televisheni ilikata matangazo yake ya moja kwa moja kitendo ambacho hakikuwafurahisha wajumbe wote wa baraza hilo kutoka pande zote mbili.
Wakati wajumbe wa CCM wakisema itabidi matangazo hayo yarejewe kwa kuwa wananchi hawajaona kiapo cha ushindi wa CCM ndani ya baraza hilo, CUF wamesema wanasikitishwa wananchi kukosa kuona kitendo cha ujasiri cha wao kutoka nje kukataa kushuhudia kiapo.
Awali akizungumza nje ya ukumbi wa baraza la wawakilishi, Abubakar Khamis Bakari ambaye ni waziri wa sheria na katiba alisema kitendo cha kutoka kwao nje ni kufikisha ujumbe kwa wananchi kwamba hawatoi mashirikiano kwa mwakilishi huyo kama chama hicho kilivyoahidi.
“Ujumbe utakuwa umefika kwa wananchi kwamba tuliahidi hatutaoa ushauri wowote kwa mwakilishi huyu kwa hivyo ujumbe utakuwa umefika hata kama televisheni imezimwa lakini wananchi wanafuatlia katika radio watakuwa wamefaamu kinachoendelea hapa” alisema Bakari.
Hivi karibuni katika mkutano wa hadhara wa chama cha wananchi CUF uliofanyika uwanja wa Bububu chama hicho kiliwaahidi wafuasi wake kwamba wajumbe wa baraza la wawakilishi wa chama hicho hawatatoa ushirikiano wowote kwa mwakilishi huyo huku taratibu za kufikisha shauri la kupinga ushindi wa mwakilishi huyo likifikishwa mahakamani.
Akizungumza katika mkutano huo aliyekuwa Naibu Katibu mKuu wa chama hicho Ismail Jussa Ladhu alisema yeye na wawakilishi wenzake hawamtambui kama ni mwakilishi halali wa jimbo la Bububu kutokana na kudai uchaguzi wa jimbo la Bububu haukuwa huru na haki na kutawaliwa na fujo.
Jumla ya kura zilizopigwa katika uchaguzi huo uliofanyika Sepemba 16 zilikuwa 6720 wakati waliojiandikishwa walikuwa ni 9799 ambapo Hussein Ibrahim Makungu (CCM) alishindwa kwa kura 3371 dhidi ya mpinzani wake wa CUF Issa Khamis Issa aliyepata kura 3204 wakati chama cha ADC kilipata kura 45, AFP kura 8, Jahazi kura 7, NCCR Mageuzi kura 1 SAU kura 4, TADEA kura 3.
No comments:
Post a Comment