ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 10, 2012

TEKNOLOJIA YA LIVELINE KUMALIZA TATIZO LA UMEME


MC DONALD AKIONESHA , NAMNA LIVELINE INAVYOFANYAKAZI BILA KUKATA UMEME 
Na Khadija Kalili, aliyekuwa Morogoro
“MIMI nilikuwa Mkufunzi Chuo cha Shirika la Umeme(Tanesco) Morogoro. Tulikuwa tunafanya matengenezo bila kuzima umeme… Tanesco haihitaji kuzima umeme, teknolojia hii ilitambulishwa na shirika hilo,  lakini baada ya Chuo kufa nayo ikafa.”
Hayo ni maneno ya Donald Mwakamele ambaye ni Mhandisi na Mmiliki wa Chuo Mc Donald Live Line Training Centre   kilichopo Dakawa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro kinachotarajiwa kuanza kutoa mafunzo ya umeme.
Kutokana na utashi aliokuwa nao ameamua kujenga Chuo hicho  kitakachotoa elimu ya teknolijia ya Live Line inayohusu masuala ya ufundi bila kuzima umeme, ambacho hadi sasa kimegharimu zaidi ya sh milioni 900.
Hivi karibuni Tanzania Daima ilifika katika Chuo hicho na kukikuta kikiwa katika hatua za mwisho kukamilika.
Akizungumza chuoni hapo Mwakamele anasema chuo kitaleta faida kubwa nchini huku teknolojia hiyo ikiweza kunusuru mamilioni ya fedha zinazopotea kutokana na kukata umeme wakati wanapofanya matengenezo. 
Mwakamele ambaye alifanya kazi Tanesco kwa miaka 15 anasema aliwasilisha mawazo kwa wataalamu wa umeme kutoka nchi mbalimbali ambao waliangalia teknolojia hiyo licha ya kutotumika sasa nchini. 
“Sasa hapa tunaweza kuendelea na matengenezo yetu hata ya kuondoa kikombe kwenye muunganiko, lakini siyo lazima tuzime umeme ambao unailetea hasara kubwa Tanzania kwa ujumla. 
“Unapozima umeme nchi  nzima kwa dakika kumi tu, hasara inayopatikana ni kubwa sana  na haielezeki , hivyo upo ulazima wa kuondoka huko, ndiyo maana nimeona niendeleze wazo la Rais Kikwete na juhudi hizi zifanikiwe kabla hajamaliza muda wake wa kuongoza taifa,” anasema Mwakamele. 
Mwakamele anaongeza kwa  kusema kwamba teknolojia hiyo itakuwa tiba mbadala kwa nchi ya Tanzania ambayo imegubikwa na matatizo makubwa katika nishati ya umeme. 
"Hakika teknolojia hii ikitumiwa ipasavyo na Mainjinia wa Tanesco, wataweza kufanya matengenezo bila kuzima umeme hatua itayoikomboa nchi na tatizo la kuzimwa kwa umeme, pindi wanapofanya matengezo," anasema.
Mafunzo
MC Donald anazungumzia kuhusu  mafunzo yatakayokuwa yakitolewa katika chuo hicho ni kwamba atakuwa Mwalimu. 
Anasema chuo hicho kitatoa fursa kwa wanafunzi kutoka Kenya, Uganda  na Malawi ambao  nchi zao hakuna wataalamu wa teknolojia hiyo.
Mkufunzi huyo anasema Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) itafanya ukaguzi wa chuo hicho  na kutoa tathmini.
 Mbali na hilo anatoa rai kwa wanafunzi wanaochukua mchepuo wa sayansi kwamba watapata fursa ya kujiunga kupata mafunzo hayo muhumi kwa muda mfupi wa wa miezi  mitatu wa mrefu miaka mitatu.
  “Nitafundisha elimu hii ya Live Line huku mkandarasi akitoka hapa atakuwa na vifaa  seti nzima ili isiwe tabu kwake kufanya kazi huko aendako,” anasema. 
Kwa mujibu wa Mwakamele, chuo hicho kitaanza kwa kutoa elimu kwa wadau wakubwa wa umeme, wakiwamo mainjinia na maprofesa ili elimu hiyo iweze kusambaa haraka katika  kila mkoa na kuondoka kwenye ubabaishaji huo.
Anasema endapo Chuo hicho kitaanza kazi haraka iwezekanavyo, wakazi Dar es Salaam huenda wakanufaika zaidi, maana ndiyo sehemu za nchi hii ambayo umeme wake umekuwa sio wa uhakika. 
MC Donald alikuwa Mkufunzi katika Chuo cha Tanesco kwa miaka 15 akiwa kati ya Watanzania wachache waliopata mafunzo ya elimu ya Live Line  iliyotambulishwa rasmi mwaka 1988 na Rais Jakaya Kikwete  na kuitumia kwa muda wa miaka 20 lakini hivi sasa haitumiki tena.
Anaongeza kwa kusema kuwa yeye sio Mkandarasi bali ni Injiania hivyo haoni sababu ya kuificha elimu aliyonayo hivyo anaona bora awarithishe kizazi kipya na yeye abaki kuwa Mwalimu wa Live Line.
 “Kwa kuwa nina nia nitatafuta Injiania mmoja kila Mkoa niwasuke  vijana wa  Chuo Kikuu  tuwape chachu  ya kuchukia  kuzima umeme,”anasema.  
Anasema  viongozi waliopo madarakani watambue kwamba lile Tanesco ni Shirika la Umma na siyo la mtu binafsi, hivyo ni hatari kuicha jinsi ilivyo.
 
 “Ni fedheha kwa uongozi wa Tanesco Morogoro kunihujumu na kuwakosesha wananchi wenye kiu ya maendeleo… teknolojia hii imefanyakazi kwa miaka 20 iliyopita hapa nchini,” anasema Mwakamele.
Awali aliishangaa serikali kuikataa teknolojia hii ambayo ilitambulishwa mwaka 1988 na kufanyakazi kwa ufanisi huku akisisitiza kwamba teknolojia hiyo ina uwezo wa kufanya matengenezo ya umeme bila kuathiri huduma hiyo kwa wananchi.
 
Kabla ya ziara hiyo Mainjinia  hao  walikuwa wakihudhuria mkutano mkubwa  wa sekta ya Umeme  Afrika Mashariki (EAPIC), uliofanyika Dar es Salaam na kuwatanisha watendani wakuu wa kampuni  26  kutoka nchi mbalimbali  zinazohusisha  na nishati ya  umeme  katika Bara la Afrika.
 Mainjinia hao walioneshwa  jinsi teknolojia ya Live Line inavyofanya kazi  na kuelezwa kwamba kama itaanza kutumika itaokoa kiasi kikubwa cha fedha  kwani kwa kukata umeme  wakati wa matengenezo  huleta hasara kubwa  kwa nchi na mzigo kwa wananchi.

No comments: