ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 2, 2012

Mbunge amcharukia waziri Bungeni

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema (kulia) akimsikiliza Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge walipohudhuria kikao cha Bunge, mjini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi

Mwandishi Wetu, Dodoma
MBUNGE wa Tunduru Kusini, Mtutura Abdallah Mtutura (CCM) jana aliibana Serikali na kuitaka kuacha kutoa majibu ya uwongo ambayo yanapatikana kutoka kwa watuhumiwa.
Mtutura alitoa kauli hiyo baada ya kutokubaliana na majibu ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kuhusu kukanusha kuwa wananchi wa Tunduru hawateswi wala kupigwa wanapoingia kuvua samaki kandokando ya Mto Ruvuma.

“Mheshimiwa Spika, hivi itakuwaje kama nitaleta ushahidi hapa kuwa wananchi wanapigwa, wanateswa na kuporwa mali zao pindi wanapoingia katika maziwa na bahari kwa ajili ya kuvua samaki tu,” alihoji Mtutura na kuongeza.
“Maana ninachoona hapa ni kuwa Naibu Waziri amekuja na majibu ambayo kwa vyovyote ameyapata kutoka kwa watuhumiwa wa jambo hilo ndio maana anajibu hivyo majibu ambayo sikubaliani nayo.”
Katika swali la msingi Mbunge huyo alitaka kujua kwa nini wananchi wa Vijiji vya Wenje, Nasomba Makande, Kazamoyo, Misechele na Meyamtwaro vilivyo kandokando ya Mto Ruvuma wanasumbuliwa na askari wa maliasili kwa kupigwa na kunyang’anywa mali zao wanapovua samaki kama kitoweo.
Naibu Waziri alisema kuwa kutokana na wananchi wengi kuharibu mazingira kwenye maeneo ya wazi, kumesabisha upatikanaji mdogo wa samaki na hivyo hulazimika kuingia kwenye pori la Mwambesi kinyume na sheria na kuvua samaki huko.
Alisema wananchi hao wanapokutwa katika maeneo hayo, hukamatwa na kikosi cha doria na kupelekwa katika kituo cha Polisi kama taratibu za nchi zinavyoelekeza.
Hata hivyo alibainisha kuwa yapo matukio kadhaa ambayo hubainika kwa kisingizio cha kuvua samaki, lakini wananchi wanaingia na kufanya ujangili ndani ya hifadhi.
Waziri alilieleza kuwa Bunge kuwa hali ya ujangili hivi sasa ni kubwa nchini na majangili wengi huingia ndani ya hifadhi kwa lengo baya huku wakiwa na silaha nzito zikiwamo za kivita hivyo ni vema hata askari wa wanyamapori kuwa makini na jambo hilo.

Mwananchi

No comments: