ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 26, 2012

Michoro ya kampasi ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kinachojengwa Mloganzila



Michoro ya ujenzi wa Kampasi ya Mloganzila iliyo kijijini Kwembe  katikati ya Wilaya za Kisarawe Mkoa wa Pwani na Kinondoni Mkoa wa Dar es salaam. Hii ni sehemu ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili
  (MUHAS) inayojengwa kwenye eneo la ekari 3800 kwa ajili ya kutolea mafunzo kwa wanafunzi wa udaktari na huduma za Afya wapatao 15,000 kwa mwaka, na pia itakua sehemu ya kutolea matibabu ya maradhi yote makuu na ya kawaida nchini. 


 Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, ujenzi  wa Hospitali hii, ambayo pesa ya ujenzi wake imeshapatikana, unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Januari, 2013 na unatarajiwa kukamilika miaka miwili baada ya ujenzi kuanza. Kwa maneno mengine Kampasi ya Muhimbili ya Mloganzila inategemewa kuanza kazi mwanzoni mwa mwaka 2015.

Tayari wataalamu na wafanyakazi wanaotarajiwa kufanya kazi katika kampasi ya Mloganzila wameshaanza mafunzo ndani na nje ya nchi. Mara hospitali hiyo kubwa na ya kisasa itakapokamilika itakua na uwezo wa vitanda vya kulaza wagonjwa mia sita (600). 

Sambamba na kampasi ya MUHAS ya Mloganzila pia ujenzi wa Kampasi ya Afya ya Chuo Kikuu cha Dodoma  (UDOM)  umeshaanza na kufikia hatua ya juu na ambapo pia hospitali  hiyo inatarajiwa kuanza shughuli zake rasmi mwaka 2015.

Kwa mujibu wa  Mkurugenzi wa Mfuko wa Afya ya Jamii (National Health Insurance Fund) NHIF Bw. Emmanuel Humba mchakato wa  kufanikisha uanzishaji wa Chuo Hospitali hiyo vimeshaanza ambapo baadhi ya wataalamu wakiwemo Madaktari na watumishi wengine wako nchini na nje ya nchi kwa ajili ya masomo na mafunzo mbalimbali.

Chuo hicho kinatarajia kuwa na vifaa vya kisasa vya tiba vinavyokidhi mahitaji ya Afya na Elimu ya Udaktari wa kiwango cha Kimataifa, ikiwa ni mikakati kabambe ya serikali ya awamu ya nne katika kuhakikisha nchi ina wataalamu wengi na huduma za kisasa za afya ili kuondokana na adha ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Kwa sasa MUHAS inachukua takriban wanafunzi 2442 wa udaktari na huduma za afya kwa mwaka. Hivyo ujio wa kampasi ya Afya Mloganzila na Kampasi ya afya ya UDOM   utaharakisha mpango wa serikali wa kupunguza wastani wa wagonjwa  kwa daktari mmoja kwa kiwango kikubwa. Hivi sasa wastani ni daktari mmoja anahudumia wagonjwa 30,000. 

No comments: