ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 2, 2012

Vituo vya mafuta Dar vyafungwa

Newstar Rwechungura na Suzan Mwillo
KUSHUKA kwa bei ya mafuta ya petroli na dizeli, kumepata taswira mpya jijini Dar es Salaam kwa jinsi mafuta hayo, yanavyoendelea kuwa kero kwa watumiaji wa huduma hizo.
Baadhi ya vituo vya kuuzia mafuta vimefungwa kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kukwepa hasara, inayotokana na kushuka kwa bei, kulikotangazwa mwanzoni mwezi uliopita.
Wakizungumza na Mwananchi jana, baadhi ya wasimamizi wa vituo vya kuuzia mafuta, walisema kuwa kazi imekuwa vigumu kwao kuuza mafuta kwa bei ya chini wakati shehena zilinunuliwa kwa bei ya juu.
Meneja wa Kituo cha kuuzia Mafuta cha Comel Oil ,kilichoko mikocheni, Truman Katowa, alisema Serikali inapaswa kuwafikiria wamiliki wa vituo hivyo kwa mafuta waliyonayo waliyanunua kwa bei kubwa na kwamba wakiuza kwa bei ndogo itakuwa hasara kwao.

“Hata mimi nikimaliza haya mafuta kidogo niliyonayo ,nafunga kituo mpaka hapo nitakapojipanga upya, ili kukabiliana na suala hili,”alisema Katowa.

“Ni bora wafunge vituo vyao kuliko kuendelea kupata hasara kwa kuuza mafuta kwa bei ambayo haina manufaa kwao,” alisisitiza.
Hata hivyo Meneja wa Kituo cha Engen, Raymond Kiama, alisema pamoja na kushuka kwa bei ya mafuta, hawezi kufunga au kuacha kutoa huduma kwa wateja wake kwa sababu bado anapata faida japokuwa ni kidogo.
Kwa upande wao, watumiaji wa mafuta walisema licha ya kushuka kwa bei, bado wanapata usumbufu wa upatikanaji wa mafuta kwa sababu vituo vingi vimefungwa na huduma zinapatikana katika vituo vichache.
Dereva wa bajaji Nsajigwa Issack, alilalamika kuwa mafuta hayapatikani kwenye vituo alivyo kuwa akinunua. “Ninaishi Mwenge lakini imenilazimu kuja Mikocheni kununua mafuta kwa sababu kule hayapatikani na vituo vimefungwa,”alisema Nsajigwa.

Mwananchi

No comments: