ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 1, 2012

Ruksa wafanyakazi kupata mafao ya kutoka mifuko ya jamii

Julius Magodi, Dodoma
SERIKALI jana iliwasilisha tamko bungeni kurejesha kwa fao la kujitoa katika mifuko ya jamii, ambalo liliondolewa na Mamlaka ya Kusimamia na Kudhibiti Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Agosti mwaka huu.
Akiwasilisha tamko hilo bungeni jana, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka alisema kwa kuzingatia mchakato ulioanza wa kuangalia upya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii, SSRA imeliondoa agizo la kuzuia mifuko kutoa fao la kujitoa.

Alisema kufuatia hatua hiyo , mifuko yote itaendelea kutoa fao hilo kama ilivyokuwa kabla ya zuio hilo na kwa vigezo vilevile kwa wanachama wanaostahili kupata fao hilo.

Waziri huyo alisema Serikali inaandaa muswada wa sheria wa kufanyia marekebisho sheria ya mifuko ya jamii sambamba na kuondoa katika muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali sehemu inayohusu fao la kujitoa.

Alisema kabla ya kuandaa muswada huo, Serikali itafanya majadiliano na wadau wote wakiwamo wabunge, vyama vya wafanyakazi, waajiri na wananchi.

Juzi SSRA ilitoa taarifa ya kufuta tamko lake la kuzuia fao la kujitoa kwa wanachama wa mifuko ya jamii nchini.

“Mamlaka ya Usimamazi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), inapenda kuufahamisha umma kufutwa kwa tangazo lililotolewa na mamlaka Agosti 2012 kwenye vyombo mbalimbali vya habari lililohusu kusitishwa kwa fao la kujitoa,” ilisema sehemu ya taarifa ya SSRA.

Pamoja na maelezo hayo, taarifa hiyo pia ilieleza kuwa uamuzi huo unaendana sambamba na hatua za Serikali za kuendelea na utekelezaji wa azimio la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kikao cha nane kilichoazimia pamoja na mambo mengine kuirejesha sheria ya hifadhi ya jamii.

Mwananchi

No comments: