*Serikali yasema ni kelele tu
Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Imelda Urio, alitoa ushauri huo baada ya kupatiwa maelezo ya uzoefu wa uchimbaji wa madini hayo na wataalamu kutoka Ujerumani jana jijini Dar es Salaam.
Alitoa ushauri huo baada ya wataalamu hao kuthibitisha kuwa hakuna namna salama inayoweza kutumika katika uchimbaji wa madini hayo duniani kote.
Akifafanua juu ya athari hizo, Mwenyekiti wa Mtandao wa Uchimbaji wa Madini hayo kutoka Ujerumani, Gunter Wippel, alisema uchimbaji wa madini hayo ni wa gharama kwa kuwa unahitaji vitu mbalimbali, ikiwamo maji mengi.
Mbali na maji mengi, alisema pia unahitaji umeme wa kutosha na ardhi kubwa ambayo itatosha ili kunusuru wakazi wa maeneo, ambayo madini hayo yanachimbwa na madhara yanayotokana na uchimbaji huo.
“Madini haya yanapatikana juu ya miamba kwa asilimia 0.01. Kwa hiyo, madini mengi yanapatikana chini ya miamba. Hivyo, inabidi miamba ipasuliwe ili yapatikane. Na hutumia maji mengi kwa ajili ya kupasulia,” alisema Wippel na kuongeza:
“Tafiti zinaonyesha kuwa ukitumia maji ya chini ya ardhi kuchimbia madini hayo, baada ya miaka 40 kutakuwa hakuna maji asilia na hivyo kusababisha ukame kwa Taifa.”
Alisema uchimbaji wa madini hayo huleta madhara kutokana na vumbi linalochimbwa na mabaki ya madini kuwa na mionzi asilimia 80.
Wippel alisema kuwa mionzi hiyo inasababisha kansa na inasambaa kwa njia ya hewa na haraka hivyo kusababisha madhara kwa watu wengi na kwa muda mfupi.
Alisema mionzi ya madini hayo mbali ya kusababisha kansa, pia huua viungo vya uzazi kwa wanawake na wanaume, hivyo kusababisha kuzaliwa kwa watoto wasiokamilika viungo vyote au waliozidi viungo vya mwili.
Wippel alisema baada ya uchimbaji wa madini hayo, inahitajika kazi ya kufukia mashimo na kusawazisha maeneo yaliyotumika ili kupunguza athari, ambazo zinadumu kwa muda mrefu.
“Ujerumani imepata hasara ya zaidi ya Sh. Trilioni 14 kwa muda wa miaka 20 sasa kwa ajili ya kufanya marekebisho ya maeneo yaliyotumika kwa uchimbaji wa madini hayo, lakini bado hawajafanikiwa,” alisema.
Aliitaka serikali ya Tanzania kujifunza kwa nchi zilizochimba madini hayo na kufahamu madhara yanayotokana na uchimbaji huo kabla ya kuanza kwa zoezi hilo.
Pamoja na tahadhari hiyo, serikali mara kadhaa imesisitiza kuwa itaendelea na maadalizi ya kuchimba madini hayo.
Jana Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, alipoulizwa kuhusu tahadhari iliyotolewa na LHRC, alisema kuwa makelele ya kutaka kusitishwa kwa uchimbaji wa urani, yanashangaza sana kwani madini hayo hayajaanza kuchimbwa na kwamba, hadi sasa serikali haijapokea maombi yoyote ya kuyachimba.
Alisema watapokea maombi hayo hadi hapo watakapopata uthibitisho wa tathmini ya athari za kimazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (Nemc).
“Hatujaanza kuchimba urani. Hakuna sehemu yoyote nchini inayochimba urani,” alisema Masele.
Alisema kilichokwisha kufanyika ni tafiti, ambayo ndiyo iliyogundua kuwapo kwa madini hayo nchini, lakini bado hayajachimbwa.
Baadhi ya maeneo, ambayo madini hayo yamegundulika ni pamoja na Mkuju, Namtumbo, Mbuga za Selous, mkoani Ruvuma. Maeneo mengine ni Bahi, mkoani Dodoma, Manyoni (Singida) na Galapo (Arusha).
Naibu Waziri huyo alisema kazi ya Wizara ya Nishati na Madini ni kutoa leseni baada ya Nemc kufanya tathmini ya athari ya kimazingira.
Hata hivyo, alisema kinachotarajiwa kuchimbwa nchini ni malighafi, ambayo kwenye ardhi ya Tanzania ipo na haijaleta madhara yoyote.
“(Wilayani) Bahi (mkoani Dodoma, hiyo malighafi) ipo. Niambie watu wangapi wamekufa na wanachota maji kwenye visima?” alihoji Masele.
Kutokana na hali hiyo, alisema kuna haja kwa wataalamu kutoa semina ili kuwasaidia wananchi kujua ukweli kuhusu madini hayo.
Pia Masele aliwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kujiamulia mambo yao wenyewe, badala ya kuendelea kutegemea watu kutoka nje.
Alisema makelele yanayopigwa kuhusu urani, yanaashiria kuwapo vita na mvutano mkubwa baina ya mataifa makubwa duniani, ambayo kila moja ‘linayamezea mate’ madini hayo nchini.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment