ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 2, 2012

Mgogoro wa dini wakimbiza Mkuu wa shule, wanafunzi


Mgogoro mkubwa umeibuka katika Shule ya Sekondari ya Bagamoyo mkoani Pwani kati ya wanafunzi wa Kiislamu na Kikristo na kusababisha Mkuu wa Shule hiyo, Bonus Ndimbo, kuikimbia shule na familia yake kuhofia usalama wa maisha yake.

Pia, baadhi ya wanafunzi wa Kikristo wamekimbia shule hiyo na kurejea majumbani mwao kutokana na vitisho wanavyopewa.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salehe Mbaga, akizungumza na NIPASHE jana kwa simu, alithibisha kuwepo kwa mgogoro huo, lakini alisema hajapata taarifa za kukimbia kwa Mkuu wa Shule.

“Kama kweli Mkuu wa Shule amekimbia shuleni atakuwa amefanya vizuri kwa sababu alikuwa hatakiwi na wanafunzi,” alisema Mbaga ambaye hata hivyo, hakutaka kufafanua zaidi chanzo cha mgogoro huo.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi, alipotafutwa, alisema mgogoro huo upo, lakini alikataa kutoa maelezo zaidi na hatua zilizochukuliwa yatolewe na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.

Hata hivyo habari zilizopatikana shule hapo zinaeleza kuwa mgogoro huo ulianza wakati wa mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa serikali ya wanafunzi.

Wakati wa uchaguzi huo walijitokeza wagombea wawili wa nafasi ya Kilanja  Mkuu wa Shule, Answal Abdul na Emmanuel Mmari ambao walikuwa wakichuana nafasi hiyo. Wote ni wanasoma kidato cha tano.



Chanzo cha habari kinaeleza kuwa kampeni zilipoanza wanafunzi wa Kiislamu ambao baadhi yao ni viongozi wa msikiti uliopo shuleni hapo, walianza kumpigia kampeni mgombea wa dini yao na wa dini ya Kikristo walianza kufanya hivyo.

Habari zaidi zinaeleza kuwa wakati kampeni zikiendelea, inadaiwa Mkuu wa Shule aliwasihi wanafunzi wa Kiislamu waache kupiga kampeni kwa kufuata misingi ya dini.

Kauli hiyo ya Mkuu wa Shule inadaiwa iliwakera wanafunzi wa Kiislamu ambao walichukua uamuzi wa kumuondoa katika kinyang’anyiro mgombea wa waliyekuwa wakimpigia kampeni, Answal Abdul na kubakia mgombea pekee Emmanuel Mmari.

Habari zinaeleza kuwa siku ya uchaguzi wanafunzi wote walishiriki, lakini wanafunzi wa Kiislamu licha kupewa karatasi za kupigia kura hawakuandika chochote katika karatasi hizo huku wanafunzi wa Kikristo wakipiga kura.

Baada ya uchaguzi huo, Mmari alichaguliwa kuwa Kiranja Mkuu wa shule hiyo.

Mkuu wa Shule hiyo, Ndimbo baada ya kukamilika uchaguzi huo alitangaza siku ya kuapisha viongozi wa serikali ya wanafunzi waliochaguliwa na ndipo mgogoro ulioanza.

Siku ya kuapisha viongozi hao, wanafunzi wa Kiislamu inadaiwa walimvamia Mkuu wa Shule na kumnyang’anya karatasi zilizokuwa zimeandika majina ya viongozi waliopangwa kuapishwa,  hali iliyozua vurugu ambazo hata hivyo, baadaye zilitulia.

Mtoa habari watu amesematangu siku hiyo wanafunzi wa Kiislamu walianza kushinikiza Mkuu wa Shule ahamishwe na kwamba hawautambui uongozi wa shule uliochaguliwa na pia hawataki walimu Wakristo shuleni hapo.

Habari zaidi zinasema kuwa vitisho viliendelea na kuwa nyakati za usiku watu wasiofahamika walikuwa wakipita na pikipiki kuzunguka mabweni na shule.

Kutokana na hali hiyo, wanafunzi wa Kikristo waliamua kuondoka shuleni hapo kurejea majumbani hadi sasa kuhofia usalama wa maisha yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Samuel Saliyanga, alipoulizwa alisema bodi ya shule hiyo ilikuwa inakutana jana kutoa maamuzi ya suala hilo na kwamba yeye atapata taarifa kupitia kwa Afisa Elimu ya Sekondari.
CHANZO: NIPASHE

No comments: