ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 20, 2012

HUKUMU YA FUNDIKIRA YAZUA KILIO MAHAKAMANI, WENGINE WAZIMIA!



Wauaji Ali na Mohamed wakitolewa kutoka ndani ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo baada ya kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua Swetu Fundikira..
Wanajeshi watatu waliokutwa na hatia ya mauaji na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa leo.
Marehemu Swetu Fundikira ambaye aliuawa na wanajeshi wa JWTZ.


Wale askari watatu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji dhidi ya Swetu Fundikira ambaye ni mtoto wa kigogo wa zamani wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa leo baada ya kukutwa na hatia kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Waliokumbwa na hukumu hiyo ya kunyongwa hadi kufa iliyotolewa na Jaji Zainabu Miruke ni Sajent Rhoda Robert, Koplo Ally Ngumbe na Mohamed Rashid. Marehemu Swetu alikuwa ni mtoto wa Chifu Abdallah Said Fundikira, mmoja wa viongozi wa juu katika serikali ya awamu ya kwanza ya Tanzania.
Watu kibao walifurika kwenye ukumbi wa mahakama kuanzia mishale ya saa 2:00 asubuhi kusikiliza kesi hiyo iliyokuwa gumzo.
Jaji Zainab aliingia mahakamani mishale ya saa 4:45 kabla ya kuanza kusoma hukumu hiyo. Akasema washitakiwa wanatuhumiwa kwa kosa la mauaji ya kukusudia.
Jaji akaongeza kuwa Oktoba 5, 2011, washtakiwa walifikishwa mahakamani hapo na waliposomewa mashitaka yao na maelezo ya awali, walikana na kukubali tu kwamba majina na vyeo vyao jeshini ndivyo vilivyokuwa sahihi.
Mashahidi sita waliitwa na upande wa Jamhuri na ikathibitika kupitia maelezo yao kuwa kweli, washtakiwa walifanya mauaji ya kukusudia dhidi ya Swetu.
Jaji Zainab akaongeza kuwa mbali na maelezo ya ushahidi, upande wa mashitaka ulitakiwa pia kuthibitisha mambo manne ambayo ni kufa kwa Swetu, kufa kwa Swetu kwa kifo ambacho si cha kawaida, kuhusika kwa washtakiwa katika kifo hicho na pia kuieleza mahakama kama washtakiwa waliua huku wakiwa na nia ovu.
Jaji akasema kuwa upande wa Jamhuri ulipaswa kuithibitishia mahakama namna nia ovu ilivyotumika ikiwamo kueleza kama washtakiwa walitumia silaha, aina ya silaha waliyotumia, nguvu iliyotumika ili kutimiza nia ovu, tabia ya washtakiwa kabla na baada ya tukio na majeraha mangapi walimsababishia marehemu.
Akasema katika maelezo ya shahidi wa nne ambaye ni daktari aliyechunguza mwili wa marehemu, ilithibitika kuwa Swetu alikufa kutokana na majeraha yaliyotokana na kupigwa na kitu chenye ncha kali.
Hata hivyo, Jaji Zainab akasema hakukuwa na shahidi aliyethibitisha kuwa aliwaona washtakiwa wanavyomuua Swetu, bali mashahidi watatu walithibitisha kuwaona washtakiwa wakiwa na Swetu kabla ya kukutwa na umauti.
Akasema ushahidi wa mazingira unatakiwa uwe kwenye mtiririko ambao utatoa jibu moja, na ndivyo ushahidi ulivyoonesha kuwa washtakiwa walimuua Swetu kutokana na mazingira ambayo ushahidi wake ulikuwa mmoja dhidi ya washtakiwa.
Jaji akasema kuwa kwenye kesi hiyo, ushahidi wa mazingira umeowanyooshea kidole washtakiwa moja kwa moja, wanahusika na mauaji hayo na hivyo akawatia hatiani na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa
Kabla Jaji Zainab kutoa hukumu yake, wakili wa utetezi, Kaloli Mluge, aliomba mahakama iwahurumie kwa kuwapunguzia adhabu kwani umri wao ni mdogo na bado wanahitajika kwa ujenzi wa taifa na pia familia zao.
Hata hivyo, Jaji Zainab akasema kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu, pasi na kuacha shaka, mahakama imewatia hatiani washtakiwa na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa.
Washtakiwa walidaiwa kutenda kosa hilo Januari 23, 2010, mishale ya saa 7:30 usiku katika barabara ya Mwinjuma, eneo la Kinondoni jijini Dar es Salaam. Walifikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Januari 27, 2010, mbele ya Hakimu Mkazi, Genivitus Dudu kwa usikilizwaji wa awali. Upelelezi ulipokamilika, kesi hiyo ikahamishiwa kwenye Mahakama Kuu. 
Wakili wa upande wa uetetezi uliokuwa na mashahidi watatu, Mluge, alisema kuwa hajaridhika na hukumu ya Jaji zainab na hivyo watakata rufaa.
Washtakiwa walimuua kwa makusudi Swetu Januari 23, mwaka 2010, saa 7:30 usiku Kinondoni katika barabara ya Mwinjuma.

No comments: