ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 1, 2012

Watuhumiwa mauaji ya Barlow kortini

Watu watano kati ya kumi waliokamatwa wakituhumiwa kuhusika na mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Mwanza.

Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Angelo Rumisha, na kusomewa shitaka la mauaji huku wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi waliokuwa na silaha za moto.

Waliofikishwa mahakamani ni Muganyizi Michael (36) mkazi wa Nyakabun;, Magige Marwa maarufu kama “Tatoo”(48), mkazi wa Bugarika; Chacha Mwita (50) mkazi wa Gongolamboto (Dar es Salaam);  Buganze, Edward Luseta (22), mkazi wa Tandika  na Bhokle Mwita (42) mkazi wa Mombasa Ukonga Dar es Salaam.

Mwendesha Mashtaka, Castus Ndamugoba, alidai kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Oktoba 13, mwaka huu majira ya usiku eneo la Minazi Mitatu Kitangiri wilaya ya Ilemela.

Hata hivyo, watuhumiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi za mauaji.

Watuhumiwa wengine watano akiwemo Mwalimu Doroth Moses Lyimo aliyekuwa na Kamanda Barlow wakati tukio  hawakufikishwa mahakamani.

Mbali na Mwalimu Doroth, watu wengine waliokuwa wakishikiliwa na kuhojiwa na polisi kuhusiana na mauaji ya Barlow, lakini hawakufikishwa mahakamani ni Felix Felician (50).

Wengine ni Philemon Felician maarufu kama “Fumo” (46) aliyewahi kuzichezea klabu za Pamba ya Mwanza na Yanga ya Dar es Salaam ambaye pia ni kaka mdogo wa Felix, Bahati Lazaro (28) na Amos Woibe Mabhoto maarufu kama “Bonge” (30), wote wakazi wa jijini Mwanza.

Watuhumiwa hao walireshwa rumande hadi Novemba 15, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
CHANZO: NIPASHE

No comments: