ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 20, 2012

MAISHA NDIVYO YALIVYO

 "Nilisalitiwa wakati wa uchumba hadi sasa sina amani:"

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita nilikuletea kisa cha jamaa aliyekuwa akimlipizia kisasi mkewe eti kwa fumanizi kabla ya kuoana. Matoke yake akawa anasulubu mahausigeli kama hana akili nzuri. Tusikie maoni ya wadau, kisha tupate kisa kingine kilichobeba kichwa cha maneno hapo juu.

Msomaji huyu anasema; Mh! Ama huyu ndio ana kisasi cha masafa marefu. Sijui huyu mwenzetu ni muumini wa dini gani asiyeweza kusamehe na kufanya watoto wa wenzake ndio ndio dampo la kutupia taka na ni bora angelipiza kwa njia nyingine. Je, haogopi magonjwa. Hapo upendo hakuna bora huyu dada ajifikirie mara mbili. Maana majibu yenyewe kama msumari

Kwa kweli wanaolipiza kisasi ni wanawake zaidi ya wanaume. Maana mwanaume yeye akikufuma atakufukuza moja kwa moja bila kuangalia tatizo liko wapi. Ila mwanamke yeye hawezi mfukuza mumewe ila atajitahidi alipize ili kukonga moyo wake. Kwa upande wangu naona tusilipize kisasi bali tumuombe Mungu. (Mama Lulu, Kitunda).
Msomaji mwingine ametoa maoni kwamba; “Ukiona jamaa analipiza kisasi kwa tukio la siku nyingi, basi ujue huenda hata wakati huu wakiwa ndani ya ndoa bado anazo tetesi kwamba mkewe huyo bado kwa siri anatoka na washikaji hao wa zamani. Si unajua tena’ mavi ya kale hayanuki’? Kule kujikumbushana kwa wengine ni jambo ambalo halikwepeki, watatafuta uchochoro tu ili wafurahishane.

“Hata ingekuwa ni mimi, lazima ningehisi mke wangu kuendeleza mahusiano na washikaji niliokuwa wanapamba wakati wa uchumba. Ila tabia hiyo ya mumewe kupepesa macho kwa mahausigeli, tena mbele zake na wakati mwingine kumfumania live ni jambo lisilokubalika.

“Huo ni ushenzi unaokera. Labda kama hata baada ya kumuoa mwanamama huyo, aliwahi kumfumania tena. Kama sivyo, basi hana sababu ya kumuumiza mkewe eti analipiza kisasi. Mashindano ya aina hii ndiyo yanayoangamiza familia kwani hanja hanja hiyo ndiyo inayozoa maradhi mabaya ikiwemo ukimwi.(Msomaji Moro).

Msomaji mwingine ujumbe wake unasomeka; “Mimi naitwa Mahamed Haruna Nsheshe naishi Mburahati Barafu Dar. Mimi maoni yangu nasema hivi endapo yatatokea mambo ya kufumaniana ubora ni kuachana kwa sababu mapenzi ni raha ikiingia karaha nyumba inakuwa haina furaha, nyumba inakuwa haina baraka hata kidogo”.

Mpenzi msomaji, hayo ni baadhi ya maoni ya wasomaji wetu kuhusiana na mada ya wiki iliyopita iliyobeba kichwa cha maneno “Nani mwenye visasi kati ya mwanamke na mwanaume?”. Bila shaka bado wengine wanatafakari swali hilo na atakayekuwa tayari atujibu kupitia ujumbe mfupi wa simu au email iliyoko mwishoni mwa makala haya.

Wakati tukisubiri maoni hayo, tumsikie mwenzetu mwingine aliyetoa dukuduku lake kuhusu mkewe kumuomba radhi kwa jambo fulani alilofanya, ambalo hadi sasa linamuumiza sana roho. Ujumbe wake mfupi kwa simu ya kiganjani ulisomeka namna hii;

…..Habari, pole na kazi. Nimekuwa nafuatilia mara nyingi kuhusu makala yako. Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 24 nipo kwenye ndoa yapata miaka miwili sasa. Tumebahatika kupata mtoto mmoja. Kitu kinachonisumbua ni kwamba kuna siku mke wangu aliniomba radhi kuwa kuna kitu ambacho alifanya kipindi tukiwa wachumba, lakini mpaka sasa roho haina amani kwa kitendo alichokifanya. Alinisaliti kwa hiyo ananiomba msamaha na mimi nilikuwa sijui na sijawahi kumhisi kitu kama hicho. Alivyonieleza niliishiwa nguvu na kushindwa hata nimjibu namna gani.

Kwa kifupi kuna siku nilirejea kutoka kazini nikamkuta hana furaha kama kawaida yake ikambidi nimuulize kulikoni akajibu kuna kitu anataka kunieleza kama nipo tayari kumsamehe.

Ndipo akaniambia enzi za uchumba alinisaliti haikuwa kusudio lake alishawishiwa na rafiki yake ndio maana kila akikaa akikumbuka anakuwa hana amani akaona bora aombe msamaha.Naombeni maoni yenu wadau(Msomaji -jina linahifadhiwa kwa sasa) .

Mpenzi msomaji, kijana huyu baada ya kuona bado yapo maswali kwenye ujumbe wake, ilibidi nimpigie simu kutaka ufafanuzi na yafuatayo ndiyo yalikuwa majibu yake.

Swali: Ni kosa gani hilo lililokufanya ujisikie vibaya na kushindwa kujibu hata msamaha wa mkeo?

Jibu: Sijui nikuelezeje. Yaani yupo best (rafiki) yake ambaye alikuwa akimfundisha mambo ya kihuni na akawa anamwambia asinipende mimi. Sasa nikifikiria najisikia vibaya kwani angalau angeniambia wakati ule.

Mpenzi msomaji, hata hivyo, nilimpa ushauri ufuatao kwamba maadam amemuomba msamaha basi amsamehe mara sabini. Tena ni mwanamama mzuri kwani angeweza kukaa kimya bila kumwambia kilichotokea wakati ule wa uchumba lakini kutokana na upendo kwake akaona asafishe nafsi yake kwa kuomba msamaha.

Kijana huyu alishukuru kwa ushauri huo na akasema atakwenda kumwangukia mkewe yaishe wasonge mbele kimaisha na kulea mtoto wao kwa amani.

 Je, msomaji wangu, nawe una ushauri gani kwa kijana huyu? Au unacho kisa tujadili pamoja? Ukiwa tayari kwa maoni, ushauri kuwa huru kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 774268581(usipige), au barua pepe; HYPERLINK "mailto:fwingia@gmail.com" fwingia@gmail.com

No comments: