ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 20, 2012

MAPENZI BORA HUPITIA KATIKA MZANI, JIFUNZE KUPIMA NA ‘KUBALANSI’-4


KUNA MABADILIKO?
Vema kujiuliza swali hilo na matawi yake. Hii itakusaidia kutanzua mambo ambayo yanaweza kusababisha uhusiano wenu ukaenda na maji hapo baadaye.

* Kuna kiasi cha mabadiliko kwa kila mmoja wenu tangu mlipokutana kwa mara ya kwanza?
* Bado unachangia na mwenzi wako kila kitu chenu kama ambavyo mlifanya wakati mnaanza kupendana?
* Kinatokea nini pale kila mmoja hufanya mambo anayojisikia mwenyewe?
* Una muda kiasi gani kutumia na mwenzi wako? Je, unajihisi upo kwenye uhusiano imara na wenye mafanikio? Jiulize, inamaanisha nini kuwa na masilahi tofauti kati yako na mwenzi wako?
* Umewahi kutafakari na kugundua kwamba wewe na mwenzi wako, kila mmoja ni mtu huru lakini mmeamua kuwa pamoja au zipo dalili za kifungo?
* Je, unaamini mapenzi ni kujitoa mhanga? Kama ndivyo ni kwa nini?
JADILI MASWALI HAYO NA MWENZIO
Lazima maswali hayo uyapatie majibu, si kwa wewe peke yako bali kwa kushirikiana na mwenzi wako. Kama kuna sehemu yenye utata basi haraka sana, mnaitolea macho na kuondoa tofauti. Hakikisha kila kitu kinakuwa chanya.
Hata hivyo, pengine kila unapoweka mezani ‘ishu’ ya kujadili inageuka ubishi. Ndani ya ubongo wako, unaamua kuachana na ‘topiki’ hiyo kwa lengo la kuepuka migogoro. Unahisi mbele ya ubishi kuna ugomvi, nawe hupendi kugombana kwani inaweza kuhatarisha mapenzi yenu.
Hata hivyo, kuacha kujadili jambo ambalo linawatofautisha ni hatari zaidi, hivyo ni busara kutafuta meza ya mazungumzo kwa namna yoyote ile. Ni kosa kubwa kuwa na masilahi tofauti kwenye mapenzi. Mnaweza kutofautiana mambo mengine lakini siyo hilo.
Mathalan, wewe unaamini kwamba mpenzi uliyenaye kwake ndiyo umefika, yeye hilo halipo akilini. Unawaza ndoa mwenzako anakutafsiri kama ni wa kuzugia. Uhusiano wa namna hiyo haupo sawa, una matege, haufai kuendelea kujengwa. Unaweza kumrekebisha, kama habadiliki, ni bora ukimbie.
Vema ukajiuliza mwenyewe, ni muda gani utaishi na mtu ambaye hana mpango na wewe. Kila ukianzisha mada ya ndoa anakuwa mkali. Lazima wote muwe na masilahi ya aina moja, nyote mtamani kuoana, hapo mtaweza kufika, vinginevyo utakuwa unajenga, mwenzako anabomoa.
Kama nilivyotaka ujiulize hapo juu, kwamba wewe na mwenzi wako kila mmoja ni mtu huru. Hii inamaanisha kuwa mapenzi siyo kifungo. Unapaswa kumuacha aamue mwenyewe kuhusu hatma ya mapenzi yenu. Ukionekana unambana, anaweza kufanya mambo kukuridhisha lakini kuna siku atakuadhiri.
Baadaye anaweza kuthubutu kukwambia: “Sikutaka kufunga ndoa na wewe, sema tu ulinilazimisha.” Kauli hii ni tusi, endapo utaitafakari kwa mlengo kuwa uliyenaye hana mapenzi ya dhati nawe. Hata kuwa naye ni kama umemlazimisha.
Tafakari kisha upate jibu kwamba mwenzi wako hana hisia na wewe. Huo ndiyo ukweli kwa maana mapenzi ni hisia. Kama mwenzi wako anakupenda, maana yake ana hisia juu yako, baada ya hapo sasa tafsiri kinyume chake. Unaweza kujiona mdogo kama piritoni.
Hutakiwi kufika huko, vema ujiwekee utaratibu wa kutafakari kila hatua ya uhusiano wako. Kuna maswali mengi ambayo nimekutaka ujiulize. Hayo yatakusaidia kukupa picha ya uhusiano wako ulipo na unapoelekea.
Si kukimbilia kuachana au kuvumilia yasiyovumilika kwa kudhani mwenzi wako atajirekebisha. Bila dira, hutafanikiwa. Vema ujue kuwa hakuna ugumu kwenye mapenzi kama utajifunza na kuyaelewa kikamilifu.

CHANZO:GPL

No comments: