SHIRIKA la Nishati na umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Mbeya limewataka wateja wake wilayani Ileje waliotapeliwa na Mhasibu wa shirika hilo Emmanuel Ntahemuka kutoa taarifa Polisi kisha kumshitaki.
Wito huo umetolewa na Meneja wa Tanesco mkoa wa Mbeya John Bandiye alipokuwa akizungumza na wateja wa shirika hilo na waandishi wa habari waliofika katika ofisi za Tanesco wilaya ya Ileje wakati zoezi la kukata umeme na kukusanya mapato ya shirika hilo likiendelea.
Bandiye alisema hayo baada ya wateja kulalamikia utaratibu wa shirika hilo kukata umeme bila taarifa kwa madai kuwa wateja hao wanadaiwa madeni mengi huku wao wakiwa wamelipa na kupewa stakabadhi ambazo zinadaiwa kuwa ni za kugushi.
Meneja huyo alisema kuwa lengo la shirika lake si kukata umeme bali ni kukusanya mapato na kwamba tayari baadhi ya wateja kuelimishwa na kupewa ufafanuzi wameanza kulipa kwa makubaliano maalum kutokana na madeni yao kuwa makubwa.
‘’Lengo la Shirika siyo kukata umeme bali ni kukusanya mapato yake ambayo hayajalipwa kwa muda mrefu na malipo mliyokuwa mnalipa hayakuwa yanaingia kwenye mtandao wa Shirika na ndiyo maana hata mihuri ya stakabadhi siyo ya mashine mhasibu mliyekuwa mnampatia fedha mpaka sasa tumemsimamisha kazi kwa ajili ya uchunuzi na anayetaka kumshitaki ni ruksa na sisi tutawasaidia ili akamatwe na Polisi’’ Alisema Bandiye.
Alisema Ntahemuka amesimamishwa kazi kwa ajili ya uchunguzi na hatua zingine zitachukuliwa dhidi yake pamoja na wenzake.
Mbali na hayo ameomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kwa wateja wote na kwamba kuanzia sasa wateja wenye shida wafike katika ofisi hiyo au wapige simu yake ya kiganjani ambayo aliitaja kuwa ni 0754 214499.
Jumla ya wateja 989 wa Tanesco wapo wilaya ya Ileje ambayo ni wilayailiyopo pembezoni mwa Tanzania mpakani na nchi ya Malawi.
Kwa hisani ya Gordon Kalulunga, Ileje |
No comments:
Post a Comment