ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 10, 2012

Sheria ya usafi yaleta matumaini kwa wajumbe


KUWEPO kwa Sheria ya Hifadhi na Usimamizi wa vihatarishi vya afya ya jamii na Mazingira imeelezwa kwamba kunaleta matumamini makubwa katika utekelezaji wa kazi zinazohusiana na masuala ya afya ya mazingira na jamii kwa ufanisi.

Amina Iddi Mbarouk ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii ya Baraza hilo alisema hayo wakati akiwasilisha maoni ya kamati hiyo kuhusiana na sheria hiyo na mambo mengine yanayohusiana nayo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi.


Alisema kwamba kwa muda mrefu kulikosekana sheria maalumu ambayo inasimamia masuala ya afya na mazingira jambo ambalo limepelekea kuwepo kwa udhaifu mkubwa katika kutekeleza shughuli mbali mbali za afya ya jamii na mazingira kwa ufanisi.

“Mheshimiwa Spika ni ukweli usiopingika kwamba kwa muda mrefu kumekosekana sheria maalumu ambayo inasimamia masuala haya, na kuwepo kwake sasa kunaleta matumaini makubwa katika utekelezaji wa kazi zinazohusiana na masuala ya afya ya mazingira na jamii kwa ufanisi’, alisema Amina.

Alisema kwamba katika sheria hiyo kuna ugumu mkubwa wa kufahamika kwa jamii hasa kwa vile ukizingatia umekusanya mambo mengi ambayo yanaigusa jamii moja kwa moja kama vile yanayohusiana na usafi na makaazi, usumbufu, kukinga na kuzuia maradhi ya kuambukiza, kukinga na kuzuia wadudu na panya wenye kusababisha maradhi katika jamii.


Mwenyekiti huyo amesema kutungwa kwa sheria hiyo kutatoa fursa kwa wazanzibari kuendeleza usafi na kuweka mazingira mazuri katika maeneo mbali mbali nchini kwani hivi sasa kumekuwa na tabia ya uchafu katika maeneo hasa ya mijini.


“Kamati yetu inaishauri serikali kuwaelimisha wananchi juu ya suala zima la madhumuni ya mswaada huu ili jamii ifahamu namna ya utunzaji mazingira” alisema mwenyekiti huyo.

Kuhusu utaratibu wa kuweka na kuyashughulikia maeneo ya kutupa taka, kamati hiyo imeshauri kuyazingatia maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekosa sehemu maalumu za kutupa taka kama vile maeneo mapya ya makaazi na kupelekea wakaazi wa maeneo hayo ya kutupa taka ovyo katika maeneo yasio rasmi.


“Kamati imeona kuna haja ya kuwepo kwa juhudi za makusudi katika kuhakikisha kuwa kunatengwa maeneo maalumu ya kutupia taka na wananchi wafahamu maeneo hayo” alisema Mwenyekiti huyo.

Alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza ama kuondosha kabisa kuenea kwa taka taka ovyo katika maeneo ya mji wa Zanzibar, ambapo alisema serikali za mitaa na halmashauri zake zishirikiane katika kuhakikisha maeneo hayo maalumu yanapatikana.

Aidha kamati hiyo imependekeza kiingizwe kipengele cha adhabu kwa atakayechanganya taka hatari na taka zisizo za hatari.

“Kamati imependekeza adhabu iwe kubwa kwa taasisi au kampuni kwa ajili ya kuweka kinga kwa taasisi au kampuni juu ya kutupa taka za hatari ovyo ambazo zinaweza kuleta athari kwa jamii na mazingira yetu” alisema Amina.


Amina alisema kamati hiyo imeona ipo haja kwa wizara kuendelea kuelimisha jamii juu ya madumuni ya mswada huo ili yale yaliyomo yaweze kufahamika na kuleta ufanisi katika suala zima la utunzaji mazingira katika maeneo yaliyozunguka na afya kwa ujumla.

No comments: