KAMPUNI ya Reli Tanzania (TRL), imesema kwa sasa imeelemewa na wingi wa abiria katika usafiri ulioanzishwa wiki hii kiasi cha kushindwa kuwahudumia kwa mara moja.
Imesema kwa kuzingatia hali hiyo imepanga kuanzisha safari za treni mpya haraka iwezekanavyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ofisa Uhusiano wa TRL, Midladjy Maez, alisema wameshangazwa na mwitikio wa wananchi kuhusu usafiri huo na kwamba sasa wako kwenye mikakkati ya kuongeza treni nyingine ya abiria, ili hatari ya abiria kuning’inia milangoni.
“Wakandarasi wapo katika mchakato wa matengenezo wa vituo viwili vya kubadilishana treni, vikikamilika kutakuwa na treni mbili zitakazofanya kazi,” alisema Maez.
Alisema mabehewa yaliyotengwa kwa ajili ya usafiri wa jijini yapo 14 na kwamba yanayotumika kwa sasa ni sita tu.
Alisema maeneo ambayo yatatumika kubadilishana kwa treni hizo ni Buguruni Mnyamani na Ubungo Maziwa na kwamba huduma ya treni inasaidia wananchi wengi.
Alisema wananchi hawapaswi kuning’inia milangoni kwa sababu kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha.Kwa upande wa abiria wanaotumia usafiri huo , wameiomba TRL kuongeza mabehewa ili kukidhi mahitaji.
“Nimeshindwa kupanda kama unavyoona treni imejaa sana, watu wamesimama mpaka mlangoni hamna hata sehemu ya kusimama na tiketi nimeshakata, itabidi nisubiri hapa hapa iende ikirudi nipande niende Ubungo,”alisema abiria aliyejitambulisha kuwa ni Hamisi.
Alisema upungufu wa mabahewa unasababisha abiria kupanda bila utaratibu huku wakisukumana milangoni.
“Wengine tunaamua kupanda treni kutokana na kuchoshwa na fujo za daladala na foleni lakini kuna watu wanaamua kupanda treni, ili kujifurahisha”alisema abiria mwengine aliyejitambulisha kwa jina la Aisha.
Changamoto nyingine iliyojitokeza katika usafiri huo ni kukosekana kwa vibao vinavyoonyesha mwelekeo wa vituo vya treni, hali inayosababisha abiria wengi kukosa huduma.
Hali hiyo ilijitokeza jana katika maeneo ya Ubungo ambapo abiria wengi walionekana kuulizia vituo v ya treni.Moja ya abiria ambaye hakutaka jina lake litajwe alishauri kuwepo kwa vibao pembezoni mwa Barabara ya Mandela hasa karibu na kituo cha gesi cha Songas na maeneo ya barabara ya Morogoro karibu na kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo.
Vibao hivyo vitawasaidia wageni kuweza kupata huduma ya treni.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment