JUMLA ya Dola za Marekani milioni 2.6 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi mkubwa wa Umarishaji wa huduma za Mjini (ZUSP), ikiwemo uwekaji wa taa barabarani katika manispaa ya Mji wa Zanzibar imeelezwa.
Waziri wa Nchi ofisi ya rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Mwinyihaji Makame Mwadini aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kilichoanza jana mjini Unguja wakati akijibu suali la mwakilishi wa jimbo la Muyuni Jaku Hashim Ayoub (CCM) aliyetaka kujua idadi ya fedha zilizotengwa kwa ajili hiyo.
Waziri huyo alisema kuwa Serikali katika kuimarisha huduma za taa za barabarani katika maeneo ya mji ina mpango wa kudumu kwa kuweka mfumo mpya na wa kisasa wa taa hizo ambao unatumia mifumo miwili kwa pamoja kwa kutumia nguvu za jua na gridi ya taifa ili kuhakikisha mji wa Zanzibar unakuwa na taa ambazo zitakuwa zikiwaka kila siku.
Katika suali lake mwakilishi huyo alitaka kujua Serikali ina mipango gani ya kudumu ya kuhakikisha mji wa Zanzibar unawekwa taa hizo katika barabara zake ambazo zitakuwa zikiwaka kwa siku zote.
Waziri Mwadini aliwafahamisha wajumbe wa baraza hilo kwamba kwamba mpango huo wa kudumu unatarajiwa kuanza kutekelezwa mapema mwakani kwa awamu mbili tofauti, ambapo maeneo yatakoyonufaika na awamu ya kwanza ni Shangani, Mkunazini na Kiponda ambapo maeneo yote hayo yapo katika Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Mwadidini alisema kwamba awamu ya pili ya mpango huo utalenga kuweka taa katika barabara za Amani hadi Kwabiziredi, Amani hadi Mwanakwerekwe, Mwanakwerekwe hadi Kariakoo, Mnazi Mmoja hadi Kikwajuni ikiwa na lengo la kungarisha maeneo hayo na kuyaweka katika mazingira mazuri.
Sambamba na hilo alisema kuwa mpango wa kuweka taa za barabarani za Michenzani pamoja na barabara za Malindi hadi Mnazi Mmoja unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu, kupitia ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ambapo jumla ya RMB 5,000,000 zimetengwa na Serikali hiyo kusaidia mradi huo.
Baadhi ya wajumbe wametaka kujua iwapo kuna maeneo mengine yaliotengwa kwa ajili ya kuwekwa taa ikiwamo miji ya Pemba, ambapo Waziri huyo alisema serikali inafanya kazi zake kwa mipango malumu lakini itazingatia ushauri wa wajumbe wa kuangalia zaidi maeneo mengine muhimu yakiwemo huko Pemba.
No comments:
Post a Comment