ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 9, 2012

MCHEZO WA MASUMBWI, TAA INAYOZIZIMA – SEHEMU YA KUMI NA NNE


UNAPENDWA NA KUOGOPWA NA WATU WENGI DUNIANI
■UKO HATARINI KUPOTEZA ASILI YAKE KABISA


Na Onesmo Ngowi

 



Masumbwi au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa, mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa endelea………………………………….!





            Mashindano mengi ya ngumi za ridhaa kama vile mashindano ya taifa, Afrika, Jumuiya ya madola na Olimpic yatatoa nafasi kubwa kwa mabondia wetu kujenga viwango vitakavyowasaidia baadaye kwenye ngumi za kulipwa. Kuna tofauti kubwa kwa waliokwisha shiriki kwenye mashindano ya ridhaa yaliyotajwa hapo juu na wale ambao waliingia kwenye ngumi za kilipwa moja kwa moja kabla hata ya kushiriki kwenye mashindano ya ridhaa ya taifa. Tofauti hii inadhihirishwa wazi na upinzanmi wanaotoa kwenye mapambano ya ndani na nje.



            Tunajionea wazi wazi jinsi baadhi ya mabondia waliokwisha kushiriki kwenye mashindano haya makubwa yaliyotajwa hapo juu wanavyojizolea sifa kemkem hata wanaposhindwa kwenye mapambano ya nje. Hii ni pamoja na ukweli kuwa mabondia hawa wanajua mbinu nyingi za mapambano tofauti na waliojiunga moja kwa moja na ngumi za kulipwa bila ya kushiriki kwenye mashindano makubwa ya ridhaa.



Sio rahisi kwa mabondia hawa wenye viwango na misingi mzuri wa ridhaa kujiangusha chini au kukataa kuendelea na mpambano kirahisi kama wanavyofanya hawa wengine.

           

Tanzania ina mabondia wengi wanaoweza kuendelezwa na kuiletea sifa kemkem nchi hii. Ni vigumu kuelezea jinsi nchi inavyoweza kufaidika kutokana na mafanikio ya kwenye mchezo wa ngumi lakini kwa uchache tu faida zifuatazo zinapatikana;



Heshima, kuitangaza kwenye medani ya kimataifa, kuipatia pato la fedha za kigeni, watalii wengi kuijua, mabondia wengi kupata uwezekano wa kupangwa kwenye viwango vya mashirikisho makubwa ya kimataifa, kuongeza pato la taifa kwa fedha zinazopatikana kwenye mapambano mbalimbali, kutoa nafasi kwa wadau wa ngumi kualikwa kwenye semina mbalimbali za kimataifa na hivyo kuwapa nafasi ya kujenga mitandao mingi ya kimataifa na juongeza ajira.



            Ni wazi kwamba faida nyingi zitapatikana kutokana na mafanikio ya mabondia wetu. Ili kufikia mafanikio haya wadau wote wa ngumi hawana budi kushirikiana bega kwa bega ili kuendeleza mchezo huu, na hatimaye Tanzania kufanya vyema kwenye medani ya kimataifa.       Iaendelea………………………….!





Mwandishi wa makala haya ni; Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Shirkisho la Ngumi za Kulipwa Afrika Mashariki na Kati (ECAPBF), Shirikisho la Ngumi la Kimataifa bara la Afrika, Masharilki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi (IBF/AFRICA) na Mkurugenzi wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) E-mail: ibfafrica@yahoo.com

No comments: