ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 10, 2012

Serikali kufanya upembuzi wa maji ya chumvi


SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa imeshafanya jitihada mbali mbali katika kukabiliana na tatizo sugu la maji nchini kwa kufanya upembuzi yakinifu katika maeneo ambayo maji yake yana kiwango kikubwa cha chumvi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Mkaazi, Maji na Nishati Haji Makame Mwadini alipokuwa akijibu suali la mwakilishi wa jimbo la Wawi  (CUF) Saleh Nassor Juma, katika kikao cha baraza hilo kilichaonza jana hapa Zanzibar.

Alisema kwamba katika kufanikisha hilo tayari Mamlaka ya Maji imeshafanya majaribio ya kuyachuja maji ya bahari katika eneo la chuo cha usimamizi wa fedha Chwaka kwa matumizi ya chuoni hapo na maeneo ya jirani.

Alisema kwamba majaribio hayo yalifanywa kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani, chini ya Kampuni ya DOW na Mork Solution.

Hata hivyo alisema kuwa kukauka kwa vyanzo vya Maji asili kunatokana na mabadiliko ya tabia nchi tatizo ambalo si la Zanzibar pekee bali ni kwa nchi zote duniani.

Katika suali lake mwakilishi huyo alitaka kujua ni lini Serikali itafikiria kuyachuja maji ya bahari na kuweza kutumika kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kama inavyofanywa na baadhi ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea.

No comments: