ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 24, 2012

Kinana azungumzia urais



Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewatisha makada wake kwa kuwaeleza kuwa kitamtosa bila kumuonea haya mwanachama yeyote atakayeomba kuteuliwa kugombea urais mwaka 2015 huku akiwa kinara wa kutegemea makundi ya kumwigiza katika nafasi hiyo.
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Abdulrahman Kinana, alisema badala yake CCM itahakikisha mgombea inayemsimamisha ni mwanachama asiyeendekeza makundi, mwadilifu ambaye kila akiteuliwa atakuwa hatiliwi shaka.
Alitoa kauli hiyo jana wakati akijibu swali la mmoja wa wana-CCM katika mkutano wa shina la Isesa mkoani Rukwa, akiwa katika ziara ya kujitambulisha na sekretarieti mpya na kueleza usimamizi na utekelezaji wa ilani ya CCM.
Jibu hilo lilitokana na mwanachama huyo, Peter Lilata kutaka kujua CCM imejiandaa vipi kuhakikisha katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 inateua mgombea ambaye atakubalika na wananchi wengi, na kutofanya kosa kuteua mgombea ambaye hakubaliki kwa maelezo kuwa kufanya hivyo kutakisababishia chama usumbufu katika kupata ushindi.

Kinana hakuwataja vinara wa makundi, lakini baadhi ya makada wamekuwa wakitajwa kuwa na nia ya kugombea urais mwaka 2015.
Baadhi ya wanaotajwa ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye. Hata hivyo, hakuna aliyewahi kuthibitisha kuwa atagombea zaidi ya kusema kuwa watafanya hivyo kuda ukifika.
Mapema akizungumza baada ya kuzindua shina hilo, Kinana aliwataka viongozi wa CCM kuonyesha mfano wa ujenzi wa Chama kwa kutembelea ngazi za mashina na matawi.
“Kuanzia sasa tutawapima viongozi wetu kwa namna wanavyokuwa wepesi kutembelea mashina na matawi ya CCM kwa sababu utaratibu huu ndiyo pekee utakaokiimarisha Chama, na si vinginevyo,” Kinana na kuongeza:
“Kutokana na kutambua hilo na kwa kuwa ni maelekezo yaliyotokana na maazimio kwenye Mkutano wetu Mkuu uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, ndiyo sababu baada ya kupatiwa wadhifa huu mimi na wenzangu tumeanza ziara hii, na kila ninapofika lazima nitembelee mashina na matawi ili kuwa mfano kwa viongozi wengine.”
Akizungumzia rushwa na mizengwe katika uchaguzi, aliwataka wana-CCM kuhakikisha kuwa katika kila chaguzi wanahangaika kuunga mkono wagombea ambao ni watendaji wazuri na wenye maadili safi badala ya kukumbatia wanaowapa rushwa.
“Lazima mjue kwamba mnapoamua kumchagua mgombea anayewapa rushwa, mnafanya kosa kubwa sana kwenu, maana akishapita anakuwa kiongozi wa kutetea maslahi yake na siyo yenu,” alisema Kinana.
Aliwataka wana-CCm kuacha kutungiana fitina, mizengwe na kuacha makundi kila baada ya chaguzi kwa sababu mambo hayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kudhoofisha mshikamano na umoja ndani ya Chama.
Aidha, Kinana amewahakikishia Watanzania, hususani wanachama wana-CCM kwamba yupo tayari kuhakikisha anatekeleza kwa ufanisi mkubwa majukumun makubwa aliyopewa.
“Ni kweli nilikuwa nimetangaza kustaafu siasa kwa kuzingatia kwamba nimeshashika kwa muda mrefu nyadhifa za kuchaguliwa, nikaona kwamba kama wenzako wameshakuamini mwa muda mrefu ukafanya nao kazi wakikupenda, basi usisubiri mapaka uchokwe ndiyo uondoke,” alisema na kuongeza.
“Lakini sasa baada ya maamuzi yangu, Mwenyekiti wa Chama Chetu, Rais Jakaya Kikwete akaamua kwa kadiri alivyoona inafaa, akaniteua nikisaidie Chama. Kwa mtu mwenye hekima na uadilifu unapoteuliwa na Mwenyekiti wa Chama chako, tena Rais wa Chama kinachotawala, lazima ukubali tena bila kinyongo, nikakubali.”
“Sasa baada ya kuwa mimi ndiye Katibu Mkuu wa Chama hiki, napenda kuwaambia kwa dhadi ya moyo wangu kwamba nipo tayari, kimwili, kiakili kuhakikisha nawatumikia Wana-CCM na watanzania kwa jumla kwa weledi na ufanisi mkubwa,” alisema.
Kinana anafuatana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Katibu wa Oganaizesheni, Mohamed Seif Khatib na baadhi ya mawaziri.
‘TUITANE NDUGU’
Katika hatua nyingine, Kinana ameagiza kuanzia sasa wanachama wa CCM kuacha kuitana waheshimiwa badala wake watumie jina la ndugu kama alivyoasisi Mwenyekiti wa kwanza wa CCM, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
“Katika maisha yangu yote ya kumfahamu Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere, sikupata kumsikia akijiita au akitaka aitwe Mheshimiwa Mwenyekiti, au Mheshimiwa Rais, sasa haya mambo ya sisi kuitama mheshimiwa tunayatoa wapi?” alihoji Kinana.
Alisema, Mwalimu Nyerere hakujiita mheshimiwa kwa sababu ina maana kubwa sana, kwa hiyo ni lazima Wana-CCM kuendelea utamaduni huo wa kuitaka ndugu kwa sababu unazuia matabaka ya ubwana na utwana.
CHANZO: NIPASHE

No comments: