ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 23, 2012

Kili Stars 'full' kujiamini Chalenji


Kocha wa Kilimanjaro Stars,  Kim Poulsen 
KOCHA Kim Poulsen amesema anakwenda na Kilimanjaro Stars Uganda kushiriki fainali za Chalenji akiwa na dhamira ya kufuta dhana ya utumwa wa kutokuwa na imani na kikosi chake inayowasumbua mashabiki wengi wa soka nchini.
Poulsen ataiongoza Stars kwa mara ya kwanza kushiriki Chalenji tangu alipochukua nafasi ya kuifundisha timu hiyo akirithi mikoba ya mtangulizi wake, Jan Poulsen.
Stars haijawahi kutwaa taji la Chalenji nje ya ardhi ya Tanzania tangu ilipofanya hivyo kwa mara ya mwisho mwaka 1965 na 1994 Uganda na Kenya.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu akiwa Mwanza jana, Poulsen alisema yeye binafsi na wachezaji wameshaweka malengo ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.
"Ni kweli, historia inahukumu tumeshindwa kufanya vizuri ugenini, na hii imekuwa kama dhana iliyokwepeka kwa mashabiki," alisema Poulsen.
"Lakini sasa dhamira yetu ni kuwaonyesha Watanzania kuwa, nafasi ya kufanya vizuri ugenini tunayo na tutafanya hivyo," alisema Poulsen.
"Tunachokifanya kwa sasa ni kujindaa vizuri kwa lengo la kutwaa ubingwa na siyo kinyume chake.
"Kama historia ingekuwa na nafasi, basi siku zote Brazil, Hispania na Uholanzi zingekuwa zinashinda wakati wote. Nadhani muhimu ni maandalizi ya mipango madhubuti tu."
Wakati huuo Kim alisema, msafara wa kikosi chake utaondoka Mwanza leo kuelekea Kampala tayari kushiriki michuano ya chalenji.
Hakuna majeruhi kwenye kikosi changu kwa sasa, wachezaji wote wana afya njema. Tunakwenda tukiwa na matumaini ya kufanya vizuri," alisema Kim.
Aidha, Meneja wa Kilimanjaro Stars Leopold Taso Mukebezi, amesema kuwa kikosi cha timu hiyo kipo tayari kwa ajili ya michuano hiyo.
Alisema:"Hali ya hewa ya Mwanza ni sawa na ya Uganda na viwanja vingi ni vya nyasi za kawaida kama ambacho tunafanyia mazo.
Kikosi kinaendelea vizuri, wachezaji wote kwa jumla wapo katika hali nzuri na wana ari na morali ya kucheza kwa mafanikio."
Mwananchi

No comments: