Dk Abdallah Kigoda.
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda ameivunja Bodi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kutekeleza nia ya wizara hiyo ya kuboresha utendaji kazi wenye tija na ufanisi katika shirika hilo.
Uamuzi wa kuvunjwa kwa bodi hiyo umekuja miezi sita baada ya Dk Kigoda kuitaka bodi hiyo kumsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa TBS, Charles Ekelege ili kupisha taratibu za kisheria ikiwamo suala la uchunguzi kufanyika dhidi yake.
Akizungumzia uamuzi huo, Dk Kigoda amesema umetokana na bodi hiyo kutokuwa na tija na ufanisi kama ilivyotarajiwa.
“Shirika hili ni nyeti sana kwa taifa, hivyo ni lazima tuimarishe bodi ili kuhakikisha inafanya kazi kama inavyotarajiwa na wananchi,” alisema Dk Kigoda.
Alisema kuwa pamoja na wizara kutoa maagizo ya awali yaliyoitaka bodi kuhakikisha inafanya kazi kwa ufanisi, bado bodi ilishindwa kufanya kazi kwa tija na ndiyo maana wizara imechukua uaumuzi wa kuvunja bodi hiyo.
“Tutahakikisha bodi mpya inapatikana haraka ili kutokwamisha shughuli za shirika hili nyeti,” alisema Dk Kigoda.
“Tutahakikisha bodi mpya inapatikana haraka ili kutokwamisha shughuli za shirika hili nyeti,” alisema Dk Kigoda.
Bodi hiyo imevunjwa miezi michache baada ya kuapishwa mwezi wa tatu mwaka huu na aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyrill Chami,
Waliokuwa wajumbe wa bodi hiyo iliyovunjwa ni mwenyekiti wa bodi Oliver Mhaiki, Donald Chidomu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Rashidi Salimu kutoka Wizara ya Viwanda Zanzibar, Dk Bertha Maegga kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Odilo Majengo kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara.
Wengine ni Profesa Ntengwa Mdoe kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine, Peter Mahunde kutoka Shirika la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Mariki kutoka Tume ya Ushindani, Suzi Leizer kutoka shirikisho la mashirika madogo na ya kati (SMEs) na Elpina Mlaki kutoka Wizara ya Fedha.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza tangu atepoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Waziri wa wizara hiyo takribani miezi sita iliyopita, Dk Kigoda aliiagiza TBS kumsimamisha kazi Ekelege kutokana na kuibuka kwa mjadala mkali bungeni juu ya utendaji kazi wa shirika hilo.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), chini ya Makamu Mwenyekiti wake, Deo Filikunjombe ilimtuhumu Ekelege baada ya kubaini kuwepo kwa udanganyifu kwenye mpango wa TBS kukagua bidhaa nje ya nchi.
Filikunjombe alieleza kuwa waligundua madudu baada ya kutembelea vituo vya ukaguzi wa magari nchini Singapore na mjini Hong Kong, China. “Tulikwenda Hong Kong na Singapore na tumegundua kwamba TBS ni wababaishaji, huwezi kuamini anachokifanya Mkurugenzi (Ekelege) huko nje.”
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa kamati, Ekelege aliwapeleka katika ofisi hewa ambayo baadaye waligundua kuwa haikuwa ya ukaguzi wa magari.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment