ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 26, 2012

Dk Slaa: CCM wasubiri majibu 2015

KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema CCM watazunguka nchi nzima lakini majibu yatajulikana 2015 kwani ndiyo utakuwa mwisho wao.
Pia Dk Slaa amesema Chadema hakiyumbishwi na kuahimia CCM kwa waliokuwa madiwani wake mkoani  Arusha, na badala yake kinapata nguvu ya kuweza kusimamia maadili ya viongozi wake.
Dk Slaa alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na gazeti hili kuhusu mambo mbalimbali ya kisiasa yanayoendelea nchini, ikiwa ni siku moja tangu uongozi wa juu wa CCM ukiongozwa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahaman Kinana umalize ziara yake ya kwanza katika Mikoa ya Mtwara, Rukwa, Geita na Arusha.
Alisema Chadema siku zote kitabaki kuwa mwalimu na vyama vingine vitafuata kwa kuiga mambo ambayo chama hicho kimeyaanzisha.
“CCM kuzunguka huku na huko na ni kutuiga sisi kwani tumeanza muda mrefu, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 tumekuwa tukizunguka na kuwaeleza wananchi mambo mbalimbali,” alisema Dk Slaa na kuongeza;
“Wao (CCM) wazunguke tu lakini mambo yote yatajulikana 2015 kwani Watanzania wa sasa siyo wa kudanganywa tena.”
Dk Slaa alisema anashangaa kwa nini CCM wanazunguka huku wakilalamika wakati wao ndiyo wanaiongoza nchi hivyo majibu ya matatizo ya wananchi wanayo.“Chadema ni mwalimu na wao hufuata, waendelee na mzunguko wao lakini waache kulalamika kama sisi bali watoe majibu kwa kuwa wao ndiyo wanaongoza Serikali,”alisema Dk Slaa.
Akizungumzia baadhi ya madiwani wa chama hicho waliohamia CCM, Dk Slaa alisema kuwa hawakiyumbisha chama chao na kwamba hata kama wamehama wasipolipa Sh15 milioni kama amri ya mahakama ilivyotolewa watakwenda jela.
Juzi katika mkutano wa CCM Arusha, madiwani wa Chadema walitangaza kujiunga na CCM huku wakipinga hatua ya Dk Slaa, kuwa alikuwa akitaka kuwafunga baada ya kuwatimua ndani ya chama hicho.
Madiwani hao ambao walitimuliwa na Chadema kutokana kitendo chao cha kumtambua Meya wa Jiji la Arusha Gaudensi Lyimo wa CCM ni Rehema Mohamed, Simba Salum wa Kata ya Kati na Frank Joseph Takachi wa Kata ya Olasiti.
Jana Dk Slaa alisema kitendo hicho kinaonyesha jinsi gani kuna wanasiasa ambao ni matapeli hapa nchini kwani madiwani hao walikwenda mahakamani kutaka warudishiwe uanachama wao sasa wamekimbilia  CCM. “Watanzania sasa wanajua aina ya wanasiasa matapeli, kama walienda mahakamani kuomba uanachama wanahangaika nini,”alisema Dk Slaa na kuongeza; “Chama hakitayumba na tutaendelea kusimamia maadili ndani chama kama ilinavyotakiwa.” Alisema baadhi ya madiwani wameshaanza kulipa fedha ambazo mahakama imesema, hivyo hao waliokimbilia CCM wasipolipa fedha hizo ndani ya miezi miwili watakwenda jela kama mahakama ilivyosema.
NCCR wanena
Katika hatua nyingine Chama cha NCCR-Mageuzi kimemtaka Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzania Bara,  Philip Mangula kushughulikia rushwa ndani ya chama hicho kwa muda wa siku saba na siyo miezi sita kama alivyoahidi.
Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Faustin Sungura amesema vinginevyo chama hicho kitawahamasisha wananchi waikatae CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Sungura alisema wahusika wa rushwa wanafahamika na ametoa siku hizo kutokana na kuona miezi sita ni mingi na watendaji wa vitendo hivyo wanafahamika katika chama na Serikali na kwamba kinachokosekana ni dhamira ya dhati ya kuchagua viongozi wenye mikono safi.
Alisema kwa hali ilivyo sasa, wananchi wanaoombwa rushwa hawana mahali pa kulalamika na kusikilizwa, hali ambayo imeendelea kuchangia kukua kwa vitendo hivyo.
“Tunakitaka Chama cha Mapinduzi, kiiagize Serikali yake, iwape madaraka watu wenye mikono safi na ambao watakomesha tatizo hili ndani ya muda mfupi ili muda mwingine utumike kupanga mambo ya maendeleo,” alisema Sungura .
“Hilo ndilo ambalo litatokea, kama wasipochukua hatua hivi sasa kani tutawahamasiaha wananchi kufanya ukomo wa CCM uwe 2015”.
Mwananchi

No comments: