ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 2, 2012

KAULI ZENYE ISHARA MBAYA KATIKA UHUSIANO - 3

MATATIZO katika maisha ni jambo la kawaida, kila siku lazima utakutana na changamoto ambazo zinahitaji utatuzi. Hata katika mapenzi ni hivyohivyo, kutofautiana kwa wapenzi kupo.

Achana na kuwaza namna ambavyo mpenzi wako amekuwa akikukosea; sogea mbele zaidi na uanze kufikiria ni kwa nini anakukosea. Angalia kwenye mzizi. Mfundishe, mwelekeze polepole.
Katika mapenzi, unapotumia lugha ya taratibu kumuelekeza mwenzako anaelewa vizuri zaidi na anakuwa katika nafasi ndogo sana ya kurudia makosa kuliko kutumia lugha ya ukali ambayo huiona kama kawaida yako tu na anaendelea kubaki na maudhi yale yale.
Hili kwako liwe somo la utangulizi wakati tunakwenda kuhitimisha mada yetu iliyokuwa hapa kwa wiki ya tatu leo. Nazungumzia kuhusu kauli zenye ishara mbaya kutoka kwa mpenzi wako.
Tayari nimeshaainisha kadhaa, lakini jambo kubwa ambalo unatakiwa kulifahamu ni kwamba, wakati mwingine mwezi wako anaweza kutamka jambo ukadhani ni la utani, lakini kumbe ndani yake kukawa na ujumbe mzito. Kujua maana zaidi hakutakusaidia kitu kama hutalifanyia kazi. Tuendelee...
HUSISIMUI
Hii ni kauli nyingine mbaya unayoweza kuambiwa na mpenzi wako. Ukisikia mpenzi wako anakuambia hivi, anza kuwa na mashaka naye. Unajua unapoambiwa husisimui, maana yake humshawishi na anakuona wa kawaida tu.
Hii haina tofauti kubwa na ambaye anakuambia hakutaki tena au yupo kwenye uhusiano na wewe akipoteza muda tu. Ikitokea ukiambiwa hivi, fumbua macho yako ndugu.
HUJUI KITU
Mara nyingi kauli hii ni ya kukushusha uelewa au kukuonesha kwamba hujui mambo. Kwa bahati mbaya, labda mlikuwa mnajadiliana jambo, wewe ukichangia chochote, anakukatisha na kukuambia hujui kitu.
“Unaongea nini wewe, hebu nyamaza bwana, hujui kitu kabisa,” anaweza kukutamkia kauli hii hata kama kuna watu wengine jirani yenu. Hii si kauli nzuri kwa wapenzi kuambiana.
Mwenzi wako akikuambia hujui kitu, maana alikosea sana kuchagua, hasa kutokana na ukweli kwamba hakuna anayependa kuishi na mtu asiyejua kitu!
LUGHA CHAFU
Wakati mwingine mkiwa mmetofautiana ni mwepesi wa kutoa maneno makali na hata kukutukana. Hana hofu juu ya hilo kabisa, kwani haoni kama kukuheshimu ni sehemu ya kuonesha mapenzi yake ya kweli.
Ni rahisi kukukashifu, wakati mwingine hata mbele za watu unaowaheshimu. Hajali wala haoni kama unahitajika kuheshimiwa kama mwenzi wake. Hii ni dalili mbaya kwamba mwenzi wako ana kitu kingine kichwani mwake.
HATAKI MAHABA
Hii ni alama nyingine tena, hapendi aina yoyote ya mahaba. Hataki utani wa kimapenzi na mambo yanayohusiana na mahaba kwa ujumla wake.
Mbaya zaidi, inawezekana mkawa mpo faragha, akakataa kushirikiana na wewe katika michezo ya kimapenzi, kana kwamba anakuonea kinyaa! Hili ni tatizo rafiki zangu.
Kama wewe ni mpenzi wake anayekupenda kwa nini ashindwe au akatae kufanya mahaba na wewe? Hapo lazima ujifunze kitu kichwani mwako.
Umewahi kuona wapi mapenzi yakawa na kinyaa? Mapenzi yakawa na mipaka?
KWAKO SASA
Naamini umefunguka na unajua maana ya kauli chafu anazozitoa. Kamwe usiwe katika penzi la majaribio. Jifunze kupitia kauli zake, fanya uchunguzi, halafu mwishoni ytutapata jibu la moja kwa moja.
Si busara kuwa katika penzi la utumwa na manyanyaso. Kuwa na mwenzi ambaye anaonekana dhahiri hashtushwi na uwepo wako, hatambui thamani yako ni wa kumfikiria mara mbili.
Amua mwenyewe, kuendelea kubaki na mateso au kutua matatizo na kusonga mbele katika maisha yako.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani

No comments: