ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 15, 2012

serikali kuunda shirika la nyumba


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema mchakato wa kuanzisha shirika la nyumba la taifa ambalo litasimamia maendeleo ya nyumba zinazomilikiwa na Serikali ya Zanzibar unaendelea.

Naibu waziri wa Ardhi Makaazi, Maji na Nishati, Haji Mwadini Makame alipokuwa akijibu swalililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Wawi (CUF) Saleh Juma Nassor aliyetaka kujuwa mipango ya serikali ya kuzifanyia ukarabati nyumba za serikali wanazoishi wananchi Unguja na Pemba ambazo kwa sasa zipo katika hali mbaya.

Katika suali lake la msingi Mwakilishi huyo alitaka kujua ni sababu zipi zilizopelekea serikali kushindwa kuzitunza na kuziendeleza nyumba hizo na kuzijenga upya.

Naibu waziri huyo alisema lengo la serikali ni kuwatengeneza wananchi wake makazi mazuri ya kuishi na lengo la serikali kuendelea juhudi za Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ambaye alianzisha mpango wa kujenga nyumba za maendeleo kwa wananchi.

“Katika jitihada za kuwapatia wananchi nyumba bora na za kisasa, serikali kwa kusudi hivi sasa inaendelea kuyatarisha sheria ya uanzishaji wa shirika la nyumba, ikiwa ni imani kuwa shirika litaziendeleza na kuzitunza nyumba zilizopo na pia shirika litakuwa na nguvu na uwezo wa kisheria kuibua miradi mipya na ujenzi wa nyumba za makaazi katika visiwa vyetu” alisema Waziri huyo mbele ya wajumbe wa baraza la wawakilishi.

Alisema mbali na shirika la nyumba bado serikali inaendelea kuwasiliana na wawekezaji mbali mbali ili kuweza kuwekeza katika ujenzi wa nyumba za makaazi.


Mwadini alisema ingawa ni kweli nyumba hizo zilijengwa na Marehemu Mzee Karume katika maeneo mbali mbali ikiwa ni sehemu ya maendeleo katika vijiji na miji ya Unguja na Pemba ikiwa na lengo la kuwasaidia wananchi wa visiwa hivyo kupata makaazi bora na yalio salama lakini ni muda mrefu na ndio maana nyumba hizo zimeanza kuchakaa kutokana na kuwa ni za muda mrefu.

Alisema licha ya kuwa nyumba hizo zilijengwa miaka mingi lakini katika awamu hii pia imejenga nyumba kwa ajili ya wananchi na bado inaendelea na mpango wake wa kuwarahisishia wananchi wake katika makazi yalio bora zaidi kwa kuwa na nia ya kuendelea majengo mapya zaidi.

“Serikali imeona upo umuhimu wa kuunda shirika la nyumba la taifa ikiwemo kusimamia maendeleo ya nyumba hizo pamoja na kuzifanyia ukarabati ili ziwe katika mazingira mazuri ya kuishi wananchi”. Alisema waziri huyo.

Hata hivyo alisema ni kweli nyumba hizo zipo katika hali mbaya kwa sasa kiasi ya nyengine kuhatarisha maisha ya wananchi kutokana na uchakavu wake kwa mfano nyumba ziliopo vijijini kwa kiasi kikubwa zimechakaa na kuharibika kabisa.

“Sera ya kuwapatia wananchi makaazi bora na salama yapo pale pale” aliahidi waziri huyo.

Alisema nyumba nyingi za maendeleo ni kweli kuwa zipo katika hali mbaya na zinahitaji matengenezo makubwa na hii inatokana na kukosekana kwa fedha za kuzifanyia matengenezo nyumba hizo.

Aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba fedha zilizopatikana kwa matengenezo kwa sasa zinaelekezwa kwa kufanya matengenezo ya makaro na mabomba ya maji machafu katika nyumba hizo.

Alizitaja baadhi ya nyumba ambazo kwa sasa zipo katika hali mbaya huko vijijini Unguja na Pemba ikiwemo Macho Manne,Kengeja.Vitongoji pamoja na Micheweni kwa upande wa Pemba pamoja na nyumba ziliopo Gamba na Bambi.

Mwadini alifafanua na kusema kwamba nyumba hizo kwa sasa zinakabiliwa na matatizo mbali mbali ikiwemo kuharibika kwa mfumo wa maji taka,ambao umeharibika kabisa na kusababisha uchafu.

'Ni kweli nyumba za wananchi za maendeleo zipo katika hali mbaya ya uchakavu wa maeneo mbali mbali ikiwemo mfumo wa maji taka ambao umeharibika na kusababisha uchafuzi wa mazingira yake'alisema.

Waziri wa wizara hiyo Ramadhan Abdalla Shaaban naye akitoa ufafanuzi zaidi alisema kwamba hivi sasa kumejitokeza vitendo mbali mbali vya uharibifu wa makusudi wa nyumba za maendeleo ikiwemo wizi wa vifaa vya nyumba hizo ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiharibiwa na wananchi wenyewe na hivyo kuiunja moyo serikali ambayo imekuwa na lengo zuri kwa wananchi wake.


Shaaban alitoa mfano nyumba nambari 11 ambayo walipewa wananchi na kubakia vyumba vitano ambavyo katika kipindi kifupi watu wasiojulikana waliiba milango na madirisha pamoja na vioo jambo ambalo amesema halipendezi kwa mutakabali wa maendeleo ya nchi.

“Tunasikitika sana hivi sasa jamii yetu imekuwa na tabia mbaya ya kujishungulisha na vitendo vya wizi wa mali za serikali kwa mfano katika nyumba nambari 11 watu wameiba milango na madirisha na wamengoa vioo ….sasa hiyo sio tabia njema hata kidogo iweje serikali iwatengenezee wananchi wake maakazi mazuri halafu hao hao wawe wanaharibu?” alihoji waziri huyo.

Suala hilo Shaaban alisema  upo umuhimu mkubwa wa kuanzisha shirika la nyumba kwa ajili ya kutunza nyumba za serikali ili kuziweka katika mazingira mazuri.

No comments: