ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 26, 2012

UNAPOPEWA, JIULIZE UNATOA NINI? USIENDEKEZE MAPENZI YA KIZAMANI -6

MDAU wangu, leo namalizia kuelezea mada hii inayohusu wapenzi kusaidiana na kuacha tabia ya mmoja wao kuwa na mkono wa birika. Tuwe pamoja.
Sabrina ni rafiki yake Gift, akaamua kuingilia kati, kumshauri Gift atambue umuhimu wa Khalid kwa sababu pale alipo asingefika kama siyo mwanaume huyo lakini ushauri huo ulionekana sawa na takataka.

“Sikiliza Sabrina, mimi ni msomi, daktari, natakiwa niwe na mwanaume msomi mwenzangu.”
Akaendelea: “Nilikuwa na Khalid kwa sababu alijipendekeza kwangu na alionesha anao uwezo wa kunisaidia. Nisingeweza kuacha hiyo nafasi lakini sasa hivi nimefanikiwa, Khalid kwangu wa nini tena? Ataniharibia tu maisha yangu. Lazima niyatengeneze maisha yangu kisomi.”
Gift alipoona msimamo wa Sabrina kwa Khalid umekuwa mkali, akimsisitiza anachokifanya siyo kizuri, alimjibu: “Hivi Sabrina, na wewe si mwanamke? Kama unamuona Khalid ni mwanaume wa maana sana, si uende akakuoe wewe? Tusisumbuane, kwanza yule siyo mwanaume wangu, sijawahi kutembea naye.”
Khalid alilia, machozi yakakauka, akaamua kuongeza juhudi kwenye biashara zake. Hatua zilikuwa ndefu na mafanikio yaliendelea kwa Khalid. Akafanikiwa kuanzisha maduka ya nguo, Dar es Salaam, Mwanza na Arusha. Vilevile akaanzisha biashara mbalimbali ambazo zilimfanya awe anasafiri kwenda nchi mbalimbali.
Kutokana na historia yake ya kukosa mke kwa sababu ya elimu, aliamua kutumia utajiri wake kuanzisha mfuko kwa ajili ya kuwasaidia vijana wa kiume kujiendeleza kielimu. Alifanya mambo mengi makubwa, ikiwemo kujenga majumba ambayo baadhi aliyafanya kuwa ofisi zake kwa ajili ya kuratibu biashara zake.
Khalid alipotaka kufunga ndoa, akamuona Sabrina ndiyo mke sahihi kwake. Japo mwanzoni ilikuwa ngumu kueleweka lakini baadaye kilieleweka. Gift aliposikia Sabrina na Khalid wamefunga ndoa, moyo ukamuuma sana, aliumia zaidi kwa sababu wanaume wasomi aliowataka walimtesa sana.
Hata hivyo, hiyo haikumuuma kama siku alipoomba kazi kwenye hospitali binafsi inayoitwa KS Health Centre bila kujua inamilikiwa na nani. Siku anaitwa kwenye usaili ndipo aliposhtuka, kugundua kwamba hospitali hiyo ni ya Khalid lakini inasimamiwa na mkewe (Sabrina) ambaye naye ni daktari.
Gift baada ya kufanyiwa usaili, aliondoka kichwa kikiwa kizito. Wakati yeye alikwenda kwenye usaili akiwa na taksi na kuondoka kwa taksi, kwa macho yake alimshuhudia Sabrina anaendesha gari la kifahari aina ya BMW X6 rangi ya chungwa.
Kwa haraka, Gift akaingiwa na mawazo kwamba kumbe maisha ya raha aliyonayo Sabrina, yangekuwa yake kama asingemdharau Khalid. Alimuona ni kijana aliyeishia kidato cha nne lakini ameweza kufanya mambo makubwa kumuwezesha kumiliki pesa na mali nyingi.
Mfano wangu una maana kuwa Gift ni mnyonyaji, alimuona Khalid ni daraja la kutimiza malengo yake kimaisha bila kuzingatia kwamba Khalid naye ni binadamu. Kumbe badala ya kumfanyia visa, kumnyanyasa, kumsimanga na kumdhalilisha kielimu, angeweza kushirikiana naye kujenga maisha bora.
Ingependeza kama Gift angeona umuhimu wa kutumia elimu yake kushirikiana na Khalid kujenga maisha lakini kwa sababu aliingiwa na ubinafsi, dharau kwa kumuona ni mwaume mbumbumbu, ndiyo maana baadaye akajuta. Ni sawa na mtu anayekumbuka almasi aliyoitupa, wakati akiwa bize anakusanya mawe.
Hakuna sababu ya kujuta baadaye, wala haitakiwa kuachana kisa mmoja amemuona mwenzake mnyonyaji, isipokuwa kila mmoja anapaswa kujiuliza na kupata jibu: “Ninapewa, je mimi natoa nini kwa mwenzangu?”

Chanzo:GPL 

No comments: